Fatma Ally, akiongea na wananchi |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
WANANCHI wa
vijiji mbalimbali halmashauri ya wilaya ya Mtwara wamehamasika na kuunga mkono
jitihada zinazofanywa na mkuu wa wilaya ya Mtwara Fatma Ally, za kutatua changamoto
ya ukosefu wa madawati katika shule za msingi na sekondari.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti katika ziara iliyofanywa na mkuu wa wilaya huyo kwa ajili
ya kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli na mipango
mbalimbali ya kimaendeleo, walisema awali suala hilo lilipokelewa tofauti kwa
kujua ni jukumu la viongozi wa ngazi za juu pekee.
“Agizo baada
ya kupokelewa, tulisema ameagizwa mkuu wa wilaya, ameagizwa mkuu wa mkoa
hatukujua kwamba tumeagizwa mpaka sisi sasa leo umetuzindua tuko macho, nasema
kwamba miti ipo na watu wakufanya kazi wapo mimi mwenyewe ninao mti mmoja na
ninautoa sasa hivi..taratibu sasa ya jinsi gani tunafanya ndio tulikuwa
hatujajua..” alisema Sadiki Sadiki, mkazi wa kata ya Mpapura.
Alitoa wito
kwa viongozi wa vijiji kuwafikishia kwa wakati wananchi wao taarifa za
kimaendeleo zinapowafikia sambamba na kuwapatia elimu pale inapobidi kufanya
hivyo ili wapate fursa ya kushiriki katika mambo muhimu yanayohitaji nguvu ya
pamoja.
Naye, Yusufu
Chikunyembe, mkazi wa kijiji cha Mpapura ambaye alikuwa anawakilisha vijana,
alisema ataitumia elimu aliyoipata kupitia kikao hicho cha mkuu wa wilaya kwa
ajili ya kwenda kuwahamasisha vijana wenzake katika kuunga mkono na kushiriki
katika utatuzi wa mahitaji hayo.
Alitoa mti
mmoja ambao upo katika shamba lake kwa ajili ya kupasuliwa mbao zitakazotumika
kutengenezea madawati huku akiiomba serikali ya kijiji kuwaandaa watu kwa ajili
ya kwenda kufanya kazi hiyo.
Moses
Mnunduma, ambaye ni mwenyekiti wa kijiji cha Mayanga, aliahidi kwenda kuwahamasisha
wanakijiji wake kuanza harakati za kuchangia madawati huku akilalamikia vitendo
vya viongozi wa kata kuchelewa kuwasilisha taarifa kwa wananchi wao.
Aidha, mkuu
wa wilaya ambaye kupitia mfuko wake wa kuhamasisha wananchi kuchangia madawati
kwa hiyari aliyouita ‘Haba na haba hujaza kibaba’ ambao mpaka sasa amekusanya
sh. Milioni 14, aliagiza ziundwe kamati za watu 10 katika kata Tatu ambazo
alizitembelea juzi na kuzipa jukumu la uhamasishaji wa suala hilo.
Alisema,
kamati hizo zitakuwa na wajumbe watakaowakilisha makundi mbalimbali ikiwa ni
pamoja na wazee maarufu wa kijiji, vijana maarufu pamoja na viongozi wao wa
vijiji ambapo aliahidi kurudi tena baada ya siku 10 kwa ajili ya kupata
mrejesho wa utekelezaji wa maagizo yake.
Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akiongea na wananchi wa tarafa ya Mpapura, halmashauri ya wilaya ya Mtwara, juu ya masuala mbalimbali ya kimaendeleo. |
“Muhamasishe
vijana wenzenu maarufu kwa ajili ya wale wazee wetu ambao wametupa heshima ya
kutupa mbao mshirikiane nao mkacharange hiyo miti ili tupate hizo mbao
zipelekwe kwenye eneo ambalo tumeliandaa..mgambo wa tarafa wapewe kazi ya
kulinda zile mbao, mafundi waanze kazi baada ya siku 10 nitakuja na mkuu wa
mkoa atakuja kuwakagua kazi inaendeleaje..” alisema mkuu wa wilaya.
No comments:
Post a Comment