Na Juma
Mohamed, Mtwara.
MGOMBEA
ubunge katika jimbo la Mtwara mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) Joel Nanauka, amezitaja sababu zilizomfanya kuhama Chama Cha Mapinduzi
(CCM) ni pamoja na kuwa na misimamo tofauti wakati wa vurugu za gesi kiasi cha
kutishiwa maisha pamoja na familia yake.
Akizungumza
na Mtandao huu wiki iliyopita, alisema sababu nyingine ni kupingana na matakwa yao kuhusu
mradi wa bomba la gesi ambapo katika ilani ya CCM katika Ibara ya 63 (k) na (h)
ilisema kuwa mradi wa Mnazi Bay wa Megawati 300 ni tofauti na wa Kinyerezi wa
Megawati 240, jambo ambalo alitaja kuwa lilikiuka mpango wa maendeleo wa miaka
mitano uliopitishwa Bungeni.
Alisema
mambo hayo yalipelekea viongozi wa CCM kuona kama anahujumu chama na kujaribu
kukalishwa katika vikao vya nidhamu lakini bado aliendelea kubaki katika
misimamo yake, ambapo baadae akaona bora aende katika chama ambacho kinaamini
katika haki na uwazi.
“Nilipata
ushauri wa watu wengi viongozi wa Chadema sio tu wa hapa Mtwara, wa maeneo
mbalimbali wengine rafiki zangu ambao nilikuwa nao chuoni wabunge kama akina
Silinde..nikasema ngoja nikapigane katika upande ule ambao wanaamini katika
haki, uwazi na masuala ya kijamii..” alisema Nanauka ambaye tayari ameshachukua
na kurudisha fomu.
Joel Nanauka, wapili kushoto, akiwa amepozi na wanachama wenzake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Mtwara, katika moja ya mikutano ya hadhara. |
Aliongeza
kuwa, “niko hapa nataka wananchi wa Mtwara wanitume kama mwakilishi wao kwenda
kusema katika Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania lakini kuleta
mabadilikio ambayo tumekuwa tukiyasubiria kwa muda mrefu na kushindwa
kuyapata.” Aliongeza.
Alisema swala
la mwanasiasa kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine sio la ajabu kwani wapo
viongozi wengi waliopo katika nafasi mbalimbali katika vyama vyao kwa sasa
ambao walishafanya hivyo huku akitolea mfano kwa katibu mkuu wa Chama cha
Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa kamati
kuu ya CCM toka mwaka 1977-1987, waziri kiongozi na mwenyekiti wa kamati ya
uchumi na uwekezaji wa CCM lakini leo hayupo huko nab ado CUF wanazidi
kumuamini.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mtwara mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joel Nanauka, akiwa katika jukwaa akihutubia wananchi wa Mtwara. |
Aidha,
alisema hana hofu na ushindani utakaojitokeza kutoka kwa watia nia wengine iwe
ndani ya Chadema au nje kwani ushindani wa kiuongozi ni ushindani wa hoja,
uwezo, uzoefu na matakwa ya wananchi hivyo anamini kwakuwa chema cha jiuza na
kibaya chajitembeza, na kwakuwa amejipima na anawafahamu wagombea wengine
anaimani wakiwekwa kwenye mizani atashinda.
“Mimi nasema
nimejipima, nimejiangalia, uwezo wangu naujua na nauamini na wapo wananchi wa
Mtwara ambao wanafahamu msimamo wangu na shughuli za kimaendeleo ambazo
nimezifanya..kwahiyo naamini tutakapokwenda kwenye mizani na hao wanaogombea
wengi nawajua ambao wametajwa kwa majina yao na nilipojipima na wao ndipo
nikapata nguvu kwasababu nawafahamu..” alisema.
Nanauka
ambaye amefanya kazi na kampuni mbalimbali za serikali na binafsi, kwa sasa ni
muajiriwa wa shirika la Umoja wa Mataifa (UNESCO) linaloshughulika na maswala
ya elimu, na yupo hapo kama msaidizi maalumu wa Mkurugenzi nchini Tanzania.
………………………………mwisho……………………………………………..
No comments:
Post a Comment