Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akimkabidhi cheti mhitimu wa mafunzo ya mradi wa elimu na demokrasia. |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
SERIKALI
mkoani hapa imesema elimu ya ziada inahitajika kutolewa kwa viongozi katika
ngazi za kata, vijiji na vitongoji ili kuwawezesha kutambua majukumu yao na
mipaka ya kazi zao.
Hayo
yamezungumzwa na mkuu wa wilaya ya Mtwara Fatma Ally, wakati wa maafali ya
wahitimu wa mafunzo ya mradi wa Elimu na Demokrasia, yaliyoendeshwa na kituo
cha demokrasia Tanzania kwa ufadhili wa serikali ya Norway, ambapo alisema viongozi
wengi wa ngazi za chini hawajui majukumu yao na kujikuta wanaingilia kazi za
wenzao.
“Unakuta
wakati mwingine kiongozi anakuwa hajui mipaka yake, anaweza kuwa ni Diwani
akaenda kuingilia kazi za mkaguzi mkuu wa mahesabu ngazi ya kata, anaweza kuwa
ni mwenyekiti wa kijiji akaenda kufanya kazi ya polisi..lakini yote hii ni
kwasababu viongozi wale hawajui majukumu yao..” alisema.
Fatma Ally |
Alisema,
kazi za viongozi hao zinahitaji zaidi maelekezo kwasababu ni tofauti na kazi za
kuajiriwa ambazo mtu anafanyiwa usaili baada ya kuomba nafasi anayohitaji
akijua wazi kuwa ana ujuzi wa kutosha kwa kile alichokiomba.
Alisema, pamoja na serikali ya wilaya yake
kuwa imejipanga kutoa elimu kwa viongozi wa siasa katika ngazi hizo, bado kuna
haja ya kupata msaada kutoka katika kituo hicho kwa ajili ya kutoa elimu hiyo
ambayo itakuwa ni msaada mkubwa kwa madiwani, watendaji kata, vijiji na wenye
viti wa vijiji.
Mratibu wa
mradi huo ambao unatekelezwa katika halmashauri za wilaya ya Mtwara na ya mji
wa Nanyamba ulioanza mwaka 2011, Lucy Agostino, alisema mradi huo unasimamiwa
na makatibu wa wilaya kutoka katika vyama vinne vya siasa ambavyo ni Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha
Mapinduzi (CCM) na UDP.
Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akimkabidhi cheti mhitimu wa mafunzo ya mradi wa elimu na demokrasia. |
Alisema,
wahitimu hao 23 waliofanyiwa mahafali ni wahitimu wa awamu ya pili katika mradi
huo ambao walianza kupata elimu hiyo mwaka 2012 baada ya wahitimu wa kwanza
walioanza kupata elimu mwaka 2011 na kuhitimu mwaka 2014.
“Hawa
wawezeshaji tulikuwa tunawapa mafunzo kuhusiana na dhana za demokrasia na
utawala bora, mifumo ya serikali inavyofanya kazi nikimaanisha uongozi na
uwakilishi katika ngazi za serikali za mitaa na hapa tulikuwa tunalenga
kitongoji, kijiji, kata na bunge na pia walikuwa wanapata mafunzo kuhuisu dhana
za jinsia.” Alisema.
Alisema,
wawezeshaji hao walikwenda vijijini na kuanzisha vikundi kwa ajili ya kuendesha
majadiliano kutokana na yale waliyofundishwa, ambapo yalionekana kuwa na
manufaa kwa wanavikundi na wawezeshaji wenyewe ambao baadhi yao waliweza kupata
nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali baada ya uchaguzi wa serikali za
mitaa wa mwaka 2014.
Haji
Machemba, ambaye ni mhitimu na mwezeshaji kutoka kata ya Nanyamba, alisema miongoni
mwa faida alizozipata kupitia mafunzo hayo ni kuwa mwenyekiti wa serikali ya
mtaa kupitia cha cha CUF pamoja na kikundi chake kutoa wajumbe saba katika
serikali ya mtaa.
“Katika
wajumbe hao, akina mama ni watatu na wanume wane..pia katika kikundi changu kumetokea
mwanamama ambaye alijituma akajiingiza katika siasa na hivi ninavyozungumza ni
diwani wa viti maalumu, kwahiyo ni mafanikio ambayo yametokea katika masomo
haya..” alisema.
No comments:
Post a Comment