Monday, April 9, 2012

SUPERSPORT KUONYESHA LIVE MSIBA WA KANUMBA

Kanumba
KAMPUNI ya M-Net itaonyesha kwa dakika 15 katika Televisheni ya Super Sport kupitia chaneli ya African Magic msiba wa aliyekuwa mwigizaji nguli wa filamu Tanzania, Steven Kaumba aliyefariki usiku wa wa kuamkia Jumamosi, Dar es Salaam.
Mjumbe wa Kamati ya Mazishi ya Kanumba, Rugemarila Mutahaba ameiambia bongostaz kwamba watakachokifanya ni kutengeneza documentary ya pamoja ya mfululizo wa matukio yote ya msiba huo tangu Alfajiri ya Jumamosi hadi kesho atakapozikwa.
Mapema leo, Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Kayanza Peter Pinda alifika nyumbani kwa marehemu kuhani msiba huo.
Pinda akiwa nyumbani hapo, Sinza Vatican, aliwaasa wasanii kuendeleza mazuri ya Kanumba na kujenga upendo baina yao, kuondoka makundi, ili iwe rahisi hata kwa serikali kuwasaidia.
Jana, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete alifika nyumbani kwa marehemu, Sinza Vatican kuhani msiba.
Akiwa msibani, Kikwete alisema kwamba kifo cha Kanumba ni pigo kubwa kwa tasniya ya filamu Tanzania, kwa msanii huyo alikuwa mwenye jitihada na kuthubutu katika kutaka kutimiza malengo yake.
Kikwete alisema Kanumba amefanikiwa kuitangaza nchi na sanaa ya filamu za nchi hii katika anga za kimataifa. Hata hivyo, rais Kikwete alisema hatuna kukubali juu ya kifo cha msanii huyo, kwani ni kazi ya Mungu.
Mama wa marehemu amewasili na amekubaliana na Kamati ya Mazishi mwili wa marehemu uzikwe katika Makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam Jumanne.
Kamati ya Mazishi, imefanikiwa kumshawishi mama huyo aliyetokea Bukoba, akubali Kanumba azikwe Dar es Salaam, baada ya awali kuwapo hofu angependa mwanawe azikwe Shinyanga.
Mwili wa marehemu unatarajiwa kuagwa Jumanne katika viwanja vya Leaders, Dar es Salaam na baada ya hapo ndipo litafuatia zoezi la mazishi makaburi ya Kinondoni.
Taarifa ya awali ya Polisi, imesema pombe kali (Whisky) aina ya Jack Daniels, ndio imesababisha kifo cha Kanumba.
Kamanda wa Polisi Kinondoni, ACP Charles Kenyela alisema jana kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha hivyo, lakini bado wanaendelea na uchunguzi zaidi, ili kujua zaidi.
ACP Kenyela amesema kwamba Kanumba wamefanikiwa kumuhoji mtuhumiwa wa kwanza katika tukio hilo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na katika maelelezo yake amekanusha kumsukuma Kanumba.
Vyombo vingi vya habari vilimnukuu ndugu wa Kanumba, Sethi jana akisema kwamba Lulu alimsukuma mwigizaji mwenzake huyo katika ugomvi wao wa wivu wa kimapenzi hadi akaanguka na kufariki dunia.
Akizungumza kutokana na maelezo ya Lulu, Kamanda huyo alisema kwamba; ugomvi wao ulitokana na Kanumba kutaka kumdhibiti Lulu wakati akizungumza na simu.
“Kanumba aliamua kumfuata Lulu nje huku akifoka kwa sauti, akitaka aelezwe kwa nini alitoka nje kupokea simu, huku akimtuhumu kuwa huenda alikuwa akizungumza na mwanaume mwingine.
Baada ya Lulu kuona Kanumba anamfuata, aliamua kukimbia kutoka nje ya geti, lakini kabla hajafanikiwa kufungua geti, Kanumba  alimkamata na kumrudishwa ndani. Kanumba akiwa amemshikilia, waliingia wote chumbani na kufunga mlango. Sasa haijulikani nani aliyefunga mlango, ingawa maelezo ya Lulu, anadai kuwa aliyefunga mlango ni Kanumba,”alisema Kamanda huyo.
Akiendelea kumnukuu Lulu, Kamanda huyo anasema; “Baada ya Kanumba kufunga mlango, alimuona akilegea na kujigonga kisogo chake kwenye ukuta wa chumba hicho kabla ya kuanguka chini,”alisema.
Alisema uchunguzi wa tukio zima ukikamilika, hatua inayofuata ni kumpeleka Lulu mahakamani kama mtuhumiwa wa mauaji.

HISTORIA YAKE:
Steven Charles Kanumba alizaliwa Januari 8, mwaka 1984, mkoani Shinyanga, kabla ya umauti kumfika Aprili 6, mwaka 2012.
Elimu ya msingi alipata katika shule ya Bugoyi, Shinyanga na baadaye akajiunga na sekondari ya Mwadui, kabla ya kuhamia Dar Christian Seminary.
Baada ya kumaliza Kidato cha Nne Dar Christian, Kanumba alijiunga na sekondari ya Jitegemee, Dar es Salaam pia kwa elimu ya Kidato cha Tano na Sita.
Ni wakati huo akiwa Jitegemee, Kanumba alianza shughuli za sanaa katika Kundi la Kaole Sanaa Group la Magomeni, Dar es Salaam.
Baada ya kukomaa Kaole, Kanumba aliamua kuanzisha kampuni yake mwenyewe ya filamu na hadi anakutwa na umauti alikuwa mwigizaji anayefahamika Afrika nzima.
Ameshirikiana na wasanii wakubwa duniani kama Ramsey Nouah wa Nigeria na amefanya kazi na mastaa wengine kadhaa wa Nigeria.
Miongoni mwa filamu ambazo alifanya ni Dar To Lagos, She is My Sister, Ancle JJ, Oprah, Tufani, Johari, Gharika, Baragumu, Sikitiko Langu, Dangerous Desire, Cross My Sin, Village Pastor, Family Tears na kadhalika.
Hivi karibuni, alikaririwa akisema atagombea Ubunge katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.
Kanumba atakumbukwa na wengi sana kwa ucheshi wake- upole na ushirikiano mzuri na wenzake katika kazi.
Kifo cha Kanumba ni pigo katika tasniya ya filamu Tanzania. Taifa limempoteza mtu ambaye alikwishaanza kuitangaza vema nchi kupitia sanaa hiyo na ambaye angetarajiwa kuitangaza zaidi katika anga za kimataifa zaidi kupitia sanaa hii.
Nigeria sasa wanajua Tanzania kuna filamu. Nchi nyingi za Afrika zinajua sasa na hii sehemu ya kazi nzuri ya Kanumba.
Mwenyewe aliwahi kukaririwa alifika hadi Hollywood, Marekani, ambayo ni ‘makka’ ya wacheza filamu. Kwa sasa mwili wa marehemu upo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam. Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amin.

No comments: