Matina Nkurlu, Dar es Salaam.
Kampuni
ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania imetangaza dhamira yake ya kuuza hisa kwa
umma itakayofuatiwa na kujiunga kwenye Soko la Hisa la
Dar es Salaam (DSE) ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya Elektroniki na
Mawasiliano ya Posta (EPOCA) na sheria ya Fedha ya mwaka 2016 ambayo inaelekeza
makampuni ya simu kumilikisha asilimia 25 ya hisa zake kwa wananchi
kwa kujiunga na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Akizungumzia hatua hiyo jijini Dar es Salaam,
Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom, Bwana Ian Ferrao alisema “Tunayo furaha
kutangaza kuwa tumeanza rasmi mchakato wa kuuza hisa kwa umma kwa mujibu wa
matakwa ya sheria na tumewasilisha maombi na utaratibu mzima utakaotumika
kuuza hisa zetu na ratiba yetu nzima kuhusiana mchakato huu kwenye Mamlaka ya
Usimamiaji wa Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Soko la
Hisa (DSE). Hatua hii ni kubwa na inadhihirisha kuwa Vodacom
ipo mstari wa mbele katika kutekeleza agizo la kuuza hisa zake kwa umma
na inadhihirisha jinsi ilivyojipanga kuendelea kuboresha na kukuza sekta
ya mawasiliano nchini Tanzania katika siku za usoni”.
Uuzaji wa hisa kwa umma na kujiunga na Soko la Hisa
kunapitia hatua mbalimbali za kupata vibali kutoka taasisi za
serikali zenye mamlaka ya kupitia maombi na kutoa vibali vya utekelezaji
wake.Ferrao aliendelea kueleza “Tunaamini uuzaji wa hisa zetu kwa umma
utazidi kukuza shughuli za Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE),kunufaisha watanzania
kiuchumi na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.Kampuni yetu haitajulikana kwa
jina la mwanzo la Vodacom Tanzania Limited bali imekuwa na jina la
Vodacom Tanzania Public Limited Company (Plc) ikiwa ni
hatua ya awali ya kujiandaa kuingia sokoni. Tunawahakikishia kuwa mchakato wa
kuingia kwenye hatua hii umeanza vizuri kwa mafanikio na tunaendelea
kuwashirikisha wadau mbalimbali kutoka serikalini kuhakikisha tunatimiza
dhamira ya kuanza kuuza hisa kwa wananchi yenye dira ya kuleta manufaa
kwa wote.”
Ferrao alitoa msisitizo kuwa Vodacom inalo jukumu kubwa
kuhakikisha hatua hii inaleta manufaa kwa pande zote zinatazohusika
kuanzia wanunuaji wa hisa, kuendelea kuwekeza , kuendelea kuleta
mapinduzi ya ubunifu wa kiteknolojia na kuimarisha ubora wa huduma za kampuni
kwa wateja wake “Tutaendelea kutoa mchango mkubwa wa ufanikishaji wa sera ya
nchi ya miaka 5 ya kukuza sekta ya mawasiliano.Tutaendelea pia kuwaletea
taarifa mbalimbali kuhusiana na mchakato wa kuuza hisa kwa umma
unavyoendelea”Alisema Ferrao.
No comments:
Post a Comment