Saturday, February 27, 2016

Wananchi watahadharishwa kujikinga na mafuriko.


Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kasim Majaliwa (wapili kulia) akiwa katika ziara ya kikazi katika bandari ya Mtwara jana.




Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kasim Majaliwa (katikati) akiimba kwa pamoja na walimu wa mkoa wa Mtwara (hawapo pichani) alipokwenda katika ukumbi wa Chuo cha Walimu Tanzania (TTC) mkoa wa Mtwara kwa ajili ya kuzungumza na walimu. Wakwanza kulia ni mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego na wakwanza kulia ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mtwara, Mohamed Sinani.




Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kasim Majaliwa (kushoto) akimwelekeza jambo meneja wa bandari ya Mtwara, Prosper Kimaro (Kushoto) alipofanya ziara ya kikazi bandarini hapo




Na Juma Mohamed, Mtwara.

SERIKALI imezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa wananchi wote wanaishi katika maeneo salama katika kipindi hiki cha mvua ili kuwahepusha na kukumbwa na maafa pindi zinaponyesha mvua kubwa zinazosababisha mafuriko.
Agizo hilo lilitolewa jana mkoani hapa na waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kasim Majaliwa alikuwa akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mashujaa, na kusema kuwa kwamujibu wa taarifa za watabiri wa hali ya hewa ni kwamba bado mvua zitakuwa nyingi na kubwa zaidi katika kipindi cha mwezi Machi mwaka huu.
Alisema, wananchi wanatakiwa kujiandaa sasa hivi na kutopuuza taarifa hizo ambapo baadae madhara yake ni makubwa hasa kwa wale ambao wanaishi katika maeneo hatarishi.

Wananchi wa manispaa ya Mtwara na maeneo jirani waliohudhuria mkutano wa hadhara wa waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, katika uwanja wa Mashujaa, wenye lengo la kutoa pole na salamu za serikali kwa waathirika wa mafuriko.


“Wale wote mliopo kwenye maeneo hatarishi anzeni kutafuta maeneo salama ya kuishi, halmashauri zote nchini zihakikishe kwamba wananchi wanaishi kwenye maeneo salama ambayo hayafikiwi na maji na hasa kwa mvua ambazo zinakuja, tukishafanya hilo tutakuwa tumehepusha vifo na matatizo mengine ambayo yanaweza kujitokeza na kuwakwaza wananchi wa kawaida..” alisema.

Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kasim Majaliwa akizungumza na wananachi wa Mtwara katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika uwanja wa Mashujaa, wenye lengo la kutoa pole kwa waathirka wa mafuriko.


Alisema serikali imehuzunishwa na maafa ya mafuriko yaliyojitokeza katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwa ni pamoja na Mtwara ambako takriban kaya 1277 zipata madhara ya huku heka 5200 za mashamba zikiharibiwa na mafuriko hayo.
Alisema serikali inawapa pole wote waliokumbwa na maafa hayo huku ikijitahidi kutoa misaada kwa waathirika kwa kadri inavyowezekana ili kupunguza ugumu wa maisha uliosababishwa na janga hilo.
Awali mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akitoa taarifa ya maafa hayo alisema mbali na kaya na mashamba hayo yaliyoharibiwa na mafuriko, kulitokea vifo vya watu Tisa ambavyo vilisababishwa na Radi kali ambazo zilipiga wakati wa mvua huku kukiwa na upotevu wa mali zenye thamani ya sh. Bilioni 1.8.

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akiwasilisha taarifa ya maafa yaliyowakumba wananchi wa mkoa wake, kwa waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.


Aidha, waziri mkuu alijikuta akilalamikiwa na wananchi wa mkoani hapa waliohudhuria mkutano huo wakimtaka kufika katika hospitali ya rufaa ya mkoa ya Ligula, ambako wanalalamikia kuwa na huduma mbovu na wengine wakidai kuwa kuna upungufu wa vifaa tiba ikiwa pamoja na mashine ya X Ray.
Kwa kutii kile kilicholalamikiwa na wananchi hao, aliwajibu kupitia mkutano huo kuwa amewasikia na atafanya jitihada za kufika hospitalini hapo ili kama kuna majipu yanahitaji kutumbuliwa basi afanye hivyo kwa masilahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Wabunge wa mkoa wa Mtwara wakiwa katika ukumbi wa Chuo cha Walimu Tanzania (TTC) mkoa wa Mtwara  ambako Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kasim Majaliwa alikuwa akizungumza na walimu wa mkoa wa Mtwara.


Baada ya kumaliza hotuba hiyo, alifanya ziara katika maeneo kadhaa mjini hapa ikiwa ni pamoja na kwenda kuongea na watendaji wa serikali katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Mtwara (TTC) ambako aliongea na walimu na kuwaeleza mipango mbalimbali ya serikali kwa ajili ya kuboresha masilahi yao.

Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kasim Majaliwa (kushoto) akimwelekeza jambo meneja wa bandari ya Mtwara, Prosper Kimaro (Kushoto) alipofanya ziara ya kikazi bandarini hapo


Baada ya hapo alifika katika bandari ya Mtwara ambako alifanya ziara fupi ya kuangalia utendaji kazi na kisha kukutana na meneja wa bandari ambaye alimsomea taarifa ya bandari ambaye aliipokea na kuonesha kuikubali na kisha kumwambia kuwa bandari yake iko salama.

Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), James Mataragio (wakwanza kulia) akimwelekeza jambo Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kasim Majaliwa (Wapili kushoto) alipofanya ziara katika kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo Madimba, Mtwara.


Alimaliza ziara yake kwa kutembelea kiwanda cha kuchata gesi asilia kilichopo Madimba Halmashauri ya wilaya ya Mtwara, na kupokelewa na mkurugenzi mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), James Mataragio, aliyemweleza faida ambazo Taifa inazipata kutokana na uwepo wa rasilimali za mafuta na gesi kuwa ni pamoja na kuokoa fedha za kigeni na kuongeza pato la halmashauri (Service Lave)



No comments: