Mashabiki waliojitokeza kushuhudia mchezo kati ya Ndanda Sc na Azam Fc |
Jukwaa kuu |
Waandishi wa habari wakifanya yao |
Na Juma Mohamed
MWENYEKITI wa
Chama cha Soka Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA), Athumani Kambi, amesema, wameshindwa
kufikia lengo katika mchezo wa kirafiki wa kuadhimisha siku ya Ndanda (Ndanda
Day) katia ya wenyeji Ndanda Sc na Azam Fc, uliopigwa jana katika uwanja wa
Nangwanda Sijaona mkoani hapa na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Kambi
alisema, lengo la mchez huo ulioingiza kiasi cha sh. Milioni 3.1 kutokana na
mashabiki walioingia uwanjani ilikuwa ni kuwatambulisha wachezaji wapya kwa na
kuchangisha fedha za kuisaidia timu hiyo, lakini halikuweza kufanikiwa kutokana
na uchache wa mashabiki waliojitokeza.
Alisema kutokana
na hali hiyo, wanaangalia uwezekano wa kurudia kufanya tamasha hilo kwa
kuialika timu nyingine kabla ya kuanza kwa ligi kuu ili kuweza kufikia lengo
ambapo alisema inahitajika kufanya hamasa zaidi kwa mashabiki ili wajitokeze
kuona wachezaji wapya waliosajiliwa na timu yao.
“Hatujui
kwanini imekuwa hivi lakini nadhani ni hamasa na sisi wenyewe tulichelewa
kuitangaza mechi kwahiyo hatuwezi kulaumu mashabiki..kwahiyo tutajiandaa vizuri
na kuitangaza mechi na tutarudia tamasha la Ndanda..” alisema.
Na kuongeza “tulichofarijika
leo ni kuiona timu na kwa mtazamo wangu nimeona timu yetu ni nzuri kuliko ile
ya mwaka jana, kwahiyo ninaimani kwamba mwaka huu tunaweza kufanya vizuri
zaidi.” Aliongeza.
Kwa upande
wao, baadhi ya mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo kushuhudia kipute hicho
walikuwa na maoni tofauti juu ya kiwango kilichoonyeshwa na timu yao na uchache
wa mashabiki walioingia uwanjani.
Mzarubu
Shaibu, alisema bado anaimani na timu hiyo kuwa itafanya vizuri katika ligi kuu
msimu huu kutokana na namna alivyoona ikicheza ukiachiliambali ugeni wa baadhi
ya wachezaji waliosajiliwa, ambapo alisema wakikaa pamoja kwa muda mrefu
watazoeana na kutengeneza muunganiko nzuri na kuipa matokeo mazuri Ndanda.
Naye, Salum
Mabomba, alisema sababu zilizopelekea mashabiki kutojitokeza kwa wingi uwanjani
hapo ni uwepo wa mkutano wa uznduzi wa kampeni kwa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) chini ya UKAWA na michuano ya ligi za Ulaya.
“Hamasa ni
nzuri na leo tukumbuke kulikuwa na mchanganyiko wa mambo mengi, wengi wameenda
kwenye siasa wengine wameenda kwenye mipira ya Uingereza lakini kidogo watu
hajatuangusha, wamekuja kuiangalia na walikuwa na hamu sana na timu yao
walikuwa wakilalamika kila siku kuwa timu inafanya mazoezi Dar es Salaam lakini sasa imerudi..” alisema
Na kuongeza
kuwa “ikitokea mechi nyingine basi tujae zaidi ya leo walivyokuja ili tuweze
kuongeza hamasa zaidi na wachezaji wageni wajue kwamba watu wa Mtwara ni watu
wa mpira siku zote.”
Katika mechi
hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi David Paul kutoka Mtwara, Azam ndio walikuwa
wakwanza kupata bao kupitia kwa kiungo wao Kelvin Friday katika dakika ya 12
baada ya kuwazidi ujanja walinzi wa Ndanda, huku lile la kusawazisha kwa Ndanda
likifungwa kwa kichwa na mshambuliaji wao Omari Mponda dakika ya 82 baada ya
kuunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Kigi Makasy.
Azam Fc
walijikuta wakimaliza pungufu mchezo huo baada ya mlinzi wao wa kati David
Mwantika kulimwa kadi nyekundu kutokana na kumchezea madhambi Omari Mponda
wakati akielekea langoni akiwa amewatoka walinzi wote, ambapo mwamuzi aliamuru
ipigwe penaiti ambayo hata hivyo mpigaji Kigi Makasy alipaisha.
Akizungumza
baada ya mchezo huo, kocha wa timu ya Ndanda, Hamimu Mawazo, alisema bado
hajaridhishwa na kiwango cha wachezaji wake hivyo kazi ya ziada inahitajika ili
kuweza kuwaweka sawa kabla ya kuanza mikikimikiki ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Kwa upande
wake, kocha wa Azam Fc ambao walishusha kikosi B na baadhi ya wachezaji wa
kikosi cha kwanza kutokana na makubaliano baina yao na Ndanda, Benis Kitambi,
alisema mchezo ulikuwa mzuri na kwamba wao waliuchukulia kama mchezo wa
kuwapima wachezaji wao ili waeze kupata uzoefu.
No comments:
Post a Comment