Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mohamed Gharib Bilali, akizungumza na Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PPF kanda ya kusini, Kwame Temu, alipokuwa akikaguwa mabanda ya maonyesho katika kilele cha maadhimisho ya siku ya bahari Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Mtwara jana. |
Na Juma Mohamed.
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mohamed Gharib Bilali, amesema serikali ipo katika jitihada za kuboresha elimu na mafunzo katika fani za usafiri wa majini ili kukidhi mahitaji ya sekta hiyo kitaifa na kimataifa.
Akizungumza jana katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani, yaliyofanyika kitaifa mkoani hapa, alisema ili sekta ya usafiri wa majini na bandari iweze kuendelea, kuna haja ya kuwa na wataalamu wa kutosha, na kwamba mfumo wa mafunzo na utoaji elimu ya ubaharia unapaswa kufuatwa kwa lengo la kufikia viwango vya kimataifa.
“Mafunzo yenye viwango, yatasaidia kufanya uwezo wa mabaharia wa Kitanzania kutambuliwa na kupata ajira si tu kwa meli za hapa nchi, bali pia katika meli kubwa za Kimataifa..” alisema.
Alisema, kutokana na uwepo wa miradi ya utafutaji wa gesi na mafuta katika ukanda wa kusini ambayo inatoa fursa nyingi za ajira kwa mabaharia kupitia bahari ya Hindi, vyombo vinavyotumika vinahitaji nguvukazi za kuviendesha na kuvihudumia ambapo Watanzania wenye ujuzi na elimu ya ubaharia wana fursa kubwa ya kupata ajira katika vyombo hivyo.
“Hali hii imehamasisha serikali yetu kuendelea kuchukua hatua za kuboresha uendeshaji na utoaji huduma za usafiri majini hapa nchini..hatua hizo ni pamoja na kuanzishwa kwa chuo cha bahari cha Dar es Salaam (DMI) mwaka 1991, kutungwa kwa sheria ya usafiri wa majini ya mwaka 2003 na kanuni zake pamoja na kutungwa kwa sheria ya usafiri baharini ya mwaka 2006 ya Zanzibar na kanuni zake..” alisema.
Awali akitoa taarifa ya mkoa, mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, alisema serikali ya mkoa ipo katika mchakato wa kuliongezea thamani zao la korosho ambalo ndio zao kuu la biashara katika mkoa huo ambapo kwa kiasi kikubwa husafirishwa kwa njia ya bahari, ili pato la mwananchi mmoja mmoja liweze kuongezeka.
“Hivi sasa tupo katika mchakato wa kujenga viwanda viwili vya kubangua korosho ambavyo vitatutoa kwenye asilimia 20 ya kubangua mpaka asilimia 50 ifikapo mwaka 2016..lakini bado tunahangaika tunajua kwamba tukibangua kwa asilimia 100 tuwe tunaweza kufanikisha zaidi..” alisema.
Na kuongeza kwamba, wananchi wameanza kuona matunda ya kuwa na gesi asilia kutokana na kasi ya uwekezaji inavyokwenda ambapo mradi wa bomba la gesi umekamilika na kwamba unatarajiwa kuzinduliwa Oktoba 10 mwaka huu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete.
Alisema, sambamba na uzinduzi huo, Rais pia atazindua mradi wa ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Dangote, ambacho kinakadiriwa kutoa ajira za moja kwa moja zisizopungua 10,000 huku za muda mfupi zaidi ya 20,000.
No comments:
Post a Comment