Add caption |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
WAZIRI mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, amemsimamisha kazi kwa
muda usiojulikana daktari mmoja wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mtwara,
Ligula, Dkt. Fortunatus Namahala, kufuatia kuwa na tuhuma za kupokea rushwa
kutoka kwa mgonjwa.
Hatua hiyo
imekuja baada ya waziri mkuu kufanya ziara ya kushtukiza hospitalini hapo jana
asubuhi kwa ajili ya kukagua utendaji na miundombinu ya hospitali hiyo ambapo
alianza kwa kwenda katika kitengo cha mapokezi ya wagonjwa kabla ya kwenda
kusikiliza malalamiko ya wananchi waliokuwa wamekusanyika hospitalini hapo
baada ya kupata taarifa za uwepo wake.
Baadhi ya wananchi
waliopata nafasi ya kuwasilisha malalamiko yao kwa waziri walieleza mapungufu
yaliyopo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maji, vipimo na dawa ambapo wanadai kuwa
wanaelekezwa kwenda katika hospitali binafsi ambako huko watapata huduma zote
zinazokosekana katika hospitali hiyo.
Tatu
Abdallah, ambaye malalamiko yake kwa kiasi kikubwa ndio yamepelekea
kusimamishwa kazi kwa daktari huyo, alisema alifika hospitalini hapo Februari 1
mwaka huu akiwa na mzazi wake wakiume ambaye ndio alikuwa mgonjwa kwa ajili ya
kupatiwa matibabu ambapo alipatiwa vipimo na kuamriwa apelekwe Thieta.
Alisema
daktari aliyempokea mgonjwa wake alimwagiza akanunue dawa zenye thamani ya sh.
85, 000 katika maduka yaliyopo jirani na hospitali ambapo alifanya hivyo
aliporudi kwa daktari akaagizwa tena kwenda kununua uzi wenye thamani ya sh.
25,000 katika duka binafsi la Chambila.
“Nikaenda
kwa Chambila nikanunua uzi wa 25,000 nikamletea, nikamuuliza vimetimia akasema
ndio ila mimi kama mimi ninataka hela 100,000 ili nimfanyie ‘Operation’ baba
yako, nikamwambia hakuna shida nitakupa lakini ilimradi baba yangu niokoe uhai
wake..” alisema.
Aliendelea
kumweleza waziri mkuu kuwa pamoja na kukamilisha mahitaji yote aliyoagizwa na
daktari na kukubali kutoa hizo sh. 100,000 lakini upasuaji haukufanyika mpaka
kufikia Februari 7 alikuwa bado hajafanyiwa chochote huku akiamriwa tu kumpa
chakula na kujibiwa majibu ya mkato kuwa daktari huyo hajiskii kumfanyia
upasuaji mgonjwa.
Baada ya
kuona hakuna dalili za kutibiwa hazipo, alichukua uamuzi wa kumpeleka katika
hospitali binafsi ya Sajora akiwa amekabidhiwa boksi la dawa ambazo hata hivyo
zilikataliwa na waliompokea kwa madai daktari wa hospitali hiyo anayehusika na
upasuaji hawezi kuzikubali.
“Wakanipa
namba ya dkt. Kaisi wa hapo Sajora, nikampigia nikamweleza akaniambia ngoja
kwanza nije alipokuja nikamweleza akasema mimi ninaweza kumsaidia baba yako
lakini kwa hali hii ninaweza kumuua kwasababu amechoka na siku zote Nane
alizokaa Ligula hajakula, kanunue chakula umpe mzee, mimi kesho nitamfanyia
upasuaji lakini ninahitaji 360,000..mimi nikageuka nikamwangalia baba nikasema
kweli masikini tunakufa wakati siku bado..” alisema.
Alisema,
baada ya baba kumsikia daktari akitoa agizo hilo la fedha, alimwambia mwanaye
aende kijijini kwao, Kiromba ili auze shamba apate fedha hizo za kumkabidhi
daktari ili amtibu mgonjwa.
“Na kweli
mimi nikachukua pikipiki pale nikaenda siku hiyohiyo nikafanikiwa kupata sh.
500,000 nikarudi inaama shamba lake la heka 5 sasa hivi zimebaki heka Mbili na
Nusu, nikafika pale Sajora akafanyiwa ‘Operation’ tukalipa tukarudi nyumbani..”
aliongeza.
Waziri mkuu
aliwajibu wananchi kuwa ameyapokea malalamiko yao na hata wale ambao walikosa
nafasi ya kueleza aliwaambia kuwa anajua kiu yao na kuendelea na ziara yake
katika wodi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wodi ya wazazi ambako huko alikutana
na changamoto ya wazazi kutumia nguo zao kutandika katika vitanda huku shuka
zikiwa zimefungiwa.
Alitembelea
pia wodi ya upasuaji ambako waandishi hawakuruhusiwa kuingia lakini hakuchelewa
na baadala ya hapo aliamua kwenda katika ukumbi wa hospitali hiyo kwa ajili ya
kuongea na watumishi wa hospitali hiyo.
