Thursday, June 4, 2015

JENGO LA USHIRIKA KUANZA KUWANUFAISHA WANACHAMA

Viongozi wa vyama vya ushirika vya mikoa ya Lindi na Mtwara, wakiwa katika semina ya uhamasishaji wa ununuzi wa hisa za jengo la Ushirika lililopo mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, katika ukumbi wa VETA mjini Mtwara.


Mrajisi Msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Mtwara, John Henjewele, akifungua semina ya uhamasishaji kwa viongozi wa vyama vya ushirika juu ya ununuzi wa hisa za jengo la Ushirika lililopo mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, katika ukumbi wa VETA mjini Mtwara.





Na Juma Mohamed, Mtwara.

VYAMA vya ushirika vya mikoa ya Lindi na Mtwara vimetakiwa kuwahamasisha wanachama wao juu ya umuhimu wa kununua hisa katika jengo la Ushirika, lililopo mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, ili waweze kunufaika na rasilimali hiyo.

Akizungumza katika semina ya uhamasishaji wa ununuzi wa hisa za jengo hilo, ilioandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) na kufanyika katika ukumbi wa VETA mjini Mtwara, Mrajisi Msaidizi wa vyama vya Ushirika mkoa wa Mtwara, John Henjewele alisema, lengo kuu la semina hiyo ni kuwajengea uwezo viongozi wa vyama vya ushirika vya mikoa ya Lindi na Mtwara kwenda kusambaza elimu watakayoipata, kwenye vyama vyote ili waweze kununua hisa kwa wingi katika dhana halisi ya uwekezaji wa pamoja.

Naye, katibu mtendaji wa TFC, Willigis Mbogoro, alisema mfumo wa sasa wa uwekezaji katika ushirika haumnufaishi mwanachama wala vyama vyenyewe isipokuwa unanufaisha taasisi na watu wa nje kwasababu vyama vya ushirika ndivyo vyenye uwezo wa kukopa na hata kununua pembejeo za kilimo, na dio sababu sirikisho hilo likaamua kuja na mfumo wa dhana ya uwekezaji wa pamoja ili mwanachama aweze kunufaika.

“Januari 14 mwaka huu, wanaushirika walikutana kule Dodoma wakaanzisha taasisi ya uwekezaji wa pamoja ya ushirika, na kwakuanzia tumeanza na lile jengo la ushirika (Ushirika Towers Co-operative Joint Enterprise), ni taasisi ambayo tayari imekwishaanzishwa kutokana na huo mkutano.” Alisema Mbogoro.

Katibu wa chama cha ushirika cha Muungano, mkoani hapa, Abdulrahman Abdul, alisema kama kweli shirikisho hilo likitekeleza mambo yote waliyoahidi ikiwa ni pamoja na kunzisha benki ya pamoja, kununua hisa kutoka katika jengo la ushirika na kufufua kiwanda cha kuchapisha vitabu, itasaidia kuboresha na kuongeza kipato kwa wanaushirika ambao hali zao ni duni kwa sasa kwa kukosa nguvu ya pamoja.

……………………….mwisho……………………………………………….

No comments: