Tuesday, June 21, 2016

Wananchi Tandahimba waungana na madiwani na Mbunge wao kuzindua ujenzi kituo cha afya.

Mbunge wa Tandahimba, Katan Ahmed, akishirikiana na wananchi na madiwani wake wa halmashauri ya wilaya ya Tandahimba katika zoezi la uchimbaji wa msingi katika eneo la ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Nanyanga.



'Tupo kazini'



Na Juma Mohamed, Tandahimba.
Wananchi wa kata ya Nanyanga, halmashauri ya wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara wameamua kuungana na madiwani pamoja na mbunge wao katika shughuli ya uzinduzi wa ujenzi wa kituo cha afya katika kata hiyo kutokana na kuchoshwa na adha wanazozipata juu ya huduma za afya.
Wakizungumza katika eneo la ujenzi huo, walisema suala la kina mama wajawazito kujifungulia njiani na kurundikana wodini katika Zahanati iliyopo ni la kawaida, hivyo kutoa msukumo kwa wakazi wa katani hapo kuona umuhimu wa kuwa na kituo cha afya ambacho kitawasaidia kupata huduma za upasuaji.

Makazi wa kata ya Nanyanga, Tandahimba, akishiriki zoezi la uchimbaji wa msingi katika eneo la ujenzi wa kituo cha afya cha kata hiyo

“Nimehamasika hivi kwasababu kipindi cha nyuma kabla ya kituo hiki (kipindi hiki) tulikuwa na Zahanati ndani ya kata yetu, sasa kulikuwa na huduma duni pale hasa panapokuwa na wagonjwa tunawabeba kwa baisikeli kuwapeleka Mahuta, Namikupa au Tandahimba umbali wake ni kilometa Saba..” alisema Ahmad Mpita, mkazi wa Nanyanga.
Madiwani wa halmashauri hiyo walioshiriki zoezi la uchimbaji wa msingi katika kituo hicho, wamesema hatua ya upatikanaji wa eneo hilo imetokana na mchango wa wananchi hao ambao walichangia sh. 5 kwa kila kilo moja ya korosho na kufanikiwa kupata zaidi ya sh. Milioni 17.
“Tumeshirikiana kwa pamoja kuja kuzindua huu mradi wa kata ya Nanyanga kwa ajili ya kuchimba msingi hapa na mambo mengine, kwasababu ni miaka mingi miaka 54 ya uhuru watu wa Nanyanga walikua wanapata tabu ya kwenda Tandahimba kwa ajili ya kupata tiba, kwa mantiki hii ndio tumekuja hapa ili kuangalia wanakuwa na maisha angalau mazuri na huduma stahiki karibu.” Alisema Ashura Mbope, diwani wa kata ya Mchichila.
Kwa upande wake, mbunge wa Tandahimba, Katan Ahmad, amesema ujenzi wa kituo hicho ni moja ya jitihada za kuunga mkono sera za serikali ya awamu ya tano inayotaka kuwapo kwa kituo cha afua katika kila kata na Zahanati kila kijiji.
Alisema, kituo hicho kikikamilika itakuwa ni mara ya kwanza kwa kata iliyopo ndani ya halmashauri ya wilaya ya Tandahimba kupata kituo cha afya ambacho ujenzi wake umetokana na nguvu za wananchi wenyewe.

Mhe. Mbunge akiwa kazini.

“Kwahiyo suala la afya ya mama na mtoto baada ya miaka mitatu au minne kwa Tandahimba itakuwa ni historia kwasababu sio hapa tu, tunadhamiria kata zetu zote kuona zinakuwa na vituo vya afya..” alisema Katani.
Makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Bakari Makuyeka, alionesha kufurahishwa na jitihada hizo na kusema serikali itawaunga mkono.
Matarajio ya madiwani na wakazi wa taka hiyo ni kuona ujenzi huo ukikamilika baada ya mwaka mmoja, ili kuwaondolea kero ya kusafiri umbali mrefu wananchi hasa akina mama wajawazito kufuata matibabu.

No comments: