Lango kuu la kuingilia ndani ya kiwanda cha Saruji cha Dangote Industries Limited, Mtwara. |
Eneo la nje ya kiwanda cha Saruji cha Dangote. |
Mazingira hayaridhishi, nje ya kiwanda cha Saruji cha Dangote. |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
Baraza la
Taifa la Udhibiti na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kanda ya kusini limekitoza
faini ya shilingi Milioni 15 kiwanda cha Saruji cha Dangote Industries Limited
cha mkoani Mtwara kutokana na uzembe wa utunzaji wa taka ngumu za viwandani.
Mratibu wa
NEMC kanda ya kusini, Lewis Nzari, amesema uongozi wa kiwanda hicho unatakiwa
kulipa faini hiyo ndani ya wiki moja, ambayo imetokana na kiwanda kuwa katika
mazingira machafu ya taka ngumu pamoja na kukosekana kwa choo nje ya kiwanda
kwa matumizi ya madereva na makondakta.
Hatua hiyo
imekuja kutokana na ziara ya waziri wa nchi ofisi ya makamu wa Rais Muungano na
Mazingira, Mhe. Luhaga Mpina, ambaye alifika kiwandani hapo huku pamoja na
mambo mengine alibaini kuwapo kwa uchafu ndani nan je ya kiwanda hicho.
“Kwahiyo
tunawapiga faini kama fundisho na kuwakumbusha ili wengine wawekezaji wengine
wasije wakafanya kosa kama hili, faini ya shilingi za Kitanzania sh. Milioni 15..”
alisema Nzari.
Ziara ya Naibu waziri wa Mazingira, Mhe. Luhaga Mpina ndani ya kiwanda cha Saruji, Dangote Industries Limited. |
Kwa upande
wake,naibu waziri alisema pamoja na faini hiyo, uongozi wa kiwanda unatakiwa
kuhakikisha ndani ya wiki mbili wanakamilisha ujenzi wa choo katika eneo la
kuegesha malori pamoja na kuhakikisha mazingira yanakua masafi wakati wote.
“Suala la
kujenga vyoo hatuwezi kuwaruhusu mwezi nzima, kwa maana ya wiki mbili lazima
vyoo view tayari vimejengwa na vinatumika, sasa hili lingine wameshatoa
maelekezo na sitaki kulirudia lakini meseji ni hiyo kwamba choo kikamilike
ndani ya siku 14 na malipo hayo ya faini yafanyike ndani ya siku saba..”
alisema.
Aidha,
ameagiza uongozi kuhakikisha wanakuwa na afisa mazingira wa kiwanda, ambaye
pamoja na majukumu mengine atasaidia kushauri mambo mbalimbali yakimazingira
kiwandani hapo.
Kabla ya
maagizo hayo, naibu waziri alitoa nafasi kwa madereva wa malori yanayobeba
Saruji hiyo, kueleza changamoto zao ambazo zilijikita katika kulalamikia kukosa
huduma ya choo.
“Kero kubwa
sisi madereva tunajisaidia kwenye mapori humo, kwahiyo mtusaidie, sasa mtu
umekosa choo utaenda wapi, hapa (Mlango wa kuingilia ndani ya kiwanda)
huruhusiwi kuingia kama hauhusiki..kwahiyo kitu kikubwa unachukua kopo lako na
maji unakwenda maporini..” alisema Khamis Juma.
Mkuu wa
idara ya utumishi na utawala wa kiwanda hicho, Kajiri James, alijaribu kuomba
radhi kutokana na faini hiyo lakini hakuweza kukubaliwa, hivyo kuridhia kulipa
kutokana na maagizo yaliyotolewa.
“Ni jambo
ambalo linasikitisha kwamba katikati ya juhudu zote ambazo tunazifanya tunajikuta
tunawekewa hiyo adhabu..labda pia kwa heshima tu niombe adhabu isitishwe ili
tupatiwe muda na kupata fedha zaidi na kuweza kuendelea kumalizia shughuli
ambazo tumepewa.” Aliomba Kajiri.
Alisema
kilichotokea ni bahati mbaya ambayo haikutarajiwa huku akitaja kwamba walikuwa
wakikabiliwa na baadhi ya changamoto ikiwa ni pamoja na kucheleweshewa vibali vya
kuruhusu ujenzi.
No comments:
Post a Comment