Mwanasheria wa kampuni ya Unique Consultant Company Ltd (UCC), Robert Makwaia, akijibu hoja za wananchi |
Wajumbe wa kikao cha ujirani mwema |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
KAMPUNI ya
Unique Consultant Company Limited (UCC) inayofanya kazi ya kuajiri watu katika
kiwanda cha Saruji cha Dangote Industry Limited mkoani hapa imelalamikiwa na
wananchi kutoa ajira kwa ubaguzi na kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya
rushwa.
Wakizungumza
katika kikako cha ujirani mwema kilichoitishwa na mkuu wa wilaya ya Mtwara,
Fatma Ally, ambaye aliwaita viongozi wa kiwanda hicho kwa ajili ya kujibu hoja
za wananchi, walisema vijana wengi wanaoishi katika vijiji jirani na kiwanda
hicho wananyimwa fursa za kuajiriwa kwa kigezo cha kutojua lugha ya kiingereza.
Kigezo cha
kutojua lugha hiyo ambacho ni miongoni mwa sababu zilizoelezwa na mwanasheria
wa UCC, Robert Makwaia, kilipingwa vikali na wananchi hao na kudai kuwa wapo
Wachina ambao wameajiriwa huku wakiwa hawajui kiingereza wala Kiswahili.
“Nasema
kwamba pale ajira zinatolewa kama sio kwa upendeleo basi kwa kutumia rushwa,
kwasababu vigezo vilivyoelewa na mwanasheria wa UCC kwamba mtu anashindwa
kuajiriwa eti kwasababu anakosa vigezo fulani ikiwemo kutojua lugha, sisi
tumeshuhudia Wachina Mhe. Mkuu wa wilaya wamekuja pale gari wanajifunzia kwenye
hii ‘High Way’ (Barabara kuu) mimi nakaa Mbuo pale..”alisema John Ngaeje, kaimu
mtendaji wa kijiji cha Mbuo.
Alisema
wataalamu wengi katika vitengo mbalimbali kiwandani hapo ikiwa ni pamoja na
wahandisi, ni raia wa Kichina ambao awali walikuwa wanajua lugha ya Kichina
pekee, wamejifunza lugha za kiingereza na Kiswahili wakiwa kazini jambo ambalo
linaweza kufanyika pia kwa wakazi wa maeneo hayo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Naumbu Kusini, Rashid Abdelleman akichangia mada. |
Rashid
Abdelleman, ambaye ni mwenyekiti wa kijiji cha Naumbu Kusini, alisema kampuni
hiyo haifai tena kuwepo kiwandani hapo kwasababu ya kutotenda haki huku akidai
kuwa matangazo ya ajira kwa wakazi wa Mtwara yatolewa muda mfupi kabla ya siku
ya kuanza usaili huku maeneo mengine ya nje ya Mtwara yanatolewa mapema.
“Kwahiyo
kampuni hii haifai kabisa na kama watakuwa wanang’ang’ania kuna mapungufu
fulani, tunaweza kwenda kiwandani ugonvi wetu ukaishie pale, waitwe wafanyakazi
wote tujue kampuni ile ina wafanyakazi wangapi sasa hivi, wafanyakazi hao kulingana
na idadi yao, Naumbu Kusini wangapi mimi watu wangu wote nawajua kama
mwenyekiti, wa Mgao wapo wangapi..kwahiyo watu wengi wanaofanya kazi pale
hawatokei kwetu..” alisema.
Ally Ahmad,
alisema wakati anakaimu nafasi ya mtendaji wa kata, aliwahi kufuatwa na watu
kutoka Dar es Salaam ambao walitaka kumkabidhi bahasha yenye pesa ndani kwa
ajili ya kutaka awathibitishe kuwa ni wakazi wa kijiji cha Hiyari, ili waweze
kupata ajira kirahisi kiwandani hapo huku wakidai kuwa wameagizwa na watu wa
UCC na afisa muajiri wa kiwanda (H/R).
Meneja rasilimali watu na utawala wa kampuni ya Saruji ya Dangote Industry Ltd Mtwara, Gervacy Chapalwa, akifafanua jambo. |
“Hilo suala
la kuonekana hawachukui rushwa, mimi nimelishuhudia mwenyewe nakabidhiwa
bahasha ya pesa na nikaikataa nikasema ndugu zangu hawajapata ajira,
ninakukabidhije wewe barua ya kukuthibitisha kwamba wewe ni mzawa wa hapa
wakati hauna kitambulisho chochote cha kuonesha wewe unatoka wapi, unaishi
sehemu gani na unautaratibu gani..” alisema Ahmad.
Akijibu hoja
hizo, Mwanasheria huyo alisema suala la kigezo cha lugha ni sehemu tu ya vigezo
vinavyohitajika na kwamba vipo vingine vingi vinavyohitajika ambapo hata hivyo
hakuweka wazi vigezo gani vingine vinavyohitajika.
“Tunapokuwa
tunafanya ‘interview’ jamani, sio kwamba ile barua inavyokuja mtu unajua kwamba
huyu anatoka kijiji fulani hapana, inakua tu imekaa pale barua unaiangalia na
CV yake wewe unaendelea na ‘procedure’ zingine..kwahiyo tukisema tuchague kwa
kijiji kwamba tumchukue fulani na tumuache fulani hapana hatutaweza kufka
hivyo..” alisema Makwaia.
Kuhusu
tuhuma za rushwa, alisema hazina ukweli na kwamba mtoa hoja inawezekana ametunga
tu katika kikao hicho kwasababu alikuwa na uwezo wa kwenda kuthibitisha katika
ofisi za UCC kwakuwa alikua na bahasha yenye pesa hizo.
“Alitakiwa
hata kuja ofisini kuja kujihakikishia kabisa kwamba je huyo mtu alidhamiria
hapa na huyo mlengwa ni huyu hapa UCC?..kwahiyo anachokisema naweza kusema
kwamba ni porojo tu, kaka ofisini tu yeye mwenyewe au katunga tu hapa..”
alisema.
Mkuu wa
wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa miongoni
mwa wananchi juu ya kuwapo kwa vitendo vya rushwa kiwandani hapo na kudai kuwa
vitendo hivyo vipo pia katika ngazi za vijiji, kata mpaka tarafa ambapo
aliahidi katika kiako kijacho cha tarafa atamwalika kamanda wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mtwara kwa ajili ya kutoa
elimu ya kuripoti vitendo vya rushwa.
Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally. |
“Ninaamini
timu yangu ya TAKUKURU itahamia huku Chapalwa (Menejea rasilimali watu), kwasababu
hizi tuhuma za rushwa sisi kama serikali hatuwezi kuziacha hivihivi lazima
tutazifanyia kazi..lakini taarifa ambayo nimeipokea ni kwamba rushwa haipo
kiwandani tu, mpaka kwa watendaji, nimepokea kwa maandishi mjumbe mmoja mwema
ameniandikia..” alisema mkuu wa wilaya.
No comments:
Post a Comment