Wednesday, January 6, 2016

Kaya 150 Tandahimba zakosa makazi kutokana na upepo na mvua iliyonyesha kwa dk 3.

Baadhi ya nyumba za wakazi wa vijiji vya Chaume na Sokoine wilayani Tandahimba zilizobomolewa na mvua iliyoambatana na upepo mkali kiasi cha kusababisha kaya 150 kukosa makazi na upotevu wa chakula. (PICHA KWA HISANI YA FATUMA MAUMBA)

Miongoni mwa vyakula vilivyokumbwa na kadhia kutokana na mvua iliyoambatana na upepo mkali.


Paa la nyumba lililohezuliwa kutokana katika moja ya nyumba


 Na Juma Mohamed, Mtwara.

KAYA zipatazo 150 wilayani Tandahimba mkoani hapa hazina makazi kufuatia upepo mkali ulioambatana na mvua iliyonyesha kwa muda mfupi unaokadiriwa kutozidi dakika 3 katika Kijiji cha Chaume na Sokoine, kuezua nyumba na nyingine kubomolewa vibaya huku baadhi ya wakazi wakikosa chakula.
Kadhia hiyo iliyowakumba wakazi hao ilitokea January mosi mwaka huu majira ya saa saba mchana, na kuzusha taharuki kubwa ambayo  wakazi wa vijiji hivyo waliona sehemu kubwa ya kujiokoa ni kukimbilia misikitini ambako swala ya ijumaa ilikuwa ikiendelea.
Wakizungumza baada ya tukio hilo badhi ya waathirika walisema mvua hiyo licha ya kuezua paa na kubomoa nyumba pia iliangusha miti ya mikorosho, na kuharibu vyakula vilivyoifadhiwa ndani na kwamba waziomba kampuni, watu binafsi, mashirika mbalimbali kuwasaidia katika kipindi hiki kigumu ambacho wanakabiliana nacho.

Paa limehezuliwa

“Hili janga lilitukuta jana majira ya saa saba (January 1), tena nilikuwa na umati wa watu humu ndani tena ni kujihifadhi kwa masuala ya ngoma, tukajikuta tumevamiwa na upepo mkali kabisa ambao ulitushinda kila idara..ikawa kazi ya mungu ikapita na sasa hatuna chakula, na tunashukuru serikali kupitia mhe. Diwani alichukua jukumu la kuwasiliana na uongozi wa wilaya na ulifika lakini tunachoomba ni serikali, makampuni ya dini, binafsi basi yaweze kutusaidia..” alisema Hassan Mzee.
Naye Salma Khatibu, aliiomba msaada kwa majirani zake na viongozi wa serikali kuweza kumsaidia kutokana na kubokewa na nyumba na kupoteza vyakula na vyombo ambapo hali hiyo inamuweka katika mazingira magumu ya kimaisha yeye pamoja na familia yake.
Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Tandahimba, Katani Ahmad (CUF) alisema mara baada ya kupata taarifa za tukio hilo aliwasiliana na mkuu wa wlilaya hiyo, Emmanuel Luhaula ambae kwa ahraka aliwasiliana na kamati yake ya ulinzi na usalama ambayo iliwahi kufika eneo la tukio kwa ajili ya kujua undani wake.
Alisema, baada ya mkuu huyo wa wilaya kuwasiliana na kamati ya maafa ya wilaya, lilitolewa agizo la kutolewa chakula kwa waathirika ambacho ni unga kg 25 na maharage kg 5 kwa kila kaya huku juhudi zaidi zikifanyika za kuwasiliana na mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego ambaye baadae aliwasili kijijini huko.

“Ninaamini na ninamatarajio makubwa sana na ofisi ya waziri mkuu ambayo mfuko wa maafa uko chini yake itatupa ushirikiano mkubwa sana na mimi kama Mbunge nitaendelea kusukuma jambo hili kuhakikisha kwamba tahafifu kwa waathirika hawa inapatikana kwa kuweza kuezekewa nyumba zao ili warudi katika hali ya kawaida..” alisema na kuongeza:
“Lakini wito wangu kwa wananchi wa Chaume, wawe watulivu, wawe na subra, wapole kwa wakati huu ambao tunapitia kwani hili ni janga ambalo mungu ndio amelipanga na wala sio binadamu, mungu akileta jambo lake kwa sisi waisilamu lazima tushukuru kwanza maana pengine kuna jambo amelinusuru kwasababu fikiria nyumba 150 lakini waliopata athari ni watu saba ambao kati yao watu sita wamerudi kwao na mgonjwa mmoja tu ndio yuko hospitali ya Newala akipata matibabu..” aliongeza Katani.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tandahimba, Namkulya Suleiman Namkulya, alisema pamoja na jitihada zilizoanza kufanyika lakini halmashauri hiyo itahakikisha inashirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuweza kufanikisha marekebisho katika shule zilizoatihirika na ofisi za serikali.
“Tunakusudia kuona mambo ya msingi kama vile shule pamoja na ofisi za serikali, hela ikitafutwa kwa haraka ili kuona namna ya kuweza kuhakikisha wanafunzi mpaka kufikia Januari 11 wanarudi shuleni na hizi ofisi za serikali angalau baada ya wiki moja au bili ziendelee kufanya shughuli zake kama kawaida.” Alisema.
Aliongeza kuwa katika kuonyesha ushirikiano katika jambo hilo, Benki ya NMB tawi la Tandahimba wameahidi kutoa msaada wa bati 120 huku halmashauri ikiendelea kutafuta wadau wengine ili kupata msaada zaidi pamoja na kuunganisha nguvu ya halmashauri hiyo kupitia pato lake la ndani.




No comments: