Na Mwaandishi wetu
MWENYEKITI wa NCCR-Mageuzi mkoani hapa Hassan Uledi, amejikuta katika wakati mgumu baada ya kutoa taarifa
zisizo sahihi zilizodai kuwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(UKAWA) vimempitisha kuwa mgombea
wa ubunge katika jimbo la Mtwara mjini.
Julai 23 mwaka huu Uledi aliita vyombo vya habari na kutoa taarifa juu ya kuhalalishwa
na UKAWA kuwa ndio mgombea ubunge wa jimbo hilo akidai kuwa amepata taarifa
kutoka makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam kupitia kwa katibu mkuu,
Mosena Nyambabe.
“Amesema
jimbo la Mtwara mjini kupitia UKAWA ni jimbo ambalo wameachiwa NCCR-Mageuzi..na
jimbo jingine ni jimbo jipya la Nanyamba. Hii ni taarifa rasmi kabisa kwahiyo
wananchi wafahamu kwamba katika majimbo ya mkoa wote wa Mtwara ambao kwa sasa
tuna majimbo nane, NCCR-Mageuzi imepata majimbo mawili chini ya UKAWA.” alisema
Uledi.
Hata hivyo,
taarifa hizo zilikanushwa na katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe, ambaye
alisema bado wapo katika mjadala juu ya maswala hayo ya kugawa majimbo na
taarifa rasmi zitatangazwa baada ya kukamilika kwa mchakato.
Alisema taarifa
zilizozungumzwa na mwenyekiti huyo ni za mwanzo ambapo anaweza kupewa jimbo kwa
wakati huu alafu baadae likabadilishwa, kwahiyo ni vigumu kutamka kwamba ni
jimbo la NCCR kwa wakati huu.
“Kama
tukikubaliana UKAWA baada ya kukamilisha tutangaza ‘officially’ (rasmi), hayo
ambayo yanazungumzwa ni ya mwanzo..unajua kuna matokeo ya awali na yale ambayo
ni rasmi, kwahiyo anaweza akawa sasaivi amepewa jimbo lakini baadae likabadilishwa.”
Alisema Nyambabe.
Kwa upande
wake, katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Mtwara,
Willy Mkapa, alisema jambo hilo limeongelewa kwa utashi tu wa NCCR lakini wao bado
hawajapatiwa waraka wowote wa kuthibitisha uhalali wa kuachiwa NCCR jimbo hilo.
Alisema inawezekana
mwenyekiti huyo aliongea hayo kwa kuwafurahisha wanachama wake au wagombea
wake, na kwamba bado viongozi wa UKAWA hawajakaa na kutoa mrejesho juu ya
ugawaji wa majimbo kwa wagombea wa vyama hivyo.
“Kama wao
wamepata hiyo taarifa basi itakuwa wamepata wao, lakini sisi kama chama ambacho
ni miongoni mwa vyama hivyo vinavyounda UKAWA hatujapata taarifa rasmi za
kuonyesha jimbo hili amepewa NCCR, CHADEMA, NLD au tumepewa sisi CUF.” Alisema.
No comments:
Post a Comment