Na Juma Mohamed, Mtwara.
WAKULIMA wa
zao la korosho nchini wametahadharishwa juu ya uwepo wa ugonjwa wa Mnyauko
ambao unatajwa kuwa ni hatari zaidi katika kuuwa Mikorosho kwa kipindi kifupi
mara baada ya kupata maambukizi.
Hadhari hiyo
imetolewa na mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Mfaume Juma,
wakati wa utambulisho wa ugonjwa huo kwa waandishi wa habari ambao kwa kutumia
vyombo vyao wakulima watapata fursa ya kuufahamu ugonjwa na kujua dalili zake.
Kutokana na
ugonjwa huo kuenezwa na vimelea aina ya Uyoga vinavyojulikana kama Fusarium
oxysporum vinavyojificha katika udongo wa Mikorosho iliyoathirika, mkurugenzi
huyo aliwataka wakulima kusafisha majembe yao baada ya kuyatumia pamoja na kutopanda
miche kutoka katika mashamba mengine.
“Kwahiyo
udongo wa eneo lililoathirika usihamishwe kwenda katika sehemu nyingine, na
ndio maana nikasema kama mtu analima katika eneo ambalo limeathirika atoke na
jembe ambalo ni safi, asije kuhamisha udongo wa sehemu moja kwenda sehemu
nyingine ugonjwa utaenea eneo hadi eneo kwasababu ugonjwa upo ndani ya
udongo..” alisema.
Alisema
jitihada zinafanyika baina ya bodi kwa kushirikiana na wataalamu wa magonjwa ya
Mikorosho kutoka katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele mkoani hapa kwa
ajili ya kupata viwatilifu vya kuutokomeza na kuikinga Mikorosho.
Kwa upande
wake, mtafiti mstaafu kutoka katika taasisi ya Naliendele, Dk. Shamte Shomari,
alizitaja baadhi ya dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na mjani katika baadhi
ya matawi ya mkorosho kupoteza rangi yake ya kawaida ya kijani na kubadilika
kuwa njano na baadae kuwa kahawia.
Aliitaja
dalili nyingine kuwa ni mkorosho ulioathirika ukitazamwa toka mbali unaonekana kama
kuwa na mchanganyiko wa majani ya kijani, njano na kahawia pamoja na sehemu ya
kati ya mizizi ya Mikorosho iliyoshambuliwa kuwa na rangi ya kahawia.
Mtafiti mstaafu wa Taasisi ya Utafiti ya Naliendele, Mtwara, Dkt. Shamte Shomari, akiulezea ugonjwa wa Mnyausho uliolikumba zao la korosho. |
Aidha,
alibainisha athari zinazotokana na vimelea hivyo kuwa ni pamoja na kuziba
mirija inayopitisha maji na virutubisho toka ardhini kwenda katika majani na
kuziba mirija inayopitisha chakula toka kwenye majani na kusambazwa katika
sehemu mbalimbali za mkorosho kiasi cha kupelekea mkorosho kufa.
Alisema,
mkorosho baada ya kupatwa na ugonjwa huo na kushindwa kupatiwa tiba ya haraka,
utadumu kwa kipindi cha miezi mitatu na baada ya hapo unakufa.
Ugonjwa huo
ulifahamika rasmi kwa mara ya kwanza mwaka 2012 katika kijiji cha Magawa wilaya
ya Mkuranga mkoani Pwani, kabla ya mwaka 2014 kuonekana katika kata za Nanganga
na Nangoo wilaya ya Masasi mkoani hapa na kijiji cha Mnongodi halmashauri ya
wilaya ya Mtwara, huku ikisemekana kuwa upo katika baadhi ya maeneo katika mkoa
wa Ruvuma.
No comments:
Post a Comment