Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) limefanyia marekebisho kanuni zake za michuano ya ngazi ya klabu kwa
upande wa malazi ambapo sasa timu zitachagua na kujilipia zenyewe hoteli
zinapokuwa kwenye mechi za ugenini.
Kabla ya marekebisho ya kanuni hiyo,
timu ngeni ilikuwa ikilipiwa hoteli na timu mwenyeji kwa msafara usiozidi watu
25. CAF ilikuwa imepitisha hoteli maalumu katika kila nchi ambapo mwenyeji
alitakiwa kuziweka timu ngeni.
Kwa marekebisho hayo, Chama cha Mpira wa
Miguu cha nchi mwenyeji kitakuwa na wajibu wa kuitafutia hoteli timu ngeni
iwapo tu kitaombwa kufanya hivyo, lakini jukumu la kulipia malazi litakuwa la
timu yenyewe.
Mwaka huu Tanzania inawakilishwa na timu
mbili za Azam na Yanga katika michuano ya CAF. Azam inacheza Ligi ya Mabingwa
(CL) ambapo itaanzia nyumbani Februari 15 mwaka huu kwa kuikaribisha El
Merreikh ya Sudan kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.
Nayo Yanga itacheza michuano ya Kombe la
Shirikisho (CC), na imepangiwa kucheza mechi ya kwanza nyumbani dhidi ya BDF IX
ya Botswana. Mechi hiyo itafanyika Februari 14 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment