Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally. |
Na Juma
Mohamed.
MKUU wa
wilaya ya Mtwara, Fatuma Ally, ameshauri serikali kufanya marekebisho ya adhabu
zilizoainishwa katika vifungu vya sheria za makosa ya uvuvi haramu ili kuweza
kudhibiti tatizo hilo ambalo linaonekana kuwa sugu katika baadhi ya maeneo yanayojihusisha
na shughuli hiyo.
Akizungumza juzi
mkoani hapa katika semina ya kujenga uelewa juu ya athari za uvuvi unaotumia milipuko kwa Maofisa
wanaoshiriki katika uchunguzi, mashitaka na hukumu za kesi zinazohusu uvuvi huo iliyoandaliwa na Baraza la Mazingira la
Taifa (NEMC), alisema hiyo imekua ni moja ya changamoto inayoikabili sekta hiyo
kutokana na sheria zilizopo kutotoa adhabu kali kwa waalifu.
“Adhabu zilizoanishwa kwenye sheria ya
makosa ya uvuvi haramu ni ndogo, yani hazina uzito sana kwahiyo zinamfanya
muhalifu kutoogopa kwasababu anajua ataadhibiwa kwa adhabu ndogo na kuendelea
na shughuli yake..kwahiyo labda tushauri tu kwamba zitolewe adhabu kali kwa
makosa ya uvuvi haramu..” alisema.
Alisema, changamoto nyingine katika
kukabiliana na uvuvi haramu ni ushiriki mdogo kwa jamii katika utoaji wa
taarifa kwa serikali kwa kuhofia usalama wao kutoka kwa baadhi ya wahalifu,
ambapo hiyo inatokana na kuishi pamoja na wahalifu ambao wengine ni ndugu.
Alisema, wapo wanaotoa taarifa kwa
simu kwenda kwa vyombo vya usalama juu ya kinachoendelea katika maeneo yao
lakini wakifika kwa lengo la kutaka kupata undani wa kilichotokea inakua ngumu
kupata ushirikiano.
“Ukiwa mbali watakutumia massage
(ujumbe) Mhe. Huku kuna hiki na hiki lakini ukifika pale kwenye eneo
ushirikiano hupati tena, watakudanganya tu lakini ukweli ni wenzao na wako nao
kwasababu tunavyokaa huko vijijini tunaowana basi utakuta ni shemeji yake..lakini
tuna changamoto nyingine ya umasikini sasa unakuta hii hali ya kipato kuwa duni
unakuta viongozi nao muda wao wa ziada wanashiriki katika uvuvi haramu..”
alisema.
Aidha, alivitaka vyombo husika
kujitahidi kwenda vijijini kuwaelimisha wananchi waweze kuachana na dhana
potofu kwamba mapambano dhidi ya uvuvi haramu ni jukumu la serikali na vyombo
vyake, na baadala yake waamini kwamba mtu wakwanza anayeweza kufahamu wahalifu
ni mwananchi wa eneo husika.
Semina hiyo imekuja ikiwa ni wiki moja
baada jeshi la polisi
mkoani hapa kuwakamata watu watatu kutokana na kukutwa na vifaa mbalimbali vya
milipuko vinavyotumika katika uvuvi haramu wa kutumia baruti katika bahari ya
Hindi, katika oparesheni maalumu ya kuwakamata wanaojihusisha na mtandao huo.
No comments:
Post a Comment