Sunday, May 13, 2012


SIMBA, YANGA TAJIRI KULIKO BAKHRESA, BASI TU...


Jengo la Yanga, ambalo linawezwa kuboreshwa zaidi na kuingtiza fedha zaidi, ambalo limeambatana na Uwanja wa kaunda, uliozungushiwa mabati. Tuseme kwenye miti hakuna wajenzi? Jengo hili lipo tangu Bakhresa hajanunua boti hata moja na bado anauza koni tu.

KATIKA sheria 17 za soka, sheria ya kwanza ni Uwanja. Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) linatoa uzito mno katika suala la Uwanja.
Kwa nini Uwanja? Katika akili ya kawaida, kama tunataka kucheza soka, jambo la kwanza na la msingi kutilia mkazo ni Uwanja.
Ndiyo, ni hivyo. Lakini je, viongozi wa klabu zetu kongwe nchini Simba na Yanganao wana frikra kama hizo? Sidhani. Wakati tumekaribia mno kwenye kilele cha sherehe za miaka yetu 50 ya Uhuru, Simba na Yanga zinafurajia kuwapo kwa zaidi ya 75 na ushehe tangu kuanzishwa kwake.
Wakati huo huo, nchini kuna klabu nyingine za soka zinakimbiza siku ili angalau zitimize muongo mmoja tu tangu kuanzishwa kwake.
Ila leo akija mgeni na kutambulishwa kwa klabu zote nchini, zikiwemo ambazo zina miaka zaidi ya 75 tangu kuanzishwa kwake na zile change, itakuwa vigumu kumshawishi akubaliane na hali halisi.
Mpokee mgeni na uanze kumtembeza- anzia Mtaa wa Msimbazi, muonyeshe makao makuu ya klabu ya Simba, ajionee lile jingo chakavu na lile pembeni yake ambalo halijaisha.
Mtoe hapo mpelekea makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani- muonyeshe makao makuu ya klabu ya Yanga- ajionee eneo kubwa linaloweza kuwa la kifahari siku moja tu, akipatikana mtu wa kuliendeleza.
Baada ya hapo, mpeleke Mbagala, eneo la Chamazi ambako kuna makao makuu ya Azam FC na muonyeshe Uwanja mpya mdogo na wa kisasa mithili ya viwanja vingi ambavyo vipo nchi za Scandinavia barani Ulaya.
Mkutanishe na Patrick Kahamele, amtembeze kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ya soka klabu, ikiwemo soka ya vijana.
Mkutanishe na wenye timu wampe mipango yao ya baadaye- tena iliyo katika maandishi na mikakati ya utekelezaji wake.
Baada ya hapo mpe wasifu wa hizo klabu kwamba Simba na Yanga zipo tangu nchi hii haijapata Uhuru na Azam haina hata miaka mitano tangu ianzishwe.
Lazima atashangaa. Lazima atastaajabu. Hii nini maana yake? Viongozi wa Simba na Yanga bado hawajajitambua. Bado hawajatambua soka inahitaji vipaumbele gani na kama hivyo ndivyo.
Inaonekana dhahiri viongozi wa Simba na Yanga hawana dira wala mipango na watu wa aina hiyo, kutoka mikononi mwao ni vigumu mno klabu hizo kupiga hatua, hata ndogo ndogo tu za kimaendeleo.
Ukubwa wa majina ya Simba na Yanga na umaarufu wake, pekee ni mtaji mkubwa wa kuendesha klabu hizo, ambao inasikitisha hadi haujatumiwa na viongozi wa klabu hiyo kuzinufaisha klabu hizo.
Bado inasikitisha kuona hadi kesho, kitegauchumi kikubwa cha Simba na Yanga ni ‘bakuli’- yaani kutembea kwa matajiri na wafanyabiashara kuomba misaasa.
Kwa sasa Yanga wana mgogoro na chanzo ni hali mbaya ya kifedha ndani ya klabu, kama ilivyoanishwa na Wajumbe wawili waliong’atuka, Seif Ahmad ‘Magari’ na Abdallah Bin Kleb na wakati Fulani ilibidi Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga aende kumbembeleza Yussuf Manji arejeshe ufadhili wake kwenye klabu hiyo.
Dhahiri, Nchunga aliamua kufanya hivyo baada ya kuona mambo ni magumu na klabu haiwezi kujiendesha bila msaada.
Lakini Nchunga labda tu awe hajui historia ya klabu yake- ni klabu ambayo hadi mwaka 1975, ikiwa haina ufadhili wowote, tayari ilikuwa ina majengo yake mawili, dogo Mtaa wa Mafia na hilo kubwa la Jangwani, ambalo linaambatana na Uwanja wa Kaunda.
Ilikuwa ina mabasi yake ambayo mengine yalikuwa yanatumika kwa shughuli za klabu na mengine yanatumika kibiashara.
Kadhalika kwa Simba, hadi 1975 ilikuwa ina jengo lake wakati huo likiwa la kifahari na linalong’ara na kuupendezesha Mtaa wa Msimbazi- miaka hiyo Mwenyekiti wa Simba Alhaj Ismail Aden Rage aliwahi kufika Dar es Salaam na kujaribu kutaka kuichezea klabu hiyo, lakini kiwango chake kidogo hakikumpa nafasi, aliishia kujaribiwa kwenye mechi kadhaa.
Simba ilikuwa ina mabasi pia- na haikuwa na mfadhili yoyote, zaidi ya ujanja na fikra za viongozi wa klabu hiyo.
