'Tunakagua ubora wa Jalala' |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
Serikali
imeutaka mkoa wa Mtwara kuendesha oparesheni ya nyumba kwa nyumba kukagua vyoo
kwa kila kaya, na kwamba kaya itakayobainika kukosa choo itapigwa faini pamoja
na usimamizi mkali kuhakikisha choo kinajengwa mpaka kinakamilika.
Naibu waziri
wa ofisi ya makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Luhaga Mpina alitoa
maagizo hayo mbele ya katibu tawala wa mkoa huo Alfred Luanda na msaidizi wake
anayeshugulika na maji na mazingira Rejea Ng’ondya, baada ya kupewa taarifa ya
mazingira ya mkoa inayosema zaidi ya kaya elfu ishirini na tano hazina vyoo.
Choo cha shule ya msingi Maendeleo, manispaa ya Mtwara Mikindani. |
“Na hii
oparesheni ifanyike ‘immediately’ ya kuzipitia hizi familia kwasababu hizi
familia ambazo zinazungumzwa hazina vyoo zina wanaume wana nguvu kabisa na
wanaamka wanakula na wanaenda kutembea wanaenda kudhurula, tutakachofanya ni
oparesheni kubwa mnafika pale mnawapiga faini alafu mnawasimamia wanajenga choo
mpaka kinaisha..” alisema.
Aidha, naibu
waziri huyo imeitaka manispaa ya Mtwara Mikindani kuhakikisha wanakamilisha
mradi wa ujenzi wa Jalala la kisasa la kuchakata taka lililopo Mangamba ifikapo
mwezi Agosti mwaka huu.
Awali,
akitoa taarifa ya mazingira ya mkoa, katibu tawala msaidizi anaeshughulika na
Maji na Mazingira, Rejea Ng’ondya, alisema kaya ambazo hazina vyoo ni zaidi ya
25,000 ambazo ni sawa na asilimia 6 huku akikiri kuwa changamoto hiyo ipo kwa
kiasi kikubwa katika mikoa ya Pwani.
Naibu waziri wa Mazingira, Mhe. Luhaga Mpina akiwa katika ziara ya kukagua soko la halmashauri ya mji wa Masasi. Wapili kushoto ni mkuu wa wilaya ya Masasi Seleman Mzee. |
Naibu waziri
huyo amehitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani humo kwa kuwaongoza wananchi
wa wilaya ya Masasi na maeneo jirani katika kushiriki zoezi la usafi wa
mazingira linalofanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi nchini kote.
Naibu waziri wa Mazingira, Mhe. Luhaga Mpina akikagua samaki katika soko la halmashauri ya mji wa Masasi, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi katika wilaya ya Masasi. |
Aidha,
pamoja na kutoa pongezi kwa wananchi hao kuhamasika kwa kiasi kikubwa kufanya
usafi, amewataka viongozi wa mitaa na vijiji kuhakikisha wanasimamia vyema
sheria za mazingira na kutosita kuwachukulia hatua wachafuzi wa mazingira na
wanakwepa kufanya usafi.
No comments:
Post a Comment