Na Juma Mohamed, Mtwara.
WANANCHI wa kijiji cha Lyowa, halmashauri ya wilaya ya
Mtwara wameonesha kukerwa na tabia ya mlinzi wa shule ya msingi Lyowa, Athuman
Naweka anaedaiwa kuwa na tabia ya kuomba chakula katika kila nyumba anaeishi
mwanafunzi wa shule hiyo.
Wananchi hao waliwasilisha malalamiko yao kupitia
mkutano wa hadhara ulioitishwa na mbunge wa viti maalumu mkoa wa Mtwara Tunza
Malapo, wakati wa kukabidhi bati 70 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya kijiji cha
Lyowa.
Wanadai kuwa mlinzi huyo ambaye waliingia naye mkataba
kwa ajili ya kulinda shule, ameanza kuwa na tabia hiyo mara baada ya serikali
kuja na mpango wa kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari.
“Mlinzi tumeingia naye mkataba kijiji cha Lyowa lakini
tangu Rais alipotangaza elimu bure mpaka leo hajalipwa pesa zake sasa mlinzi
anapata mashaka anapita nyumba hadi nyumba anakwambia mimi ni mlinzi nalinda
shule yenu na pesa sipati kwahiyo leo nimekuja kula kwako leo na akishakwambia
leo anakuja kula kwako hatanii ndivyo ilivyo amekuwa kama mwanafamilia wa
kijiji..”aisema Twalib Mtambula.
Diwani wa kata hiyo, Hassan Likutwe alisema tabia hiyo
inayofanywa na mlinzi huyo inatokana na kukosa mshahara hivyo wamedhamiria
kuitisha mkutano wa wananchi ili kuona namna ya kuondokana na tatizo hilo.
Alisema aliwahi kwenda nyumbani kwake na kumlalamikia
juu ya kukosa mshahara na namna anavyofanya kazi katika mazingira magumu lakini
alishindwa kumpa majibu ya moja kwa moja.
“Mimi aliwahi kuja kwangu kunilalamikia lakini
nilimwambia sina jibu la moja kwa moja kwasababu sasahivi hairuhusiwi mtu
yeyote kuchangishwa michango kwa ajili ya kupelekwa shule, kwahiyo nikamwambia
itabidi tuweke mkutano wa wananchi ili tupate ridhaa ya sisi wenyewe tujitoe
ili aweze kupata stahiki zake..”alisema Likutwe.
Kwa upande wake, mlinzi huyo alikiri kufanya kitendo
hicho na kudai kuwa ni kutokana na kutopata mshahara wake kwa miezi mitatu
amekuwa akilazimika kupita nyumba hadi nyumba ili kupata chakula kwani kila
anapodai mshahara anaambiwa asubiri pesa ya serikali.
“Ni kweli nagonga nyumba hadi nyumba kwasababu nalinda
shule yenye watoto wao, mimi sijalipwa mshahara wangu wa miezi mitatu kwahiyo
familia yangu inaishi kwa tabu na kila nikidai mshahara wangu shuleni naambiwa
nisubiri pesa ya Rais ambayo mimi sijui italetwa lini..” alisema Naweka
Katika hatua nyingine, mwalimu mkuu wa shule hiyo Oraf
Mlima, alisema shule inakabiliwa na uhaba wa walimu pamoja na nyumba za walimu
hali inayowafanya kuishi kwa mashaka hasa kipindi cha mvua kutokana na nyumba
zao kubomoka na hivyo kurudisha utendaji kazi nyuma.
“Kama mnavyoona mazingira ya nyumba zetu yalivyo ni
kwamba tunapata adha kubwa sana kwanza ukiangalia zimeengeshwa na miti
kwasababu zinadondoka na wakati wa mvua kama hivi zinavuja kwahiyo inatulazimu
kutoa mishahara yetu walau kuziba lile eneo tunalolala, hiki ni kilio cha
Tanzania nzima lakini katika mazingira yetu hali ni ngumu zaidi na hata
ufanyaji wa kazi kiutendaji unakuwa mgumu kutokana na mazingira.” Alisema.
Mbunge wa viti maalumu mkoa wa Mtwara, Tunza Malapo
alisema kutokana na hali za walimu kuwa mbaya zimekuwa zikiwapunguzia hari ya
kufanya kazi na kumtaka waziri
mwenye mamlaka kuangalia suala hilo upya.
“Tuache masihara tusichezee elimu, elimu ina mambo
mengi lakini mwalimu anatakiwa aishi viruzi alale sehemu nzuri ili kesho aamke
aende shule akafundishe kwa ustadi..walimu wana moyo wa kufundisha lakini
mazingira yanawarudisha nyuma..” alisema na kuongeza:
“Mimi kama mbunge nimejionea hali hii kwa macho yangu
nitalisimamia kuhakikisha yanapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwasababu hata mimi
nimetokea kwenye ualimu.” aliongezaMalapo.
No comments:
Post a Comment