Mkuu wa wilaya ya Tandahimba, Emmanuel Luhahula. |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
VIONGOZI 37
wa vyama vya msingi 26 vilivyo chini ya Chama Kikuu cha Ushirika cha
Tandahimba, Newala Cooperation Union (TANECU), wamekamatwa na polisi kwa amri
ya mkuu wa wilaya ya Tandahimba, Emmanuel Luhahula kutokana na kushindwa
kuwalipa wakulima wa kororsho malipo yao ya tatu.
Akizungumza na Juma News, mkuu huyo wa wilaya alisema, aliamua kutoa amri hiyo kwa kamanda wa
polisi wa wilaya ya Tandahimba, kufuatia viongozi hao kushindwa kulipa deni
hilo ambalo ni sh. Bilioni 1.2 kama fedha za malipo ya ziada kwa wakulima.
Awali deni
hilo lilikuwa ni zaidi ya sh. Bilioni 1.4 ambapo vyama ambavyo vilikuwa
vinadaiwa vilikuwa 49 kabla ya vyama 11 kulipa na kubakia vyama 38 ambavyo
vimeshindwa kutekeleza agizo ambalo lilitolewa tangu Aprili 7 mwaka huu na
kuwataka walipe ndani ya siku 7.
“Siku saba
zilipoisha vyama 11 vilikubali kulipa, nikawapa muda mpaka tarehe Tisa mwezi
watano kwa maana ya mwezi mzima ikawa ni vile vyama 11 tu ambavyo vimelipa na
tumebakiza deni la Bilioni 1.2..kwahiyo jana (Mei 9) niliamua kuwakamata wote,
nilimtumia OCD (Kamanda wa Polisi wa Wilaya) na kamati yangu ya ulinzi na
usalama..” alisema.
Baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi vya wilaya za Tandahimba na Newala, vilivyo chini ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba, Newala Cooperation Union (TANECU). |
Alisema,
kabla ya kukamatwa kwao, alipata taarifa kuwa viongozi hao wanafanya kikao
katika eneo la Maghalani wilayani humo ndipo alipomuagiza katibu tawala wa
wilaya na mkurugenzi wa halmashauri waandae magari kwa ajili ya kuwasafirisha
kuwapeleka mahakamani wilayani Newala.
Alisema, ili
kuhakikisha madeni hayo yanalipwa bila kujali kuwa wahusika watakuwa kizuizini,
ameagiza kwa watendaji wa vijiji kuhakikisha wanafuatilia dhamana zao ambazo
wote wameweka saini kuwa iwapo watashindwa kulipa fedha hizo ziuzwe mali zao
kwa ajili ya kulipa.
“Nilichofanya,
wajumbe wa bodi wote wako tisa kwa kila chama, wameshaandika dhamana zao ‘commitment
letter’ za kuonesha kuyatambua madeni yao, kila ‘Body Member’ kwa nafasi yake
amekiri kwamba hili deni nalitambua na hili deni nitalilipa kwa kuweka
dhamana..ameweka aidha nyumba au shamba..” aliongeza.
Alisema yupo
tayari kutoa ushirikiano kwa mahakama pale itakapohitajika juu ya uthibitisho
wa watuhumiwa hao, na kwamba hategemei kuona mahakama ikianza kuzungusha kesi
hiyo kwa kudai ushahidi wakati tayari vielelezo vipo.
No comments:
Post a Comment