Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akielekea ndani ya ghala la TANECU kwa ajili ya kukagua pembejeo za ruzuku za zao la korosho. Kulia ni mkuu wa wilaya ya Tandahimba, Emmanuel Luhahula. |
Na Juma Mohamed, Tandahimba.
Baadhi ya
viongozi wa vyama vya msingi katika mikoa ya Lindi na Mtwara wamelalamikia
uchelewaji wa pembejeo za ruzuku za zao la korosho, zinazosambazwa na Mfuko wa
Kuendeleza Zao la Korosho (WAKFU), na kulazimika kutumia muda mwingi wakiwa
maghalani kusubiri mzigo.
Wakizungumza
mbele ya mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, katika ghala kuu la Chama
Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba, Newala Cooperative Union (TANECU), walisema
hali hiyo inapelekea kuwapo kwa mvutano kati ya wakulima na viongozi wa vyama.
“Pembejeo
kutoka mwezi wa sita haziendani na kilimo cha korosho, kwasababu sasa hivi
korosho zimeshachipuza na watu wanatarajia..kwahiyo tunakuwa tunasutana, mimi
wananisuta wakulima na mimi nawasuta watu wa pembejeo..sasa mkuu wa mkoa
tunakuomba hili ulizingatie na usome nyakati..” alisema Awadhi Mbeweka,
mwenyekiti wa AMCOS ya Masasi.
Wakulima wa korosho na viongozi wa AMCOS |
Naye,
Abdallah Matandika ambaye ni kiongozi wa chama cha msingi cha Chibula wilayani
Ruangwa mkoani Lindi, alisema katika wilaya hiyo ni vyama vinne pekee kati ya
vyama 21 ambavyo vimepata pembejeo.
Mbunge wa
jimbo la Tandahimba, Katan Ahmaed, alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi
ya wakulima wakilalamikia changamoto hiyo, ambapo amewashauri kuwasilisha
malalamiko yao ofisi ya mkuu wa mkoa kabla ya kwenda ngazi za juu zaidi, kwani
mkuu wa mkoa anauwezo wa kutatua kwa haraka changamoto zao.
“Miongoni
mwa malalamiko makubwa ilikuwa ni watu wa Liwale pamoja na Nachingwea, lakini
nilipata shida baada ya ku ‘crosscheck’ baina ya watu wale na watu wa mfuko
maelezo kidogo yalikuwa tofauti..wapo watu walitoa taarifa za mbali sana, na
hili lazima nitoe tahadhari kwa watu kwamba tuna mkuu wa mkoa kama mmeona mmempa
taarifa leo na amekuja kwa haraka, lakini kuna watu wanakawaida ya kuruka
hatua..” alisema Katan.
Kaimu katibu
mtendaji wa WAKFU Ramadhan Mmari, alisema bado mfuko unafanya jitihada za dhati
kuhakikisha pembejeo hizo zinafika kwa wakulima kwa wakati, ambapo jumla ya
tani elfu 10 tayari zimegawanywa katika mkoa wa Mtwara ambazo ni sawa na
asilimia 70 huku mkoa wa Lindi zimegawiwa kwa asilimia 56 na Ruvua asilimia 38.
Kwa upande
wake, mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego, amewataka watendaji wa ugawaji wa pembejeo
hizo kufanya kazi usiku na mchana, ili kuondoa usumbufu wa kupanga foleni kwa
viongozi hao wakati wa kusubiri kupatiwa pembejeo.
“Lakini
kubwa mhe. Mwenyekiti mimi niwaombe watendaji, waache kufanya kazi kwa mazoea,
wanapoona kuna tatizo wafanye kazi usiku na mchana saa 24 baadala ya kufanya
kazi mpaka saa 10 baadae wanaenda kulala haya magari tusingeyakuta kama
ingekuwa wanakesha hapa..” alisema.
Kwa mujibu
wa WAKFU, ni kwamba mpaka kufikia June 26 mwaka huu mzigo wote uliobaki wa tani
65,000 wa pembejeo hizo utakuwa tayari
umeshawasili kwa ajili ya kuugawa kwa wakulima.
No comments:
Post a Comment