Ratiba ya uchaguzi |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
KAMATI ya
uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA), imeahidi
kutenda haki na kufuata kanuni na sheria zilizopo katika katiba ya chama hicho
na vyama vingine vya juu, ili mchakato wa uchaguzi ulioanza juzi umalizike
salama.
Akizungumza
na waandishi wa habari juzi katika ofisi za Mtwarefa, mwenyekiti wa kamati
hiyo, Hussein Kingi, alisema kamati itahakikisha inafuata yale yaliyoelekezwa
kwenye katiba na kanuni za uchaguzi na kwamba kitendeo cha kukiuka hayo ni
kukaribisha malalamiko kutoka kwa wagombea yatakayopelekea watu kukata rufaa na
kuweka mapingamizi.
“Kwahiyo
tunawathibitishia ndugu zetu, hatutakenda nje ya kanuni na katiba ya Mtwarefa na
TFF, CECAFA mpaka CAF na FIFA..sisi katiba na kanuni kama hazifanyi kazi za
wilaya zinafanya kazi za mkoa, kama za mkoa hazifanyi kazi zinafanya kazi za
CECAFA, kama za CECAFA hazifanyi kazi zinafanya kazi za CAF na kama za CAF
hazifanyi kazi zinafanya kazi za FIFA..” alisema Kingi.
Alisema,
tangazo la uchaguzi huo utakaofanyika Mei 29 mwaka huu limesambazwa katika
halmashauri zote za mkoa wa Mtwara na kwamba kila mwanamichezo aliye na vigezo
anawajibu wa kugombea nafasi anayohitaji.
“Kila
mgombea anaetaka fomu katika ngazi ya Mtwarefa basi anatakiwa kujaza fomu
ambaye ataipata kwa katibu wa Mtwarefa aliyeanza kuzitoa kuanzia leo (Juzi)
lakini humo ndani kuna mtiririko ambao mjazaji anatakiwa awe na picha mbili
(Passport size) ambazo moja itabandikwa kwenye fomu ile lakini vilevile anatakiwa
ajaze kwa maandishi yake mwenyewe..” alisema.
Naye, mjumbe
wa kamati hiyo Selemani Kachele, akizungumza kwa niaba ya katibu wa kamati,
Baraka Kagema, alizitaja nafasi zinazogombewa kuwa ni nafasi ya mwenyekiti na
makamu wake, katibu na makamu wake, mweka hazina, mwakilishi wa mkutano mkuu wa
TFF na mwakilishi wa vilabu katika mkutano mkuu wa TFF.
Alisema,
nafasi hizo ada yake ya kuchukulia fomu ni sh. 300,000 huku akitaja nafasi
nyingine Tatu za wajumbe wa kamati ya utendaji ambazo ada yake ni sh. 200,000.
“Sifa za
wagombea, kwanza awe raia wa Tanzania, awe na kiwango cha elimu kisichopungua
kidato cha Nne na cheti cha elimu ya sekondari, awe za uzoefu wa mpira wa miguu
uliothibitishwa wa angalau miaka Mitatu, asiwe na hatia ya kosa la jinai la
kuhukumiwa kifungo bila ya uchaguzi wa faini..” alisema.
Aliongeza
kwa kutaja vigezo vingine kuwa ni pamoja na mgombea awe na umri unaoanzia miaka
21 na kuendelea, awe amewahi kuwa mchezaji wa mpira wa miguu, kocha, mwamuzi au
kushiriki katika uendeshaji wa mpira wa miguu.
Aidha, zoezi
la uchukuaji na kurudisha fomu za uchaguzi huo limeanza juzi Aprili 21 na
litafikia mwisho Aprili 24 mwaka huu saa 10:00 jioni.
No comments:
Post a Comment