Wednesday, September 16, 2015

Coastal Union waambulia kichapo kingine Mtwara, wachezaji wawashambulia waandishi wa habari.


Wachezaji wa Ndanda Sc wakishangilia baada ya kufunga bao katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union ya Tanga, uliochezwa katika jana katika uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara. Ndanda walishinda goli 1-0.


Nahodha wa Coastal Union, Hamad Juma na mshambuliaji wa Ndanda Sc, Omar Mponda, wakiwania mpira.




Ubao wa matokeo (Score Body) ulio ndani ya uwanja wa Nangwanda Sijaona kama unavyoonekana baada ya Ndanda kufunga goli.


Mashabiki wa Ndanda Sc wakishangilia baada ya mchezo kumalizika na timu yao kuweza kuchomoza na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Coastal Union.





Na Juma Mohamed, Mtwara.
Timu ya soka ya Coastal Union ya Tanga imeendelea kuwa na mwanzo mbaya katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, baada ya leo kupoteza tena mchezo wake wa pili dhidi ya Ndanda Sc ya mkoani Mtwara kwa kukubali kichapo cha goli 1-0 lililofungwa kwa shuti kali na mshambuliaji Atupele Green katika dakika ya 71 ya mchezo.

Goal Kipa wa Coastal Union, Sebwato Nicholas, akiruka kudaka mpira uliokuwa ukielekea langoni mwake.

 Hata hivyo baada ya kumalizika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Erly Sasii kutoka Dar es Salaa, kocha wa Coastal Union, Mganda, Jackson Mayanja alikataa kuzungumza chochote mbele ya waandishi wa habari na kusababisha kuzuka vurugu baina ya wachezaji wa timu hiyo na waandishi wa habari.
Mwandishi wa Clouds Tv, Fatuma Maumba, alijikuta katika wakati mgumu baada ya kumwagiwa maji na baadhi ya wachezaji wa Coastal Union, wakati akijaribu kumfuata kocha huyo kwa ajili ya kufanya naye mahojiano.

Mwandishi wa habari wa Clouds Tv mkoani Mtwara, Fatuma Maumba, akielezea juu ya vurugu zilizotokea kati ya wachezaji wa Coastal Union na waandishi wa habari, baada ya kocha wa Coatsal Jackson Mayanja kukataa kuongea na waandishi baada ya mchezo kumalizika


Maumba alisema, baada ya kocha kukataa kuzungumza na waandishi wachezaji wake wakaanza kutoa lugha za matusi huku wengine wakimwaga maji kwa waandishi, ambao hata hivyo walipata msaada kutoka kwa askari wa jeshi la polisi.
“Wachezaji wake wakaja juu wakaanza kutoa matusi wengine wakiwa wanatumwagia maji huku wakitishia kutupiga..lakini kwenye wengi hakiharibiki kitu kwasababu polisi walikuwepo na kuanza kuwazuia baadhi ya waandshi na wachezaji..wale walitaka kunipiga labda kwasababu ni mwanamke kitu ambacho mimi nisingeweza kukubali..” alisema.

Baadhi ya waandishi na askari polisi wakijaribu kutuliza vurugu zilizotokea uwanjani baada ya kocha wa Coastal Union, Jackson Mayanja, kukataa kuongea na waandishi na wachezaji wake kuanza kuwashambulia waandishi


Akizungumzia usalama wa vifaa vyake, alisema alikuwa akihofia kamera ambayo alikuwa akiitumia kwa muda huo lakini kwa bahati nzuri haikuweza kuathirika, na hata maji hayakuweza kuifikia kutokana na kuwa na mfuniko. (cover)
Kwa upande wake, kocha wa timu ya Ndanda Sc, Amim Mawazo, amesema amefurahishwa na matokeo ambayo yameonyesha kuwa timu yake ni nzuri zaidi ya wapinzani wake, huku akijipanga kwa ajili ya kucheza michezo ya ugenini.
“Sasa mechi za nje tutacheza kama mechi za nje, unajua kuna namna ya kuweza kucheza kati mechi za nyumbani na za ugenini..tactic (mbinu) lazima uzibadilishe.” Alisema.
Akimzungumzia mshambuliaji wake mpya aliyesajiliwa kutoka klabu ya Kagera Sugar, Atupele Green, alisema, ni msahmbuliaji nzuri ambaye anajua majukumu yake anapokuwa uwanjani na anatumia vizuri nafasi anazozipata huku akimuita ni ‘Opportunist’.
Aidha, Atupele Green, amesema lengo lake ni kuchukua kiatu cha dhahabu msimu huu, hivyo anazidi kumuomba mungu na kuongeza juhudi katika uchezaji ili afikie lengo hilo, ambalo alishindwa kulifikia msimu uliopita akiwa na Kagera Sugar kwa kufunga magoli sita.
“Kiukweli nimejipanga niweze kuchukua kiatu cha dhahabu ndio maana nikasema kwamba kila mechi nitakayocheza namuomba mwenyezi mungu kwamba nifunge goli angalau hata moja, na hicho kitu nimekianza kwasababu mechi ya kwanza nimefunga goli moja na leo nimefunga moja..” alisema.
Na kuoongeza “kikubwa ni kuifanya timu yangu iwe katika nafasi nzuri kwenye ligi hii ya 2015/2016 namshukuru sana mwenyezi mungu..” aliongeza.

No comments: