Fatma Ally |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
HALMASHAURI
ya wilaya ya Mtwara pamoja na manispaa ya Mtwara Mikindani zimepitisha mpango
wa matumizi ya ardhi utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka 20, ambapo
yametengwa maeneo maalumu kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya
maendeleo.
Akizungumza
baada ya kumalizika kwa kikao cha kupitisha mpango huo, kaimu mkurugenzi wa
Manispaa ya Mtwara Mikindani, Rashidi Mtima, alisema mpango huo ndio utakuwa
nguzo ya kisheria katika matumizi ya ardhi katika halmashauri hizo huku
ukilenga kuhakikisha kuwa Mtwara inahudumia shughuli za gesi.
Alisema,
mpango huo umetenga maeneo matano kutoka katika halmashauri hizo kwa ajili ya
ujenzi wa miradi ya maendeleo na kwamba miongoni mwa hayo ni pamoja na eneo la
Ziwani litakalokuwa maalumu kwa ajili ya kuhudumia masuala ya gesi na mafuta.
“Tumezungumza
pale kwamba vision ya Mtwara iwe mji bora katika kanda hii ya bahari ya Hindi,
mji bora na kama tunavyojua tunatarajia vilevile Mtwara tutoe huduma za
gesi..sehemu ya kudumu ya visima vya gesi kule baharini iwe ni Mtwara, kwahiyo
master plan imelenga hilo ndio maana ikaweka eneo lile la Ziwani kuwa kama
logistic park..” alisema.
Mkurugenzi
wa halmashauri ya
wilaya ya Mtwara, Zacharia Nachoa, alisema katika uendelezaji
wa mpango huo, kila halmashauri itakuwa na wajibu wa kuona yale yaliopo katika
mpango yanatekelezwa, jambo ambalo litasaidia kuondoa ujenzi holela.
“Mwenzako
hawezi kujenga kiwanda hapa na wewe unaweka hospitali pale, lazima pawe na
namna moja ya upangaji wa matumizi ya ardhi ambayo yanaelekeza kwamba vitu
fulani vitafanyika hapa, mambo ya utalii yatafanyika hapa, afya na nini
yatakuwa huku..” alisema.
Mkuu wa
wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, aliwahamasisha wananchi kuutambua na kuupokea
mradi huo ambao anaamini utawanufaisha kupitia ardhi zao iwapo watazitunza
vizuri na kuacha kuwauzia watu kwa ghara za chini ambazo hazitakuwa na tija
kwao.
Fatma Ally |
Alisema kama
wananchi hawna elimu ya kutosha juu ya mpango huo, ni vyema wakawauliza
madiwani wao ambao wanauwezo wa kuwaelimisha zaidi huku wakijua kuwa ardhi zao
ni thamani kubwa.
“Kwahiyo
nawahamasisha wananchi watunze ardhi yao na wasidanganyike wala wasihadaike,
kwasababu sasa hivi kuna madalali wengi wanakuja kununua ardhi ili wao wakaiuze
kwa wahusika kama wawekezaji..na wale wanunuzi pia nawaambia wasije wakanunua
ardhi kienyeji, kwasababu wanaweza kununua ardhi kumbe ni eneo ambalo
limetengwa kwa makaburi..” alisema.
Maeneo
mengine yaliyotengwa kupitia mpango huo ni eneo la Naumbu lililotengwa kwa
ajili ya Viwanda, Mjimwema ambako huko ni kwa ajili ya elimu ya juu, Nanguruwe
kumetengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo na makazi pamoja na eneo la Mtwara
mjini lililotengwa kwa ajili ya shughuli za kibiashara.
No comments:
Post a Comment