Wagonjwa katika kituo cha afya cha kata ya Kitere halmashauri ya wilaya ya Mtwara wakisubiri kupata huduma za matibabu kutoka kwa daktari. |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
UHABA wa
watumishi, dawa pamoja na ukosefu wa maji ni miongoni mwa changamoto zilizopo
katika kituo cha afya cha kata ya Kitere halmashauri ya wilaya ya Mtwara, kiasi
cha kusababisha kushindwa kutoa huduma za upasuaji.
Wakizungumza
kituoni hapo, wananchi wa kata hiyo walisema bado hawajajua kwanini kituo hicho
hakina maji wakati tayari kuna kisima, huku wengine wakidai kuwa wanapata adha
ya usafiri wakati wa kwenda kujifungua mjini Mtwara kutokana na miundombinu
mibovu ya barabara.
“Sisi bwana
tuna tatizo la maji, maji kama ingekuwa wakati wake hakika kukupa unywe
utashindwa jinsi ya kufanya..leo hii mwanamke anaweza kuzaa hapa akapata
mashaka maji aende akachote Mmambi ili apate huduma ya maji, sisi tunashida ya
maji..kwanza kuna maji yanayosukumwa kutoka Lilido hayatakiwi mashine..”
alisema Mohamed Kalias, mkazi wa Kitere.
Amina Mohamed,
alisema suala la kukosa huduma za upasuaji kituoni hapo kunahatarisha uhai wa
kina mama na watoto kutokana na umbali uliopo kutoka Kitere mpaka hospitali ya
rufaa ya Ligula iliyopo mjini Mtwara na miundombinu duni ya usafiri.
Mganga mkuu
wa kituo hicho, Dkt. Dickson Hokololo alimweleza changamoto hizo mkuu wa mkoa
wa Mtwara, Halima Dendego, ambaye amefika kituoni hapo kukagua utendaji kazi na
kusikiliza changamoto zilizopo ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika halmashauri
hiyo.
“Tuna uhaba
wa dawa, vifaa tiba na upungufu wa watumishi..changamoto nyingine ni tatizo la
upatikanaji wa maji hasa baada ya msimu wa masika kumalizika na huduma ya gari
la wagonjwa kutokuwa na uhakika..” alisema.
Hata hivyo
mkuu wa mkoa alitoa siku 20 kwa uongozi wa kituo hicho kuhakikisha kinaanza
kutoa huduma hizo na kuwaondolea usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kina mama
wajawazito kufuata huduma za upasuaji mjini Mtwara.
Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego akiwa katika ziara ya kikazi katika kituo cha afya cha Kitere, halmashauri ya wilaya ya Mtwara kwa ajili ya kukagua utendaji |
“Tukashirikiane
wote kuhakikisha madaktari wanakuja, hatuwezi kusamehewa kwa hili DMO (Mganga
mkuu wa wilaya) mimi sidhani kama ningelala usingizi mnajua kabisa Kitere kituo
kizuri kama hiki alafu mnakaa tu mnaongeaa hamlet madaktari kwanini msihame
nyie mkahamia huku..mimi matarajio yangu nitakapoondoka hapa zisizidi siku 20
hiki kituo kiwe kimeanza kufanya kazi..” alisema.
Kituo cha
afya cha Kitere ni tegemeo kwa wananchi wote wa kata hiyo na vijiji jirani
ambapo chumba cha upasuaji kimekalika na kina vifaa vyote vinavyohitajika
isipokuwa huduma zinashindikana kutolewa kutokana na kukosa wataalamu.
No comments:
Post a Comment