Wanafunzi wa shule ya msingi Kambarage, manispaa ya Mtwara Mikindani wakiwa katika harakati za usafi wa mazingira ya shule yao kabla ya kuingia darasani jana baada ya kufungua shule |
Na Juma
Mohamed, Mtwara.
BAADHI ya
shule za msingi katika manispaa ya Mtwara Mikindani zimeonyesha wasiwasi wao
juu ya kasi ya wanafunzi wanaojiandikisha na darasa la kwanza kuwa kubwa na
kuhofia kuzidi idadi inayokidhi mahitaji yao ya shule, jambo ambalo litapelekea
baadhi ya wanafunzi kukosa vyumba vya madarasa na madawati.
Wakizungumza
na Nipashe kwa nyakati tofauti, walimu wa kuu wa shule za Kambarage na Ligula
mjini hapa walisema kutokana na waraka wa elimu uliowafikia katika shule zao
kuwataka wasiwakatae wanafunzi, watalazimika kuwapokea hatakama watafikia idadi
inayokidhi mahitaji ya shule.
Hawana
Nacha, ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kambarage, alisema mpaka
kufikia jana asubuhi tayari walikuwa wameshawapokea watoto 120 na bado
wanaendelea kuwapokea wengine huku mahitaji ya shule ilikuwa ni watoto 100
kulingana na vyumba vilivyopo.
“Tumepokea
kulingana na waraka unavyosema, kwamba motto inabidi apokelewe na apokelewe
Yule ambaye yupo maeneo ya jirani na shule husika..wanaozidi tutawachomeka humo
humo ikishindikana watakaa nje watasoma huko, sasa hapo husipopokea lazima kuna
litalokukuta na hao wote wanatoka jirani na shule..” alisema.
Alisema, licha
ya mwaka huu kuwa na fursa ya elimu kutolewa bure, lakini kwa shule hiyo
imekuwa ni kawaida kwa wanafunzi kuwa wengi ambapo walikuwa wanalazimika
kuwapokea huku wengine wakikaa chini kwa kukosa madawati.
Aliitaka
serikali kuboresha miundombinu ya shule hiyo kwa kuongeza madawati, walimu na
vyumba vya madarasa ambapo jumla ya walimu waliopo ni 19 huku mahitaji ni
walimu 25 na kutokana na wanafunzi wa darasa la awali kukosa chumba,
wamelazimika kuchukua ofisi ya walimu kuifanya darasa.
Naye mwalimu
mkuu wa shule ya msingi Ligula, Angela Kariko, alisema shule yake ilikuwa ina
mahitaji ya wanafunzi 100 lakini kutokana na kasi ya kuwapokea wanafunzi wapya
wa darasa la kwanza inavyokwenda kuna uwezekano wa kuzidi idadi hiyo ambapo
mpaka kufikia jana asubuhi walikuwa wameshawapokea wanafunzi 95.
Alisema hiyo
ni changamoto kubwa kwa shule hiyo ambayo inaweza kusababisha baadhi ya
wanafunzi kukosa vyumba vya kusomea na hata madawati huku pia kukiwa na uhaba
wa walimu.
“Kwasababu
lengo ni watoto wote waingie darasani na wapate masomo tutawaingiza katika
vyumba hivi hivi vya madarasa vilivyopo na tutaendelea kuwafundisha huku
tukikabiliana na changamoto huku tukieleza ngazi zingine watusaidie..” alisema
Sofia Selemani, ambaye ni mratibu wa shule.
Kuhusu fedha
za kuteleza mpango wa elimu bure, alisema tayari zimeshaingizwa katika akaunti
za shule lakini hawajui ni kiasi gani kutokana na kwamba bado hawajaenda benki
kuangalia.
Kwa upande
wa shule ya sekondari ya Mtwara Ufundi, walisema tayari wameshapokea fedha
kiasi cha sh. Milioni 33 za kutekeleza mpango wa elimu bure zilizotolewa kwa
ajili ya matumizi ya mwezi nzima.
Akizungumza
ofisini kwake, kaimu mkuu wa shule hiyo, Ahmed Nachundu, alisema mpango huo
umesaidia kurahisisha baadhi ya majukumu katika ofisi ya msajili katika kipindi
hiki cha kupokea wanafunzi wapya ikiwa ni pamoja na zoezi la ulipaji ada na
kufuatilia maagizo mengine yanayohitajika kwa wanafunzi.
“Lakini sasa
hivi kutokana na mwongozo uliopo, mwanafunzi anakuja na kila kitu kwasababu ada
halipi, anakuja na yunifomu, godoro anakuwa ameshanunua hukohuko, hakuna kuja
na jembe, fagio wala kifaa chochote..kwahiyo utofauti ndio huo ukilinganisha na
miaka ya nyuma..” alisema.
Baadhi ya
wazazi walioambatana na watoto wao kwa ajili ya kwenda kuwaandikisha elimu ya
msingi, walielezea furaha yao juu ya mpango huo na kusema umesaidia kwa kiasi
kikubwa kupunguza majukumu ya mzazi kwa mwanafunzi, huku wakikiri kuto takiwa
kuchangia kitu chochote zaidi ya kutekeleza wajibu wao wa kuwaandaa watoto kwa
yunifomu, daftari na kalamu.
Kuhusu
changamoto zilizoelezwa na walimu wa shule za Kambarage na Ligula, kaimu
mkurugenzi wa manispaa ya Mtwara Mikindani, Donald Soko, alisema licha ya
changamoto hizo, walimu wanatakiwa kuendelea kuwapokea wanafunzi kama maagizo
yanavyosema na kwamba kama kuna changamoto zozote wanatakiwa kuwasiliana na uongozi
wa manispaa.
Alisema,
manispaa itajua cha kufanya maana inawezekana kuna shule nyingine ambazo
hazitafikisha idadi ya mahitaji ya shule, hivyo kwa wale watakaozidi itabidi
watafutiwe shule nyingine ambazo zitakuwa na nafasi.
“Mimi
nadhani wasiwe na wasiwasi sana kwasababu inawezekana labda wazazi wamehamasika
na kupeleka watoto shule, kwahiyo wasijenge dhana kwamba ni lazima watoto wazidi,
inamaana kama watoto watazidi kwa kiwango hicho cha 100 ambacho wao
watakihimili basi wawasiliane na uongozi wa manispaa..” alisema.
No comments:
Post a Comment