Unaweza kuona kabisa hali ilivyo leo Simba na Yanga ukilinganisha na miaka hiyo, maana yake haziendelei zaidi ya kudumaa. Wengi wanaamini elimu kubwa ndio msingi wa maendeleo- sahihi kabisa. Leo viongozi wa Simba na Yanga ni wenye elimu za viwango vya juu na wana taaluma. Rage Mhasibu na Nchunga Mwanasheria.
Lakini viongozi wa Yanga wa miaka hiyo, hawakuwa na elimu kubwa, ila mambo waliyoyafanya yanawafanya thamani yao iwe juu kuliko hawa waliokaa shule muda mrefu.
Dunia ya leo ni nyepesi mno kwa mtu ambaye kweli anataka maendeleo. Taasisi kubwa kama zilivyo Simba na Yanga hivi sasa zinakopesheka na mabenki ni mengi mno nchini ambayo yanaweza yakazipa mikopo klabu hizo zifanye miradi yao ya maendeleo.
Yanga wana Uwanja wa Kaunda ambao wanaweza kuuboresha, ukawa Uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kukusanya hata watu 20, 000 katika mechi moja na kuujingizia fedha nyingi.
Hivi kweli Yanga wamekwishazungumza hata na mdhamini wao tu Kilimanjaro Beer juu ya kuwasilisha programu ya kuuendeleza Uwanja wa Kaunda?
Naamini, TBL watakuwa tayari kutumia kuta za Uwanja wa Kaunda kujitangaza kibiashara- iwapo Yanga watawasilisha mapendekezo ya mradi yaliyosimama.
Watu 20,000 kila wiki mara mbili wanamiminika Uwanja wa Kaunda kutazama mechi- au watu wasiopungua 5,000 kila siku kwenye mazoezi ya kikosi cha kwanza- ni kiasi gani TBL itakuwa inanufaika?
Lakini Yanga nayo itakuwa inapata kiasi cha fedha?
Azam ‘walilaani’ kweli Uwanja wa Taifa ulipofunguliwa, kwani yale makato ya Uwanja waliyokuwa wanayapata kila mechi ambayo SImba au Yanga ilicheza Chamazi yaliota mbawa. Sasa tunataka nini ili kujua umuhimu wa kuwa na Uwanja?
Lakini si TBL tu, yapo makampuni mengine ambayo yanajua soka ina wapenzi wengi na yanaweza kunufaika kwa kuwekeza huko, je Yanga wamekwishayafikia?
Mradi wa ujenzi barabara ya Jangwani inalifanya eneo hilo liwe mjini kabisa na kuuweka sokoni zaidi Uwanja wa Yanga- je Nchunga na viongozi wenzake wanafikiria nini?
Azam wamejenga Uwanja wao Mbagala na tumeshuhudia msimu huu mashabiki wa Simba na Yanga wakienda kuzishangilia timu zao kwenye Uwanja huo, inakuwaje Simba wanashindwa kujenga Uwanja nje ya mji japokuwa walishindwa kuwa na eneo mjini?
Soka ni biashara kubwa ambayo mtaji wake mkuu ni Uwanja- ndio maana klabu zote Ulaya hata ndogo zina viwanja vyake. Ulaya itaendelea kuwa kioo chetu daima.
Wanachokifanya Rage na Nchinga kwa sasa ni kitu ambacho hata Rashid Ngozoma Matunda (sasa marehemu) na Hassan Daalal walikifanya klabu yao.
Uongozi wa staili ya kusajili wachezaji, kuweka timu kambini, kuisafirisha mikoani kucheza mechi na kukusanya mapato ya milangoni, hata yule mwanachama wa Simba mlemavu anayeitwa Kipukuswa au Soud Tall wa Yanga wanaweza kuufanya.
Nani atashindwa? Lakini Rage na Nchunga wanapaswa kujitambua sasa na kuhakikisha wanafanya kitu ambacho kitawafanya wakumbukwe na kuwa sehemu ya historia ya klabu hizo.
Wasome historia ya Simba na Yanga na baada ya hapo waache blah blah na usanii, ni mambo ambayo yamekwishapitwa na wakati.
Waonyeshe wanajiamini na kutumia ukubwa wa majina ya klabu hizo na umaarufu wake kuzipatia mafanikio klabu hizo.
Ona sasa Azam inayowaacha ‘uchi’- timu ya juzi tu, lakini ina mipango. Na hapa kisingizio kisiwe Bakhresa ana fedha hapana, ana mipango na malengo, kwani wapo wenye fedha waliojaribu kuwekeza kabla yake, mfano Mohamed Dewji, Alex Kajumulo na Merey Balhaboub na wakafeli.
Bado naamini Simba na Yanga kila moja ni tajiri kuliko Bakhresa, ila sasa hazina watu wenye kuweza kuchimba dhahabu, kusafisha na kuiingiza sokoni. Na kwa mtaji huu, zitaendelea kuwa za kubahatidha tu- mfano Simba mwaka huu wanafanya vizuri Afrika, baada ya hapo hadi miaka 10 tena baadaye.
Ndiyo- nani asiyejua mafanikio ya Simba ni ya kubahatisha? Walikuwa wana mipango gani mwanzoni mwa msimu hata tuseme wanavuna walichopanda? Weka unazi kando- jadili hili kwa kina, ukirejea ule usajili wa kubahatisha bahatisha- ambao chupuchupu umtupe nje ya kikosi Emmanuel Okwi msimu huu, ambaye sasa ndiye anaibeba timu?
Au tumesahau jamani, huyu mchezaji si alikwenda Afrika Kusini na klabu ilikuwa tayari kumuuza kwa kumuona hana manufaa, ila alipokwama kwa sababu alikuwa hajamaliza mkataba, akaambiwa arejee kikosini.
Umefika wakati sasa tuweke unazi kando ili kuzisaidia SImba na Yanga- zinatia kichefuchefu, tunazipenda basi tu!

