Na Juma Mohamed.
ABIRIA
wanaosafiri kwa mabasi ya kutoka Mtwara kwenda jijini Dar es Salaam
wamelazimika kusubiri kwa muda wa saa tatu kutokana na madereva wa mabasi hayo
kugoma kuondoka kushinikiza kuachiwa huru wenzao watatu wanaoshikiliwa na jeshi
la polisi kitengo cha usalama barabarani kutokana na kwenda mwendo kasi.
Wakizungumza
katika kituo kikuu cha mabasi mkoani hapa, baadhi ya abiria walisema hali hiyo
imekwamisha mipango yao kwasababu wapo wanaosafiri kwa matatizo na wapo
wanaosafiri kwa ajili ya kuwahi mambo mengine ya msingi kwa ajili ya shughuli
za ujenzi wa taifa.
Muhidin
Chinengo, ambaye ni msafiri anyeelekea mkoani Shinyanga, alisema juzi alikata
tiketi katika basi la Machinga kwa ajili ya kusafiri jana mpaka Dar es Salaam
ambako angeunganisha kwa usafiri wa Treni na kufika Shinyanga katika chuo cha
Maopareta lakini amekutana na kikwazo hicho ambacho hakujua hatima yake.
“Nikiwauliza
walionikatia tiketi wanasema wana mgomo kutokana na madereva wao ambao
wamekatwa kwasababu ya mwendo kasi..kila tukiwahoji ili tujue uwezekano wa
kusafiri wao wenyewe hawatupi taarifa au hawatoi ushirikiano wowote, kwahiyo
mimi nilikuwa nawaomba kama Machinga Transporter makao makuu ni Mtwara bosi
mwenyewe yuko hapa na meneja wake yuko hapa na wanajua hadha hizi tunazopata
sisi wananchi basi atusaidie..” alisema.
Naye Iddi
Selemani, msafiri wa basi la Maning Nice, alisema anashangazwa na kitendo cha
askari kuonekana kituoni hapo lakini bado hakuna muafaka wowote wa jambo hilo
huku wao wakiendelea kusota na kutojua ni muda gani wataanza kusafiri.
Kwa upande
wake, Dereva wa basi la Buti la Zungu, Abdul Mcharu, alisema hoja yao ya msingi
ni kutaka kujua hatima ya madereva hao wa mabasi matatu ambao aliwataja majina
kuwa ni Imma (Ibra Line), Athumani (No Raiz) na Rashid Machemba (Machinga)
ambao walikamatwa kwa kosa la kwenda mwendo kasi.
“Kitu
ambacho kinatutoa katika mawazo yetu ya kawaida sisi madereva na kutupeleka
katika mawazo makubwa sana ni kwamba swala la Tochi kwanzia jana (Juzi) saa 9
mpaka sasaivi saa 2 kweli mtu yuko mahabusu alafu katika hali ya sintofahamu
tulikwenda sisi pale ili kutaka suluhu inamaana maderva wa Mtwara ndio
sisi..inamaana RTO wa Mtwara amepanga moja mbili tatu kwenye hili, litakalo
mkuta ambalo tutagundua kwamba tushamweleza ni lakwake..” alisema Dereva huyo.
Mkuu wa
Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Mtwara (RTO) Meloe Buzema, alisema madereva
waliokamatwa suala lao linashughulikiwa na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani
ili wasomewe mashitaka yao.
Alisema,
jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani kwa sasa lipo katika oparesheni ya
kudhibiti makosa ya mwendo kasi kwasababu ajali nyingi zinazotokea ni kutokana
na mwendo kasi huku wahusika wanatozwa faini alafu bado wanaendelea kufanya
makosa kwaiyo namna ya kuweza kukabiliana nao ni kuwafikisha mahakani.
“Ajali zote
zinazotekea ni mwendo kasi, sasa hatuwezi kuacha tukawa tunateketeza maisha ya
watu kwa kuwafumbia macho watu ambao tunaweza tukachua hatua stahiki..kwasababu
kama faini tunaona wanapigwa faini na askari 30,000 barabarani lakini bado
wanaendelea kufanya yaleyale ndio maana tumeona tufikie hatua ya kuwapeleka
mahakamani..” alisema.
Hata hivyo
mtandao huu ulishuhudia mabasi yakianza safari kituoni majira ya saa tatu
asubuhi isipokuwa ni basi moja la Ibra Line ambalo halikupata dereva mwingine
wakuliendesha.
No comments:
Post a Comment