BIN ZUBEIRY na Saintfiet |
Na Mahmoud
Zubeiry
“NIMEKUWA nikisikia habari
nyingi kuhusu Yanga, ni timu kubwa. Na ninafurahi kuja hapa, naamini nitafanya
vizuri,”.
Ndivyo alivyoanza kuzungumza,
Thom Saintfiet katika mahojiano na BIN ZUBEIRY mchana huu, baada
ya kuwasili Dar es Salaam, tayari kusaini mkataba na kuanza kufundisha klabu
hiyo.
Thom amepata mapokezi makubwa
baada ya kuwasili na moja kwa moja alipelekwa makao makuu ya klabu, makutano ya
mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam. Akiwa hapo, alionyeshwa ofisi na
mataji mbalimbali ya klabu hiyo pamoja na Uwanja wa mazoezi na gym.
“Sifahamu sana kuhusu Yanga au
Tanzania kwa ujumla, naamini mengi nitajifunza hapa, ila mimi kama mwalimu baada
ya kukubali kuja Tanzania kufundisha, nilianza kujifunza kidogo kuhusu nchi hii
na hususan Yanga,”alisema Thom alipoulizwa kama anaifahamu Yanga au soka ya
Tanzania.
Kwa nini ameamua kuja
kufanya kazi Tanzania, hususan Yanga? “Imetokea nimekubali, lakini
nilikuwa nina ofa nyingine, ila nimetaka kubadilisha uzoefu wangu kwa sasa, kuwa
kocha wa klabu badala timu za taifa,”alisema.
Thom Saintfiet akiwa na Kombe la Kagame |
Jukumu lake la kwanza
Yanga ni nini? “Kwa sasa unaliona Kombe lile (la Afrika Mashariki na
Kati), nataka liendelee kuishi kwenye ofisi hii (ya Katibu wa Yanga), nina muda
mfupi sana, lakini najua Yanga walitwaa Kombe lile mwaka jana na wanatakiwa
kulitetea karibuni, nina uhakika hilo ndilo jukumu langu la
kwanza,”alisema.
Alipoulizwa kuhusu muda,
Saintfiet alisema kwamba Yanga imekuwa chini ya mwalimu msaidizi na ni mwalimu
mzuri, hivyo anaamini alikuwa anafanya kazi yake vizuri. “Nitaungana naye,
nianzie pale alipoishia tufanye pamoja kwa kushirikiana kuhakikisha, kwanza
Kombe linabaki hapa.
Na
viongozi wamenihakikishia timu ina wachezaji wazuri, nimeomba DVD za timu za
karibuni ili nione wanachezaje katika mechi, na nikianza kazi naamini kila kitu
kitakuwa sawa, Yanga ina wachezaji profesheno na wanajua wajibu wao, hivyo najua
watakuwa vizuri na tutaelewana,”alisema.
Amesikia kuhusu
Simba?
“Nimesikia kuhusu Simba,
viongozi wangu wameniambia, nchi yenye timu za aina hii (wapinzani wa jadi),
lazima soka yake inakuwa na msisimko mkubwa. Na upinzani huu ni changamoto
kwangu. Lazima Yanga iongoze kila wakati. Najua kuna timu nyingine inasifika,
Azam FC. Lakini mimi ni mpinzani wa kila timu ninayokutana nayo, na ninataka
ushindi kila siku,”anasema.
Ametokea wapi huyu
jamaa?
Tom
Saintfiet anasema alizaliwa Machi 29, mwaka 1973 mjini Mol, Ubelgiji na kabla ya
kuwa kocha alicheza soka katika nafasi ya kiungo kuanzia mwaka 1983 hadi 1997
alipostaafu na kuwa kocha akiwa ana umri wa miaka 24, akiweka rekodi ya kocha
kijana zaidi kuwahi kutokea katika soka ya Ubelgiji.
Saintfiet anasema amefundisha
nchi kadhaa kuanzia kwao Ubelgiji, Qatar, Ujerumani, Visiwa vya Faroe, Finland
na Uholanzi.
