Thursday, April 16, 2015

'WANANCHI TUMIENI MITANDAO KWA MAENDELEO NA SIO MATUSI'




 
Katibu Tawala wa wilaya ya Masasi, Danford Peter

Wanakikundi cha ngoma ya asili wakitumbuiza

Danford Peter, akipokea zawadi ya simu kutoka TTCL

Danford Peter, akipokea zawadi ya simu kutoka TTCL

Mnara wa mawasiliano wa TTCL uliozinduliwa

Danford Peter, mwenye koti jeupe akizindua mnara wa mawasiliano wa TTCL

Danford Peter, akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa TTCL

Mnara wa TTCL uliozinduliwa juzi, Lupaso, wilayani Masasi.



Na Juma Mohamed, Masasi.


Wananchi wametakiwa kuwa na matumizi mazuri ya simu na mitandao kwa ujumla na kuepuka kuitumia kinyume na taratibu ambapo baadhi ya watu hutumia kwa kutoa lugha za matusi, picha zisizo na maadili ya Kitanzania na ujumbe unaoashiria uchochezi.
Wito huo ulitolewa juzi na Katibu Tawala wa wilaya ya Masasi, Danford Peter, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mnara wa mawasiliano wa kampuni ya simu Tanzania (TTCL), katika kata ya Lupaso wilayani Masasi.
Alisema baadhi yawatu wamekuwa wakikiuka taratibu za matumizi ya mitandao kwa kurusha picha zisizoendana na maadili ya nchi yetu na kwamba uwepo wa sheria ya mitandao itasaidia kuwabana watu wa aina hiyo.
Aidha, Peter aliwataka wakulima kutumia simu na mitandao mingine kwa kutafuta masoko ya mazao wanayoyapata kutokana na kilimo ndani na nje ya maeneo yao wanayoishi kwa ajili ya kukuza kipato.
Alisema mitandao ni njia mojawapo ya kutangaza kiasi cha mazao yaliyopatikana hasa mazao ya ufuta, alizeti, choroko na korosho ambalo ndio zao kuu la biashara kwa mkoa wa Mtwara, na kwa kufanya hivyo wanunuzi watapa kufahamu wastani wa uzalishaji wa mazao katika maeneo husika.
“Tunafahamu kwamba korosho ndio zao pekee linalowapatia wananchi wetu kipato..sasa mitandao hii ni njia mojawapo ya kutangaza kwamba tunakorosho kiasi gani sisi tuliopo hapa Lupaso, tuna ufuta kiasi gani tuliozalisha, tuna alizeti kiasi gani tuchozalisha ambacho tunahitaji soko..sasa njia pekee ya kuwasiliana na kutangaza hivyo vitu ni kupitia mitandao.” Alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa TTCL mkoa wa Lindi ambae alimwakilisha mkurugenzi wa kanda ya Zanzibar na kusini, Nicodemus E. Mngulu, alisema kupitia mfuko wa kusimamia utoaji wa huduma ya mawasiliano kwa wote nchini (UCSAF), kampuni hiyo ilipewa jukumu la kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 20 katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa mawasiliano vijijini.
“Katika kata hizo za mwanzo, Lupaso na Lipumbulu ni mojawapo ya kata zilizonufaika na mradi huo. Hii ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha upatikanaji wa mawasiliano kwa urahisi zaidi na pia kuchangia ukuaji wa maendeleo katika maeneo ya vijijini.” Alisema Mngulu.
Mnara huo uliozinduliwa unakuwa ni mnara wa tano wa kampuni hiyo kwa mkoa wa Mtwara, na kwamba unatoa huduma katika vijiji vitatu vya Lupaso, Mchoti na Lipumbulu vyenye wakazi zaidi ya 2,000, kwa mujibu wa sense ya watu na makazi ya mwaka 2012.

……………………..mwisho………………………………………………………..

No comments: