![]() |
| Mkuu wa wilaya ya Newala, Christopher Maghalla |
![]() |
| Christopher Maghalla na Mweka Hazina wa MRENGO, Mustafa Kwiyunga |
![]() |
| Wadau waliohudhuria warsha ya kutathimini fursa na changamoto zinazowakumba vijana katika kujiletea maendeleo ngazi ya jamii, wilayani Newala. |
Na Juma Mohamed, Newala.
VIJANA
wilayani Newala wametakiwa kujihusisha na shughuli za ujasiliamali ili kuweza
kujikwamua kimaisha na kuepukana na hali ya umasikini inayowakabili vijana
wengi wasiyojishughulisha hapa nchini.
Wito huo
umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Newala, Christopher Maghalla, wakati
akifungua warsha ya kutathimini fursa na changamoto zinazowakumba vijana katika
kujiletea maendeleo katika ngazi ya jamii, iliyoandaliwa na mtandao wa asasi
isiyo ya kiserikali (NGO) ya MRENGO ya mkoani Mtwara, iliyofanyika katika
ukumbi wa haspitali ya wilaya ya Newala.
Alisema
serikali inahamasisha vijana waungane katika makundi mbalimbali ili iweze
kuwasaidia kwa lengo la kutatua changamoto za kiuchumi ambazo zimekuwa
zikiwakumba vijana wengi hapa nchini, kiasi cha kupelekea wengine kujihusisha
na vitendo visivyokubalika vya uvunjifu wa sheria.
"Serikali
kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo inatenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya kuwasaidia
vijana..hii ni kuonesha ni jinsi gani serikali yetu inajali masilahi ya
vijana." alisema Magalla.
Aidha, Mkuu
huyo wa Wilaya alitoa mfano yeye mwenyewe namna ambavyo alijipatia elimu ya
sekondari, kuwa ni kutokana na juhudi zake mwenyewe ambapo aliamua kuungana na
kaka yake na kuanza kufanya shughuli ya kusukuma mkokoteni kwa kupeleka nyanya
sokoni na baadae ikamsaidia kujipatia kipato ambacho aliamua kuanza shughuli za
kilimo cha zao hilo.
Alisema
kutokana na kipato alichokuwa akipata kutokana na kuvuna nyanya, kilimuwezesha
kufungua saluni, na baadae kujikuta akisoma bila vikwazo vyovyote vya kipato na
kutokuwa na utofauti kati yake na watoto waliotoka katika familia za kitajiri.
Katika
hatua nyingine, Magalla amewataka wananchi wote wa wilaya ya Newala na maeneo
mengine kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kujiandikisha katika daftari la
wapiga kura, na wale wanaojiona kuwa na vigezo vya kugombea nafasi mbalimbali
za uongozi wafanye hivyo, kwani kwa kufanya hivyo itasaidia nchi kuepukana na
kuwa na viongozi mafisadi na wasiokuwa na maadili.
Kwa upande
wake, mratibu wa warsha hiyo, Shaibu Kasulo, alisema warsha hiyo inafanyika
chini ya mradi wa Fahamu, Ongea, Sikilizwa Election (ii) ambao unaangalia
masuala mbalimbali ikiwa pamoja na swala la kupiga kura, kujiandikisha katika
daftari la wapiga kura pamoja na kufanya tafiti mbalimbali kuhusu wananchi
wanavyoshiriki katika upigaji kura.
Alisema
mradi umegundua kuwa asilimia kubwa ya wananchi ambao ushiriki wao ni mdogo
katika upigaji kura ni vijana na akina mama. Alitoa takwimu za jumla za namna
wananchi walivyosiriki katika zoezi la upigaji kura, ambapo alisema katika
uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, ushiriki ulikuwa ni kwa asilimia 84.4, mwaka 2005
ulikuwa kwa asilimia 72.4 na mwaka 2010 ni asilimia 42.8 hivyo kuonekana
ushiriki wa wananchi unazidi kupungua kadiri miaka inavyozi kwenda.
..............................mwisho.......................................................................



No comments:
Post a Comment