Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Madimba, halmashauri ya wilaya ya Mtwara wakiwa darasani huku wakikalia mbao zilizo juu ya matofali kutokana na uhaba wa madawati. |
Juma Mohamed, Mtwra.
WANAFUNZI wa
shule ya sekondari ya kutwa ya Madimba halmashauri ya wilaya ya Mtwara, wako
hatarini kusomea chini ya miti kutokana na shule yao kukabiliwa na uhaba wa
vyumba vya madarasa hali inayopelekea wasomee kwenye vyumba vya Maabara ambavyo
bado havijakamilika.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti shuleni hapo, walisema kwa sasa wanalazikia kutumia vyumba
vya Maabara ambavyo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika muda mfupi ujao jambo
ambalo litawafanya wakose mahala pakusomea.
“Hii hapa ni
Maabara sasa ikiisha sisi tutasomea chini ya Mikorosho, na chini ya mikorosho
kuna jua sasa tutasomea wapi wakati chini ya mikorosho kuna jua?..mvua nayo
itachangia, inamaana kwa kifupi hatuna sehemu ya kusomea endapo hii maabara
itaisha..tunaiomba itujengee madarasa ya kutosha na itujengee bweni kwa ajili
wengine tunatoka mbali..” alisema Kamilu Chilolo na kuongeza;
“Kipindi
kama hiki wanyama wakali wabaya, watu wanaweza wakawabaka wasichana..tunaomba
watujengee bweni ambalo litatusaidia sisi kusoma kwa urahisi na kufaulu
mitihani yetu..” aliongeza.
Naye, Amina
Mohamed, aliiomba serikali kuwajengea madarasa pamoja na kuongeza juhudi katika
ujenzi wa maabara ili waweze kusoma vizuri masomo ya sayansi ambayo yanahitaji
vitendo zaidi ili kuwajengea uwelewa.
Mkuu wa
shule hiyo, Ahmad Kwerendu, alisema licha ya uhaba wa vyumba vya madarasa,
changamoto nyingine wanazokabiliana nazo ni ukosefu wa ofisi za walimu pamoja
na nyumba za walimu ambapo ipo moja ya mkuu wa shule ambayo hata hivyo
analazimika kukaa na baadhi ya walimu wengine.
Mkuu wa mkoa
wa Mtwara, Halima Dendego, alimwagiza mwenyekiti wa kijiji cha Madimba, Mohamed
Madiva, kuwahamisha wananchi wake kushiriki katika zoezi la kufyatua matofali
yatakayosaidia kutatua changamoto za miundombinu shuleni hapo ikiwa ni pamoja
na ujenzi wa nyumba za walimu.
Dendego alifanya
ziara ya kikazi shuleni hapo kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo pamoja na
kusikiliza kero na kupokea maoni ya walimu katika shule hiyo ambayo huu ni
mwaka wa tatu toka kuanzishwa kwake.
Ikumbukwe kuwa kata ya Madimba ndiko ambako kuna mradi mkubwa wa kiwanda cha kuchakata gesi asilia ambao tayari umeshaanza uzalishaji ukizinduliwa na Rais wa awamu ya Nne Mhe. Jakaya Kikwete mwezi Oktoba mwaka jana.
No comments:
Post a Comment