RATIBA YA MECHI ZA KUFUNGA MSIMU ENGLAND LEO NA MUDA KIBONGOBONGO, MSIMAMO NA WAFUNGAJI WOTE WA MABAO

Silva na Tevez wa Man City, inayotarajiwa kutwaa ubingwa leo

Barclays Premier League | RATIBA

Mechi zote Live Super Sport TV
Sunday 13 May 2012
Chelsea v Blackburn Stamford Bridge Saa11:00jioni
Everton v Newcastle Goodison Park Saa11:00jioni Preview
Man City v QPR Etihad Stadium Saa11:00jioni Preview
Norwich v Aston Villa Carrow Road Saa11:00jioni
Stoke v Bolton Britannia Stadium Saa11:00jioni
Sunderland v Man Utd Stadium of Light Saa11:00jioni Preview
Swansea v Liverpool Liberty Stadium Saa11:00jioni
Tottenham v Fulham White Hart Lane Saa11:00jioni Preview
West Brom v Arsenal The Hawthorns Saa11:00jioni Preview
Wigan v Wolverhampton The DW Stadium Saa11:00jioni

Barclays Premier League | MSIMAMO

Pos Team P W D L GF GA GD Pts
1 Man City 37 27 5 5 90 27 63 86
2 Man Utd 37 27 5 5 88 33 55 86
3 Arsenal 37 20 7 10 71 47 24 67
4 Tottenham 37 19 9 9 64 41 23 66
5 Newcastle 37 19 8 10 55 48 7 65
6 Chelsea 37 17 10 10 63 45 18 61
7 Everton 37 14 11 12 47 39 8 53
8 Liverpool 37 14 10 13 47 39 8 52
9 Fulham 37 14 10 13 48 49 -1 52
10 West Brom 37 13 8 16 43 49 -6 47
11 Sunderland 37 11 12 14 45 45 0 45
12 Swansea 37 11 11 15 43 51 -8 44
13 Norwich 37 11 11 15 50 66 -16 44
14 Stoke 37 11 11 15 34 51 -17 44
15 Wigan 37 10 10 17 39 60 -21 40
16 Aston Villa 37 7 17 13 37 51 -14 38
17 QPR 37 10 7 20 41 63 -22 37
18 Bolton 37 10 5 22 44 75 -31 35
19 Blackburn 37 8 7 22 47 76 -29 31
20 Wolverhampton 37 5 10 22 38 79 -41 25

Barclays Premier League | WAFUNGAJI WA MABAO
Van Persie anayeongoza kwa mabao


Player Team Goals
Robin van Persie Arsenal 30
Wayne Rooney Man Utd 26
Sergio Aguero Man City 22
Clint Dempsey Fulham 17
Ayegbeni Yakubu Blackburn 16
Demba Ba Newcastle 16
Emmanuel Adebayor Tottenham 16
Grant Holt Norwich 14
Edin Dzeko Man City 13
Mario Balotelli Man City 13
Papiss Cisse Newcastle 13
Daniel Sturridge Chelsea 11
Danny Graham Swansea 11
Frank Lampard Chelsea 11
Luis Suarez Liverpool 11
Rafael Van der Vaart Tottenham 11
Steven Fletcher Wolverhampton 11
Gareth Bale Tottenham 10
Javier Hernandez Man Utd 10
Jermain Defoe Tottenham 10
Peter Crouch Stoke 10
Peter Odemwingie West Brom 10
Danny Welbeck Man Utd 9
Darren Bent Aston Villa 9
Steve Morison Norwich 9
Total 996

No comments: