Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akiwa amekaa katika dawati ikiwa ni katika moja ya ziara zake za kukagua zoezi la uchongaji wa samani hizo. |
Juma Mohamed, Mtwara
Ikiwa leo
ndio mwisho wa utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Magufuli juu ya kumaliza changamoto ya uhaba wa madawati nchini kwa
shule za msingi na sekondari, mkoa wa Mtwara umefikia na kupitisha lengo kwa
asilimia 2.
Akitoa
taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo, mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego,
alisema awali mkoa ulikuwa na hitaji la madawati 28,890 ambapo mpaka kufikia
leo jumla ya madawati 29,333 yametengenezwa na kufanya kumaliza tatizo kwa
asilimia 100.
“Kwahiyo
tumetimiza lengo kwa asilimia 100 na tuna madawati yaliyobaki ziada 443..kwa
upande wa shule za msingi tuna ziada ya madawati 215 na upande wa sekondari tuna
ziada ya madawati 228..ninaamini ndani ya wiki mbili zijazo ziada itaongezeka
kwasababu yapo madawati mengine tunaendelea kupokea kutoka kwa wadau
mbalimbali.” Alisema Dendego mbele ya waandishi wa habari.
Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego akiwa katika moja ya ziara zake za kukagua madawati. Kushoto ni mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara, Zacharia Nachoa. |
Aidha, aliwataka
wakuu wa shule na walimu wakuu kuhakikisha wanayatunza vizuri madawati hayo na
kuongeza kuwa hatokuwa na huruma kwa yeyote ambaye atabainika kuwa na ufujaji
wa samani hizo.
“Lakini
niwaagize pia wakuu wa shule kuhakikisha madawati haya wanayatunza, wakati
tunaanza zoezi hilo mkoa ulikuwa una upungufu wa madawati Zaidi ya elfu 50
lakini pia tuliangalia upungufu mwingine ulitokana tu dawati limetoka mbao moja
au mbili kwahiyo na wenyewe wawe na tabia ya kurekebisha pale yanapoharibika kuliko
kuacha yaharibike kabisa..” aliongeza.
Mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego. |
Kwa upande
wao, wanafunzi, walimu na wazazi mkoani humo wamepongeza jitihada za serikali
ya mkoa kwa kushirikiana na wadau wake mbalimbali kwa kukamilisha suala hilo
ambalo wanaamini litasaidia kuhamasisha wanafunzi kupenda shule pamoja na kukua
kwa taaluma.
Adam
Mtavangu, ambaye ni mwalimu katika shule ya sekondari ya Shangani, licha ya
kuipongeza serikali ya mkoa na wadau wake kwa kufanikisha zoezi hilo, anawataka
wananchi kutokuwa na tabia ya kuiachia serikali pekee katika masuala ya
kimaendeleo kama hayo.
Mwalimu katika shule ya sekondari ya Shangani manispaa ya Mtwara Mikindani, Adam Mtavangu. |
“Suala la
utengenezaji wa madawati lisiachiwe tu kuwa suala la serikali, tatizo hili
lilikuwa dogo hapo mwanzo lakini liliachwa hadi kufikia kuwa kubwa kiasi kwamba
likaleta mtazamo kwamba litazamwe kitaifa zaidi..” anasema.
Agizo la
kutatua uhaba wa madawati nchini kwa shule za msingi na sekondari lilitolewa na
Rais Magufuli mwezi machi mwaka huu.
No comments:
Post a Comment