Katika kikao
hicho ambacho kilihudhuriwa na baadhi ya watumishi pamoja na maofisa wa
hospitali hiyo, waziri mkuu aliamsimamisha mlalamikaji Tatu Abdallah, na
kumtaka aende kumshika mkono daktari ambaye alimwomba rushwa ya sh. 100,000
ambaye awali alisema hamfahamu kwa jina lakini kwa sura anamjua.
Aliinuka na
kwenda kumshika mkono na kumuinua daktari huyo ambaye alikaa nyuma kabisa ya
ndani ya ukumbi huo na kuamriwa asogee mbele karibu na meza kuu na kisha
kutamkiwa rasmi na waziri mkuu kuwa anasimamishwa kazi mara moja mpaka
uchunguzi ukamilike na kumuamuru atoke nje ya ukumbi.
“Sasa naanza
na wewe, utasimama kazi na uchunguzi unafanywa juu ya hilo..na wengine wote
ambao nitawabaini utaratibu ni huo hatuwezi kwenda na hali hiyo kwa wananchi wa
kawaida lakini hatuwezi kusita kwa ‘professional’ zenu..kama ulionywa
utabadilika na hubadiliki nitajua na kama ulikua hufanyi usifanye, nataka
mabadiliko kwanzia leo..” alisema waziri mkuu.
Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa,akiongea na watumishi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mtwara, Ligula baada ya kumaliza ziara ya kikazi hospialini hapo. |
Alimwagiza kamanda
wa polisi mkoa wa Mtwara, Henry Mwaibambe, kuhakikisha mama huyo analindwa
vizuri kwa kuhofia anaweza kuwindwa na kufanyiwa vitendo viovu.
Aidha,
alimtaka katibu tawala wa mkoa wa Mtwara, Alfred Luanda kwa kushirikiana na
maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya
uchunguzi juu ya tuhuma zinazomkabili daktari huyo katika kipindi ambacho
amesimamishwa kazi.
“RPC huyu
mama alindwe asije akafuatwa jioni nyumbni, huu ni utaratibu wa kawaida wa ukweli
na uwazi..mumemwambia akanunue dawa sawa, 100,000 ya nini? Alafu mumemwacha
kumuhudumia, akalazimika kwenda kuuza shamba na kumpeleka Sajora, yani ameamua
kutoiamini Ligula na kwenda kwenye Private Hospital..haileti picha.” Alisema.
Aidha,
alisema kupitia kikao hicho ambacho alidhani kuwa kingekuwa cha kusikiliza
changamoto kutoka kwa madaktari na kujua namna gani serikali imejipanga kuweza
kuzitatua na kuboresha masilahi yao lakini imekuwa tofauti na baadala yake
hakuweza kusikiliza hoja zao hizo kutokana na kuchukizwa na namna ambavyo
wananchi wanapata shida katika kupata huduma.
Alimwagiza
katibu tawala kuhakikisha kuwa maduka yote ya watu binafsi yaliyopo katika
maeneo ya jirani na hospitali hiyo yafungwe mara moja na baadala yake kuwe na
duka ndani ya hospitali na kitengo cha kutoa huduma za Mfuko wa Taifa wa Biama
ya Afya (NHIF)
Kabla ya
kufikia mwisho wa kikao hicho, baadhi ya madktari walisimama na kuomba kutoa
malalamiko yao, ambapo walilalamikia namna wanavyopata shida ya kutekelezewa
mahitaji yao na wakuu wao wengine wakielekeza lawama zao katika ofisi ya katibu
tawala.
“Mimi
nilifikia hatua ya kuandika barua kwa katibu mkuu wa wizara ya afya, nikampa
nakala katibu mkuu wa Tamisemi, katibu mkuu wa ofisi ya waziri mkuu, nakala
waziri wa afya na waziri wa Tamisemi..lakini nilivyorudi hapa nikaitwa na Ras
na wakuu wa Idara nikapata vitisho..na hata kama nikifa basi katibu tawala na
watu wake wawe ‘responsible’, kwasababu ubadhirifu wa majengo umekisiri hapa
hospitali haiwezekani hospitali ya mkoa tuwe na Oxygen Mashine moja..” alisema
Dkt. Hindi Mastai kutoka kitengo cha wagonjwa wanje (OPD) anaeshughulikia Bima.
Aliitaka
serikali kuwawajibisha wahusika wanaosimamia huduma za afya mkoani hapa na
kusema lawama zinaelekezwa kwao kwa makosa kwani wanaopaswa kuanza
kushughulikiwa ni hao, huku akitaja mapungufu mengine hospitalini hapo kuwa ni
pamoja na ukosefu na uchafu katika choo cha wodi ya wazazi ambayo ilifanyiwa
usafi baada ya kupata taarifa za ujio wa waziri mkuu.
No comments:
Post a Comment