Kaimu mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Donald Sokko. |
Na Juma
Mohamed, Mtwara.
WANANCHI
waliovamia na kujenga katika maeneo ya wazi katika manispaa ya Mtwara Mikindani
wametakiwa kubomoa majengo yao wenyewe ili waweze kuokoa sehemu ya vifaa
ambavyo vitawasaidia katika matumizi mengine kuliko kusubiri manispaa ianze
kutekeleza zoezi hilo.
Akizungumza
na waandishi wa habari juzi ofisini kwake, kaimu mkurugenzi wa manispaa hiyo,
Donald Sokko, alisema iwapo wanachi watakaidi kutekeleza agizo hilo na kungoja
lifanywe na manispaa, watalazimika kulipia gharama za ubomoaji na kukosa hata
baadhi ya vifaa kama mabati na matofali.
“Naomba tu
nitoe rai kwa wananchi wote ambao wamevamia maeneo ya wazi, kwamba ni vizuri
wakabomoa wenyewe ili waweze kuokoa sehemu ya vifaa ambavyo walivitumia katika
ujenzi, kwasababu wakibomoa wenyewe itakuwa ni rahisi kuweza kupata matofali,
mabati kuliko manispaa itakapoingia gharama ya kubomoa, na zile gharama kila
mwananchi atazigharamia kwa fedha yake mwenyewe..” alisema.
Alisema,
tayari manispaa imeshawatambua wananchi ambao wamevamia maeneo hayo kutokana na
tathmini ambayo ilishafanyika na kuweza kuyabaini maeneo yote yaliyojengwa kwa
makosa, ambapo wahusika tayari wameshaandikiwa barua za ilani za kuwataka
kubomoa majengo yao.
Alisema,
ilani ambazo zimesambazwa kwa wavamizi hao ni zaidi ya 100 huku zikiwataka wale
ambao wana vielelezo vyovyote ambavyo viliwapa nguvu ya kujenga waviwasilishe
manispaa kwa ajili ya kuhakiki na kuweza kuwatambua watu ambao walitoa ruhusa
ya wao kujenga.
“Na kama
kutakuwa na mtumishi yoyote atakuwa amehusika katika kusababisha kwamba
wananchi wanajenga katika maeneo yanayomilikiwa na serikali, basi manispaa
itachukua hatua kali za kinidhamu katika kuhakikisha kwamba watumishi wa aina
hiyo hawafanyi kazi katika manispaa yetu..na ilani tuliowaandikiwa tuliwapa
siku 14, na siku hizo bado hazijaisha kwahiyo baada ya kukamilika ndipo hatua
zitaanza kuchukuliwa.” Alisema na kuongeza:
“Baadhi ya
maeneo ambayo wananchi wamevamia ni Shangani, maeneo ya Chuno na kiujumla
maeneo ni mengi na tayari tumeshasambaza ilani ili wananchi waweze kubomoa
wenyewe kwa hiyari yao..” aliongeza.
Baadhi ya
wananchi wanaoishi katika maeneo hayo walisema wanasubiri tu utekelezaji wa
zoezi hilo kwani hawana la kufanya kutokana na kukiri kuwa walijenga kimakosa.
“Kibali
mwanzoni tulipata tu kwa ajili ya bustani baadae tukaona kwasababu maji
yamepungua mzee akaona bora ajenge banda la kuku, kuhusu mabati tutaangalia kwa
mchana wa leo (juzi) pengine tunaweza kutoa..” alisema, Akwinata Haule, mkazi
wa mtaa wa Majengo kata ya Chuno.
No comments:
Post a Comment