Kiwanda cha Dangote Mtwara. |
Juma Mohamed,
Mtwara
Baada ya
kuenea kwa taarifa takribani wiki mbili sasa juu ya kusitishwa kwa uzalishaji
katika kiwanda cha Saruji cha Dangote Industries Limited mkoani Mtwara, uongozi
wa kiwanda hicho umeibuka na kusema kuwa kusitishwa huko kumetokana na tatizo
la hitilafu za kiufundi.
Akizungumza
kwa niaba ya afisa mtendaji mkuu wa kiwanda hicho Harpreet Duggal, mkuu wa
usalama wa kiwanda hicho, Benedict Kajukano alisema kiwanda kimeathirika kwa
kiasi kikubwa kutokana na tatizo hilo na kudai kuwa mafundi wanaendelea na kazi
kwa ajili ya kurejesha huduma.
Aidha,
amekiri kuwa kiwanda hicho kinatumia gharama kubwa za uzalishaji ukilinganisha
na viwanda vilivyopo maeneo mengine, hali inayosababishwa na matumizi ya
jenereta za mafuta ya Dizeli katika kuendesha kiwanda.
Hata hivyo,
mkuu huyo wa usalama hakutoa nafasi kwa waandishi wa habari kuweza kumuuliza
maswali kwa ajili ya kupata ufafanuzi zaidi kwa madai kuwa sio msemaji wa
kiwanda hicho, huku wafanya biashara Saruji na bidhaa mbalimbali wakieleza
kuathirika kwao.
Kiwanda
hicho chenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 600, kina uwezo wa kuzalisha
tani Milioni Tatu kwa mwaka na kutoa ajira za moja kwa moja kwa zaidi ya watu
1,000 wa Mtwara
No comments:
Post a Comment