Anasema pia ana uzoefu wa
kutosha wa kufundisha soka Afrika akiwa amefundisha Namibia na Zimbabwe kama
kocha Mkuu wa timu za taifa za nchi hizo.
Anasema kabla hajakwenda
Namibia, Saintfiet alikuwa kocha wa klabu ya Ligi Kuu Finland, iitwayo RoPS
Rovaniemi na mwaka 2002, alikwenda kuifundisha B71 Visiwa vya Faroe ambayo
aliiwezesha kushika nafasi ya pili katika Ligi Daraja la kwanza. Anasema kutoka
hapo, akaenda kuwa kocha wa Al-Ittihad Sports Club ya Qatar (sasa inaitwa
Al-Gharafa SC) ambako alidumu hadi mwaka 2004 alipochukuliwa kuwa kocha wa timu
ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Qatar.
Anasema akiwa na U17 ya Qatar,
aliiwezesha kushika nafasi ya tatu katika Kombe la Mataifa ya Asia na hivyo
kufuzu kucheza Fainali za vijana za Kombe la Dunia la FIFA. Kuelekea Fainali za
Kombe la Dunia mwaka 2010, Saintfiet anasema alikuwa kwenye mpango wa kupewa
timu ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, wakati huo akiwa Mkurugenzi wa Ufundi wa
Shirikisho la Soka la nchi hiyo.
Anasema katika timu za taifa,
mafanikio zaidi alipata akiwa na Namibia kwanza akiifikisha robo fainali ya
michuano ya COSAFA kwa kuzifunga Comoro na Malawi na kutoka sare na Lesotho
katika fainali zilizofanyika Afrika Kusini Julai mwaka 2008.
Hata hivyo, anasema Namibia
ilitolewa na Afrika Kusini katika robo fainali, ambao mwishowe waliibuka
mabingwa wakiwa wenyeji.
Anasema mafanikio yake akiwa
na Namibia ni pamoja na kuifunga Zimbabwe 4-2 katika mechi ya kuwania tiketi ya
kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC) 4-0 katika mchezo wa kirafiki.
Anasema alipata heshima kubwa
akiwa Namibia, kiasi cha kufikia hadi kuitwa ‘Nabii’ na Mtakatifu.
Anasema sababu ni kwamba,
aliifanya Namibia ikawa inacheza soka nzuri na kupata pia mafanikio, ndiyo maana
akawa anatukuzwa mno nchini humo.
Thom Saintfiet akizungumza na Waandishi wa Habari, makao makuu ya Yanga, Jangwani. Kulia ni Katibu wa Yanga, Celestine Mwesigwa na kushoto mmoja wa wafadhili wa klabu hiyo, Seif Ahmad 'Magari'. |
Anasema moja ya matukio ya
kukumbuka ni siku tatu baada ya kutoka sare 1-1 ugenini na Lebanon Aprili mwaka
2009, Namibia ilipata matokeo ya kuvutia ya sare ya bila kufungana ugenini na
Angola.
Lakini matokeo mazuri zaidi na
yaliyomfurahisha ilikuwa ni mjini Durban, wakati Namibia ilipotoa sare ya 1-1 na
Afrika Kusini, baada ya kuongoza sehemu kubwa ya mchezo huo. Anasema kwa miezi
kadhaa, Namibia ilikuwa imeshinda mechi moja tu kati ya 12 kabla ya kuwasili
kwake nchini humo.
“Baada ya mafanikio makubwa,
vyombo vya habari Namibia vilinipa jina la utani The Saint (Mtakatifu) na gazeti
moja lilidiriki kuniita The Messiah (Nabii).
Baada ya hapo alisaini mkataba
wa miaka minne na Shirikisho la Soka Zimbabwe (ZIFA) Oktoba 1, mwaka 2010,
lakini anasema kutokana na matatizo ya kutopewa kibali cha kufanya kazi nchini
humo, alifanya kazi katika mazingira magumu, hadi Desemba mwaka 2010 alipoamua
kubwaga manyanga na kujiunga na Shabab Al Ordon.
