NA Juma Mohamed
CHAMA cha
NCCR-Mageuzi mkoani hapa kimepinga maamuzi ya kupewa jimbo la Mtwara mjini
Chama cha Wananchi (CUF) kusimamisha mgombea ubunge kupitia Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA), yaliyotolewa juzi na mgombea mwenza wa Urais kupitia Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Juma Duni Haji.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana, mwenyekiti wa NCCR mkoa wa Mtwara na mgombea wa
ubunge katika jimbo hilo, Uledi Hassan, alisema kilichotamkwa na mgombea huyo
siyo makubaliano ya UKAWA kwani makubaliano rasmi yanatolewa katika vikao
halali vinavyowahusisha viongozi wakuu wa umoja huo ambapo mpaka juzi ilikuwa
bado hayajatolewa maamuzi yoyote juu ya jimbo hilo.
“Mpaka jana
(juzi) tulipata taarifa kwamba jimbo la Mtwara mjini hakuna chama hata kimoja
kilichopewa..kwahiyo tunakwenda kwenye mkutano tukijua hilo, lakini kilichokuja
baadae kila mtu anashangaa kuona anatangazwa mtu ambae sio makubaliano ya UKAWA..”
alisema.
Aidha,
alisema iwapo taratibu za kutangazwa mgombea zitafuatwa, basi yuko tayari
kumuunga mkono mgombea yeyote atakaepitishwa na umoja huo hata kama siyo yeye,
lakini sio kwa njia ya kutangaza katika majukwaa ya mikutano ya kisiasa.
Alisema,
jana ilikuwa aanze kapeni eneo la Bima mjini hapa, lakini ilishindikana
kutokana na kusubiri maamuzi kutoka kwa viongozi wa UKAWA juu ya jimbo hilo, na
kwamba aliwataka wananchi waendelee kuwa na uvumilivu mpaka mgombea rasmi
atakapotangazwa.
“Kwahiyo
wananchi wa Mtwara mi nafikiri bado waendelee kusubiri tu, kwasababu hivi ni
vyama, na vyama ni taasisi na zina sheria na kanuni zake, sasa watakavyokubaliana
kule, wakisema apewe mtu wa CUF sisi hatuna tatizo, wakisema apewe CHADEMA
hatuna shaka..sasa kama hatuheshimiani katika maamuzi ya kitaifa nadhani UKAWA
huko mbele utakwenda kuyumba sana..” alisema.
Maamuzi ya
kupewa jimbo CUF yalitokana na wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara
wa kampeni uliofanywa na UKAWA juzi katika
viwanja vya Mashujaa mkoani hapa, kuwa na shauku ya kutaka kumjua mgombea wao
katika jimbo hilo ambalo kwa kipindi kirefu lilikuwa na mvutano kati ya vyama
vitatu vya NCCR-Mageuzi, CUF na CHADEMA.
Wananchi
walisimama kwa jazba huku wengi wao wakiwa na mabango na bendera za vyama vya
NCCR na CUF baada ya kuona mkutano unaelekea kumalizika pasipokuwaona wagombea
wao wakisimama jukwaani na kupata nafasi ya kumjua nani anasimamishwa na UKAWA
katika jimbo hilo, ndipo Juma Duni Haji akaamua kutangaza kuwa CUF ndio
wasimamishe mgombea.
No comments:
Post a Comment