Friday, February 26, 2016

Ndanda walipa kisasi kwa Ruvu Nangwanda, Mtwara.

 

Wachezaji wa Ndanda Fc na JKT Ruvu wakipeana mikono tayari kwa kuanza mchezo.





Mlinzi Paul Ngalema wa Ndanda, akiangalia kwa kupeleka pasi 




Paul Ngalema akijipumzisha baada ya kumaliza mchezo


Mashabiki wa Ndanda wakishangilia nje ya uwanja baada ya mchezo kumalizika



Na Juma Mohamed, Mtwara.
KWA mara nyingine tena katika michuano ya kombe la shirikisho nchini Tanzania ikijulikana kama Azam Sports Federation Cup (FA), timu ya soka ya Ndanda Fc ya mkoani hapa imeendeleza ubabe dhidi ya wapinzani wao katika michuano hiyo baada yah ii leo kuibugiza JKT Ruvu ya Pwani kwa magoli 3-0 katika uwanja wa Nangwanda Sijaona.
Ndanda ambao mchezo wao wa kwanza katika michuano hiyo ambayo bingwa wake atawakilisha Taifa katika Kombe la Shirikisho barani Afrika, waliichapa Mshikamano kwa jumla yamagoli 5-0 leo hii wamelipa kisasi cha kuchapwa magoli 3-1 na Ruvu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliochezwa katika uwanja huo katika mzunguko wakwanza.

Wachezaji wa Ndanda Fc wakishangilia goli la Pili lililofungwa na Paul Ngalema.


Mchezo huo ulionekana kupooza katika dakika za mwanzoni kwa timu zote kucheza kwa tahadhari kubwa kuhofia kuruhusu goli la mapema na kufanikiwa kumaliza dakika 20 za mwazo zikiwa hazijafungana.
Kadri muda ulivozidi kwenda mchezo ulionekana kuchangamka huku Ndanda wakipanga mashambulizi zaidi langoni mwa Ruvu ambapo katika dakika ya 27 mchezaji Omari Mponda alifanikiwa kuipatia goli la kuongoza Ndanda baada ya kutumia vyema mpira wa kona iliyopigwa na Paul Ngalema na kushindwa kuokolewa na walinzi wa Ruvu.
Zikiwa zimesalia dakika 4 kabla ya timu hizo kwenda mapumziko, mlinzi wa pembeni upande wa kushoto wa Ndanda Fc, Paul Ngalema ambaye leo alionekana kuwa na madhara zaidi kufuatia krosi zake alizokua akizielekeza langoni mwa Ruvu, aliipatia timu yake bao la pili kwa kuachia shuti lililomshinda mlinda mlango wa Ruvu Shaban Dihile, hivyo hadi timu zinakwenda mapumziko ni Ndanda ambao walikuwa mbele kwa magoli hayo mawili.

Wachezaji wa Ndanda wakishangilia goli la Tatu lililofungwa na Atupele Green.

Ruvu wanaonolewa na Kibaden Mputa, walirudi kipindi cha pili wakiwa na dhamira ya kutaka kurejesha magoli hayo lakini waliduwaa baada ya Atupele Green kutumia dakika Tatu tu baada ya kuanza kipindi cha pili kuweza kuandika goli la Tatu kwa kuachia shuti kali kwa guu la kushoto na kuitimisha karamu hiyo ya magoli katika mchezo huo.
Ndanda waliwabadilisha Omega Seme, Omary Mponda na Kasian Ponera alaiyeumia na nafasi zao kuzibwa na Jackson Mkwera, Salum Minelly na Masoud Ally huku Ruvu wakimbadilisha George Minja aliyeumia na kumuingiza Cecil Efrem.
Kadi ya njano ilitoka moja katika mchezo huo ikielekezwa kwa mlinzi wa Ndanda, Salvatory Ntebe baada ya kujibizana na mwamuzi.
Mchezaji Saady Kipanga wa Ruvu alikiri kuwa walicheza vibaya na kutoa mwanya kwa wapinzani wao kuweza kutumia makosa yao na kupata magoli huku akiwasihi mashabiki wao kutokata tama kutokana na mwenendo wao mbaya katika ligi unaopelekea kushika mkia.
Kocha wa Ruvu, Kibaden Mputa hakusita kukiri kuzidiwa na wapinzani wake na kudai kuwa safu yake ya ulinzi haikucheza vizuri kiasi cha kuruhusu idadi hiyo ya magoli ambapo wakati wanaelekea katika mchezo hawakutegemea kutokana na kuwa na kumbukumbu ya kuwafunga awali.
Naye kocha msaidizi wa Ndanda, Mussa Mbaya, aliendelea kutamba na kukisifu kikosi chake kucheza kwa uelewano nzuri na kuahidi kuzidi kuwafurahisha mashabiki wao hasa katika michezo ya ligi kuu iliyosalia huku wakielekeza nguvu katika mchezo wao ujao dhidi ya Toto Africans utakaochezwa jijini Mwanza wiki ijayo.


No comments: