Juma Nyosso |
BEKI wa Simba SC, Juma Said
Nyosso amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kuichezea klabu hiyo, baada ya
mkataba wake awali kumalizika, hivyo kumaliza tetesi kwamba anaweza kuhamia kwa
watani wa jadi, Yanga SC.
Makamu Mwenyekiti wa Simba SC,
Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ameiambia BIN ZUBEIRY mchana wa leo
kwamba, Nyosso alisaini mkataba huo Julai 1, mwaka huu.
Kaburu alisema kwamba Simba
ina imani na beki huyo wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na ndio maana
imemuongezea mkataba.
Aidha, Kaburu aligusia suala
la beki wao, Kelvin Yondan aliyehamia kwa watani wa jadi, Yanga akisema kwamba
bado ni mchezaji wao halali na wamekwishapeleka malalamiko yao Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), wanasubiri majibu.
Kaburu pia amesema
mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Felix Sunzu tayari amejiunga na wenzake
kambini visiwani Zanzibar, ambako timu hiyo inashiriki Kombe la
Urafiki.
Kaburu amesema Simba
itaendelea kuwa Zanzibar hata baada ya michuano hiyo, wakijiandaa na Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, ambalo linatarajiwa kuanza
kutimua vumbi Julai 14, Simba wakifungua dimba na URA ya Ugandea Julai
16.
MAREFA WA KOMBE LA YANGA WATAJWA
Marefa
wa Kagame mwaka jana, wakisindikizwa na Polisi kwa usalama wao, baada ya maamuzi yao kutowafurahisha mashabiki |
BARAZA la Vyama vya Mpira wa
Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limeteua waamuzi 15 kuchezesha michuano
ya Kombe la Kagame itakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 14-28 mwaka
huu.
Waamuzi hao wanatakiwa
kuwasili Dar es Salaam, Julai 11 mwaka huu kwa ajili ya vipimo vya afya na
mtihani wa utimamu wa viungo utakaofanyika Julai 12 na 13 mwaka huu Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam chini ya wakufunzi wa CECAFA.
Kwa
upande wa waamuzi wa kati (centre referees) walioteuliwa ni Anthony Ogwayo
(Kenya), Dennis Batte (Uganda), Israel Mujuni (Tanzania Bara), Issa Kagabo
(Rwanda), Thierry Nkurunziza (Burundi), Farah Aden Ali (Djibouti) na Waziri
Sheha (Zanzibar).
Waamuzi wasaidizi (assistant
referees) ni Elias Kuloba (Kenya), Peter Sabatia (Kenya), Musa Balikoowa
(Uganda), Hamis Changwalu (Tanzania Bara), Jesse Erasmo (Tanzania Bara), Simba
Honore (Rwanda), Abdulahi Mahamoud (Djibouti) na Josephat Bulali
(Zanzibar).
Yanga ndio bingwa wa michuano
hiyo, baada ya kuifunga Simba katika fainali 1-0, mwaka jana,
COPA COCA COLA YAFIKIA PATAMU
WAKATI hatua ya 16 bora ya
michuano ya Copa Coca-Cola 2012 inaanza Jumamosi (Julai 7 mwaka huu), timu 14
zitakazocheza hatua hiyo zimeshajulikana baada ya mechi zilizochezwa leo (Julai
5 mwaka huu) katika viwanja vinne tofauti.
Tanga iliyoigaragaza Kaskazini
Pemba mabao 4-0 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es
Salaam imechukua moja kati ya nafasi nne kutoka kundi B. Mabao ya Tanga
yalifungwa na Mbwana Musa dakika ya 30, 55 (penalti) na 58 wakati lingine
lilifungwa dakika ya 53 na Issa Mwanga.
Kwa
ushindi huo, Tanga iliyofikisha pointi tisa inaungana na Mjini Magharibi yenye
pointi 13, Morogoro pointi 12 na Mwanza pointi 11 kutoka kundi hilo kucheza
hatua ya 16 bora.
Mara iliyoichapa Mtwara mabao
4-1 kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam na kufikisha
pointi tisa nayo imepata tiketi ya 16 bora kutoka kundi C ikiungana na Dodoma
yenye pointi 12, Kinondoni pointi 11 na Temeke pointi
tisa.
Mabao ya Mara ambayo hadi
kipindi cha kwanza kinamalizika ilikuwa mbele kwa 3-0 yalifungwa na George
William dakika ya pili, Edson Mwara dakika ya 17 na 45, na Hassan Ally dakika ya
88. Mtwara walipangusa machozi dakika ya 36 kwa bao la Ramadhan
Njunja.
Ndoto za Ilala kucheza 16 bora
zimeyeyuka baada ya kulala mabao 2-1 mbele ya vinara wa kundi A Ruvuma kwenye
Uwanja wa Tamco mkoani Pwani. Mbali ya Ruvuma iliyofikisha pointi 16, timu
nyingine zilizopata tiketi ya 16 bora kutoka kundi hilo ni mabingwa watetezi
Kigoma wenye pointi 12, Rukwa pointi kumi na Arusha pointi
nane.
Mchuano wa kupata timu mbili
za mwisho kucheza 16 bora uko katika kundi D ambalo linasubiri matokeo ya mechi
ya leo jioni kati ya Kusini Unguja na Tabora itakayochezwa Uwanja wa Nyumbu
mkoani Pwani.
Kagera ambayo leo imeifunga
Shinyanga mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Nyumbu ni moja kati ya mbili ambazo
zimeingia 16 bora kutoka kundi hilo. Nyingine ni Kilimanjaro iliyoongoza kwa
kufikisha pointi 18 ikifuatiwa na Kagera yenye pointi
tisa.
Nafasi mbili zilizobaki
zinawaniwa na Pwani yenye pointi saba, Singida (7), Tabora (6) na Kusini Unguja
yenye pointi nne.
No comments:
Post a Comment