Anasema alisaini mkataba wa
miezi minne na mabingwa hao wa Ligi ya Mabingwa Asia mwaka 2007, Shabab Al Ordon
na alifanya kazi nzuri ya kutukuka huko, akijenga ukuta imara ambao katika mechi
tano uliruhusu bao moja tu.
“Baada ya mechi sita,
tukishinda tatu na kutoka sare tatu, nilitosheka na nikaiacha timu ikiwa katika
nafasi ya pili na haijafungwa,”alisema.
Anasema baada ya kupokea ofa
kutoka timu tatu za taifa za Afrika, aliikubali ya Ethiopia na mwishoni mwa Mei
mwaka 2011 akaanza kazi.
Baada tu ya kusaini mkataba,
Saintfiet anasema ndani ya siku 10 alikuwa ana mtihani mzito wa kucheza na
Nigeria kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2012.
“Nigeria ilikuwa imetoka
kuifunga Argentina 4-1 siku nne kabla ya mechi yetu na wao na pia iliifunga
Ethiopia 4-0 katika mechi ya kwanza ya AFCON nyumbani, lakini hadi mapumziko
niliiongoza timu kumaliza kwa kufungana 1-1. Tulifanikiwa kupata bao la kuongoza
kipindi cha pili, lakini kwa bahati mbaya beki Joseph Yobo akasawazisha ikawa
2-2 mwisho wa mchezo,”anasema.
Kwa
mara nyingine, Saintfiet anasema akajizolea sifa kemkem kwa staili yake ya
ufundishaji baada ya kuifanya Ethiopia kuwa timu ya ushindani yenye kucheza soka
maridadi hata dhidi ya vigogo kama Nigeria.
“Baada ya mechi, kocha wa
Nigeria, Samson Siasia alisema amestaajabishwa mno na soka ya kitaalamu na
nidhamu ya hali ya juu ya Ethiopia na Nigeria hawakupata majibu. Licha ya
kukubalika sana, lakini Oktoba 28, mwaka jana nilijiuzulu, baada ya kupata ofa
ya Nigeria” anasema.
Machi 28, mwaka huu, Mbelgiji
huyo anasema alipewa mkataba wa miaka minne wa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa
Nigeria, lakini Juni, mwaka huu akaamua kuvunja mkataba huo baada ya kuvutiwa na
ofa ya Yanga.
NONDOZ ZA ‘MTAKATIFU’
THOM
Saintfiet anasema ana leseni
Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) ya kufundisha soka ya kulipwa popote barani
humo, ambayo aliipata mwaka 2000.
Anasema kati ya mwaka 2006 na
2007 alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa FC Emmen ya Daraja la Kwanza Uholanzi na
pia amewahi kufanya kazi kama Mshauri wa Ufundi wa Shirikisho la Soka la
Kazakhstan.
Anasema amewahi kuwa
Mchambuzi wa soka katika Televisheni katika nchi za Ubelgiji, Afrika Kusini na
Namibia na alifanya kazi kama mkalimani DFB. Anasema amesomea Saikolojia ya
Michezo na Uchumi.
Anasema anazungumza lugha
kibao na kwa ufasaha zaidi ni Kiholanzi, Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani,
Kifaroe na ‘ana jua jua’ Kiarabu, Kiafrikana na Kispanyola.
Naam huyo ndiye Thom
Saintfiet, ambaye anatarajiwa kusaini mkataba wa kuinoa Yanga, akiwa tayari
amekuja nchini kikamilifu. Je, Yanga imepata mwalimu? Je, watadumu naye? Je,
hayatajirudia yale yale? Bila shaka hayo ni mambo ya kusubiri na kuona, ila kwa
mujibu wa wasifu wake, huyu ni mwalimu wa uhakika
No comments:
Post a Comment