Thursday, November 19, 2015

Tanesco Mtwara yawatahadharisha watumiaji wa umeme.

Na Juma Mohamed.

WATUMIAJI wa umeme mkoani hapa wameshauriwa kuzima vifaa vyao mara baada ya kukatika kwa umeme ili kuhepuka kusababisha madhara ya kuunguliwa na vifaa hivyo na hata kupelekea athari zaidi katika nyumba zao.
Akizungumza jana ofisini kwake, Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Mtwara, Mhandisi Azizi Salum, alisema wananchi wanatakiwa kuwa makini na vifaa vyao na kuachana na dhana iliyopo kwa baadhi yao wakiamini kuwa kuungua kwa vifaa kunatokana na umeme kurudi kwa kasi baada ya kukatika.
“Pale ambapo umeme unakatika, basi kama kulikua kuna kifaa ambacho kilikua kinafanya kazi ni vizuri kikazimwa, umeme utakaporudi basi vile vifaa vinaweza vikawashwa..matatizo yanatokea kama pale kifaa kitakua kimeachwa ‘on’ labda kama ulikua unapiga pasi ukajisahau ukaiacha ‘on’ umeme ukirudi pale kwavyovyote vile pasi ina ‘heat’ kwahiyo kama kuna kitu chochote karibu ambacho kinauwezo wa kuungua kinaweza kuleta madhara..” alisema.
Aidha, alisema hali ya upatikanaji wa umeme katika mkoa wa Mtwara kwa sasa imetengamaa baada ya kupatikana kwa vifaa vya mashine moja kati ya mbili ambazo zilipatwa na hitilafu na kusababisha mgao wa umeme katika baadhi ya maeneo kwa siku chache zilizopita.
Alisema, kutokana na kituo cha kuzalisha huduma hiyo kilichopo mkoani hapa kuhudumia pia katika mkoa wa Lindi, maeneo ambayo yaliathirika na mgao huo yalikuwa ni pamoja na Mtwara mjini, Tandahimba, Newala, Lindi mjini, Nachingwea na Masasi.
Meneja huyo alitoa wito kwa watumiaji wa umeme kuongeza juhudi katika ulipaji wa bili zao, kwani kwa kufanya hivyo inasaidia kuongeza kipato katika shirika hilo na kuwawezesha kuboresha huduma zao hasa za mitambo ambayo ikipatwa na hitirafu inapelekea ukosefu wa umeme kwa wananchi.



No comments: