Tuesday, April 10, 2012

BALOTELLI AOMBA RADHI

Balotelli kulia na Tevez kushoto katika mechi ya Jumapili
MSHAMBULIAJI wa Manchester City, Mario Balotelli leo ameomba radhi mjini Milan kwa utovu wake wa nidhamu na ameomba asiondolewa timu ya Taifa ya Italia kwa ajili ya Kombe la Mataifa ya Ulaya.
Alilimwa kadi nyekundu ya nne katika misimu miwili akiwa na City timu yake ikilala 1-0 mbele ya Arsenal Jumapili, jambo ambalo limeibua swali, huenda Balotelli amevunja agizo la nidhamu na uadilifu lililowekwa na kocha wa Italia, Cesare Prandelli.
“Samahani sana kwa kilichotokea kwa pigo nililoisababishia Manchester City, na maalum kwa (kocha) Roberto Mancini, ambaye ninamzimikia na kumtakia mema,” Balotelli alisema katika taarifa yake iliyotolewa na shirika la habari la ANSA na wakala wake, Mino Raiola.
“Ninahusika sana katika timu ya taifa, lakini jana nilicheza faulo mbili katika matukio ya mchezo, si kwa ugomvi.”
Balotelli alilimwa kadi nyekundu dakika ya 90, baada ya kupewa kadi ya kwanza ya njano kwa kumchezea rafu Bacary Sagna, dakika tatu baada ya Mikel Arteta kuifungia Arsenal.
“Sikuvunja kipengele cha uadilifu,” alisema Balotelli. “Tayari nimekwishaikosa timu ya taifa kwa upumbavu na siwezi kufanya hivi kwa mara ya pili.
Natumaini kuwapo katika kambi ya mazoezi Aprili. Acha tusubiri hadi mwisho wa adhabu.”
Balotelli alifungiwa mechi nne za Ligi Kuu Januari baada ya kumfanyia undava Scott Parker wa Spurs hali iliyosababisha Prandelli amteme kwenye kikosi cha Itali kilichocheza mechi ya kirafiki na Marekani Februari.
“Nitayafanyia tathmini (matukio ya Balotelli) kwenye video juu ya kadi zake kama yanakiuka kipengele cha uadilifu Balotelli,” alisema Prandelli leo, wiki mbili kabla ya kuanza kwa kambi ya Italia.
Mbali na Balotelli, kiungo Daniele De Rossi na mzaliwa wa Argentina, mshambuliaji Pablo Osvaldo pia walitoswa timu ya taifa kwa sababu ya nidhamu tangu Prandelli atambulishe kipengele cha nidhamu alipopewa timu ya taifa, mwaka 2010.
Baada ya mechi na Arsenal, kocha wa City, Mancini alisema; “ilikwisha” na Balotelli.
“Namsikitia sana, kwa sababu anapoteza kipaji chake na ubora wake,” alisema Mancini.
“Anelekea kubaya katika mustakabali wake, na anatakiwa kubadili mwenendo wake.”

No comments: