Na Juma Mohamed.
SHINIKIZO kutoka kwa wananchi limepelekea mgombea mwenza wa nafasi ya Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Juma Duni Haji, kulazimika kumtangaza Maftaha Nachuma wa Chama cha Wananchi (CUF), kuwa mgombea ubunge katika jimbo la Mtwara mjini kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Maamuzi hayo
yalitokana na wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanywa na UKAWA jana katika viwanja vya
Mashujaa mkoani hapa, kuwa na shauku ya kutaka kumjua mgombea wao katika jimbo
hilo ambalo kwa kipindi kirefu lilikuwa na mvutano kati ya vyama vitatu vya
NCCR-Mageuzi, CUF na CHADEMA.
Wananchi walisimama
kwa jazba huku wengi wao wakiwa na mabango na bendera za vyama vya NCCR na CUF baada
ya kuona mkutano unaelekea kumalizika pasipokuwaona wagombea wao wakisimama
jukwaani na kupata nafasi ya kumjua nani anasimamishwa na UKAWA katika jimbo
hilo.
Baadhi ya
viongozi wa vyama hivyo walijaribu kuwaomba wananchi kuwa na subira mpaka pale
vikao vya UKAWA ngazi za juu vitakapofikia muwafaka wa nani anafaa kupewa jimbo
hilo, lakini ilishindikana kutokana na kuona hali inazidi kuwa mbaya kwani
wananchi walitaka kuvamia meza kuu ambako alikaa mgombea mwenza, Juma Duni
Haji.
Baada ya kuona jazba imezidi kwa wananchi ndipo alipoamua kusimama mgombea huyo na kuwaomba wananchi kuwa watulivu na kumsikiliza “Kama munaniheshimu naomba nisikilizeni..hapa mgombea wa jimbo hili ni wa CUF..” alisema kwa ufupi na kuondoka katika viwanja hivyo.
Wakizungumza
baada ya maamuzi hayo, baadhi ya wananchi walikuwa na maoni tofauti juu ya
maamuzi yaliyotolewa ambapo wengine walionekana kuyaunga mkono huku wengine
wakiyapinga.
Sada
Abdallah, alisema mgombea aliyetangazwa anastaili kutokana na kuwa na sifa zote
za kuwa mbunge ambapo alisema ni msomi na hata kugombea Urais anakidhi.
Naye, katibu
wa kamati ya sheria na haki za binadamu wa CHADEMA kanda ya kusini, Hassani
Mbagile, alisema wameyapokea maamuzi hayo kama yalivyoamuliwa na mgombea huyo
lakini hayataishia hapo kwani watawasiliana na viongozi wa UKAWA ili kuhoji
kama kuna uhalali wa mgombea kutoa maamuzi kutokana na shinikizo kutoka kwa
wananchi.
“Tutawasiliana
na viongozi wetu watueleze je, maamuzi ya UKAWA yanaamuliwa kwenye majukwaa ya
kisiasa au yanaamuliwa katika viako vya UKAWA katika ngazi za kitaifa..je,
kiongozi anaweza kutoa maamuzi magumu na mazito yanayobeba mustakabali wa watu
wengi kutokana na presha ya watu kwenye mkutano wa hadhara?..kwahiyo mimi
niseme tu tumeyapokea na tunamuheshimu mzee Duni ni kiongozi wetu na ni mmoja
kati ya viongozi wa UKAWA na ni mgombea mwenza, kwahiyo tunamuheshimu kwa
nafasi yake.” Alisema.
Kwa upande
wake, mgombea wa NCCR Uledi Hassan, alipotafutwa na NEWS ROOM kuzungumzia
maamuzi hayo alisema hawezi kuzungumza chochote kutokana na kuwa katika kikao.
Naye mgombea
wa CHADEMA, Joel Nanauka, alisema hakutarajia maamuzi yaliyotolewa kutokana na
vikao vya UKAWA kuwa bado vinaendelea lakini anayaheshimu na kwamba yuko tayari
kuyaunga mkono endapo yatabaki kuwa kama yalivyotangazwa.
“Na niwaombe
tu wafuasi wangu kuwa watulivu na kuwaunga mkono waliotangazwa kuwa wagombea
katika ngazi zote kuanzia udiwani, ubunge na hata Urais ili tufikie malengo
yetu..” alisema.
Mgombea mwenza wa nafasi ya Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Juma Duni Haji, akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana mjini Mtwara katika viwanja vya Mashujaa |
Aidha, akizungumza
kabla ya maamuzi hayo, Juma Duni Haji, alisema endapo UKAWA watafanikiwa
kuingia madarakani, wananchi wa Mtwara na mikoa mingine ambako kunalimwa zao la
Korosho, watafurahia mauzo ya zao hilo na mfumo ulipo sasa wa kukopwa wakulima
utakuwa umefika mwisho.
Alisema serikali
iliyopo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndio inachangia kwa kiasi kikubwa
umasikini wa wananchi kutokana na kuwakandamiza katika kipato chao kidogo
wanachokipata, hasa pale wanapokatwa katika mazao yao ya biashara.
“Ni wizi wa
macho macho, bei ya kuistahiki ya korosho baadala ya kupewa watu wa Mtwara
inakatwa..unapewa 600 alafu unaambiwa 1000 baadae, kwahiyo kwa makusudi
wanawafanya muwe masikini kwa hata kile kilicho chako..” alisema.
No comments:
Post a Comment