Na Juma Mohamed, Mtwara.
KUTOKANA na
matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme, Tanzania inaokoa matumizi ya fedha za
kigeni dola Bilioni 1 kwa mwaka ambazo zilikuwa zikitumika kununulia mafuta
mazito kwa ajili ya kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme.
Hayo yemeelezwa
na mkurugenzi mtendaji wa Shrika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), James
Mataragio, wakati akitoa taarifa ya utendaji ya shirika hilo kwa waziri mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, alipotembelea katika
kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo Madimba mkoani hapa.
Alisema,
uzinduzi wa miundombinu hiyo ambao ulifanywa mwezi Oktoba mwaka jana na Rais wa
awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, umekuwa ni suluhisho la upatikanaji
wa nisahti ya umeme hapa nchini kwani asilimia 60 ya umeme unaozalishwa
unatokana na gesi asilia.
“Kwa sasa
tunazalisha wastani wa futi za ujazo milioni 45-50 kwa siku hapa Madimba..hata
hivyo uwezo wetu ni kuzalisha futi za ujazo milioni 130 kwa siku kutoka katika
visima Vitano vya gesi asilia vilivyopo eneo la Mnazi Bay.” Alisema Mataragio
na kuongeza:
“Ujio wa
mradi huu umetoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 170 ambapo kati ya hizo 100 ni
za wazawa toka mikoa ya Lindi na Mtwara, aidha kampuni zote zinazohusika katika
kutoa huduma ni za Kitanzania zenye matawi/ofisi hapa Mtwara..” aliongeza.
Alisema,
mradi mwingine mkubwa unaotekelezwa na TPDC kwa sasa ni ule wa kujenga mtambo
wa kusindika gesi asilia nchi kavu kwa ajili ya matumizi ya ndani na
kusafirisha nje ya nchi (LNG).
Alisema,
mradi huo unajengwa katika eneo la Likong’o mkoani Lindi na kwamba baada ya
kupatikana kwa ardhi, TPDC, wawekezaji na Serikali kupitia wizara ya Nishati na
Madini wanaendelea na hatua mbalimbali zitakazowezesha kufanikisha mradi kwa
lengo la kukamilisha ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi kwa ajili ya soko la
nje na sehemu ya gesi nyingine kutumika nchini.
“Hii itafungua
fursa mbalimbali za kiuchumi kwa Tanzania na hasa kwa wakazi wa Mtwara na
Lindi..wawekezaji katika mradi huu wa aina yake hapa nchini unakadiriwa kutumia
takribani dola za Marekani bilioni 30-40 ambapo umelenga kuendeleza gesi asilia
iliyogundulika katika kina kirefu cha bahari (47.O8 TCF)..alisema.
Waziri mkuu
ambaye alizunguka sehemu mbalimbali za kiwanda hicho kujionea namna ambavyo
shughuli za uzalishaji zinavyofanyika, aliwapongeza viongozi wa TPDC na
wafanyakazi wa kiwanda hicho na kusema kuwa serikali inatambua mchango wao
katika maendeleo ya Taifa katika sekta ya hiyo huku juhudi zao zikionekana.
“Jitihada za
kuzalisha umeme kupitia gesi ni kubwa sana ambazo mnazifanya na tuna matumaini
makubwa..haya yote ambayo tunayangumza kwenye majukwaa ya kuwahakikishia
Watanzania kwamba watapata umeme eneo kubwa ambalo tunalizungumzia ni hili la
gesi ambayo tunayo na imeshaanza kwenda Kinyerezi na niseme tu kwamba wananchi
hawa sasa wanafarijika..” alisema.
No comments:
Post a Comment