Ngawina Ngawina, wakwanza kushoto akiwa katika bechi la ufundi katika moja ya michezo ya Ndanda ya ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara. |
KOCHA
msaidizi wa timu ya soka ya Ndanda Fc ya mkoani Mtwara Ngawina Ngawina
ametangaza kubwaga manyanga baada ya kushindwa kuvumilia shinikizo kutoka kwa
mashabiki wa timu hiyo la kumtaka ajiuzulu na kumuacha kocha mkuu Amimu Mawazo.
Akizungumza na
News Room kwa njia simu, Ngawina amesema amekuwa akiandamwa na maneno
makali kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo ya kumtaka afanye hivyo, na kwa
kulinda masilahi ya timu ameamua bora ajiuzulu ili kuhepusha shari.
"Nimetukanwa sana nimesemwa sana kwamba mimi ni chanzo cha matatizo kwahiyo nimeamua nikae pembeni ili Ndanda iendelee..wananchi wa Mtwara, siunajua ile timu ya wananchi bwana, na unajua mambo yakishafika katika vyombo vya habari, katika redio wanaongea..naona na mimi nina familia bora niangalie mambo mengine.." alisema Ngawina.
Kwa upande
wake, katibu wa klabu hiyo, Selemani Kachele alipoulizwa juu ya taarifa hizo
amesema amezisikia tu kupitia vyombo vya habari lakini bado hajapata taarifa
rasmi kutoka kwa kocha huyo ambaye amedumu na klabu hiyo tangu ilipopanda ligi
kuu.
"Mimi nimesikia kwenye vyombo vya habari, kwahiyo sisi bado hatujapata taarifa rasmi kupitia kwenye Email yetu bado haijafika, ila alinipigia simu jana na kuniambia kwamba anaweza asirudi tena maana alikua Dar (Dar es Salaam) kwa mapumziko ya siku Nne kwahiyo akasema yeye hatorudi tena.."
Katika mchezo
wa ligi kuu uliowakutanisha Ndanda na JKT Ruvu katika uwanja wa Nangwanda
Sijaona, Mtwara, mashabiki wa klabu hiyo walisikika kwa kipindi kirefu
kumshambulia kocha huyo kwa maneno wakimtaka aachie ngazi kwa madai kuwa
anaigawa timu na kutokuwa na maelewano mazuri na kocha mkuu Amimu Mawazo.
No comments:
Post a Comment