Na Juma Mohamed, Mtwara.
WAGONJWA 500
watakaougua ugonjwa wa macho wa kufanyiwa upasuaji (Mtoto wa Jicho) watapata
matibabu bure katika Kliniki ya Macho iliyopo katika hospitali ya rufaa ya mkoa
wa Mtwara, Ligula kupitia mradi wa ujenzi wa Kliniki hizo unaotekelezwa na
shirika la Kikorea la Heart to Heart Foundation.
Akizungumza
juzi mkoani hapa katika hafla ya uzinduzi wa jengo la Kliniki hiyo, mkurugenzi
wa shirika hilo, Grece Lee, alisema jengo hilo lililogharimu zaidi ya dola za
Kimarekani 110,000 tayari limekamilika likiwa na vifaa vya kisasa kwa ajili ya
kutoa huduma za upasuaji wa macho (Mtoto wa Jicho).
Alisema,
pamoja na kukamilika kwa jengo hilo lakini amegundua kuwa mkoa wa Mtwara bado
unakabiliwa na changamoto kubwa juu ya mahitaji ya matibabu ya ugonjwa huo
ambapo alizunguka katika wilaya zote na kubaini uwepo wa changamoto hizo, hivyo
tayari amepanga andiko lingine atakalolituma serikali ya Korea kuomba ufadhili
kwa ajili ya mradi mwingine.
“Mimi nimeshapanga
mradi mwingine tayari sasa nitatuma serikali ya Korea na wakinijibu sawa,
tunaendelea na miradi yetu hapa Mtwara..kwahiyo kama ikiboreshwa huduma ya
macho mkoa wa Mtwara itapendeza, watu vijijini wa mjini wanoumwa macho wakipona
vizuri wataendelea na maisha yao vizuri..” alisema.
Alisema,
hali ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi katika maeneo mengi ya mkoa
wa Mtwara hasa ya vijijini ni ya shida sana huku ikichangiwa kwa kiasi kikubwa
na uhaba wa vituo vya afya, zahanati na ugumu wa maisha kwa wananchi na
kupelekea kushindwa kumudu gharama za matibabu.
“Kipato kule
vijijini watu wengine wanasema 5,000 wengine kwa mwezi 10,000 wengine kipindi
cha korosho wanasema labda wanapata 100,000 lakini bado haitoshi kwenda
hospitali kwenda kununua vitu..tukienda kwa wanafunzi zile kadi za afya watoto
wanazo mmoja mmoja shule nyingne wanayo kama nusu na wengine robo..” alisema.
Mratibu wa
huduma za macho katika mkoa wa Mtwara, Dkt. Upendo Abeid, alisema jamii ya
mkoani hapa bado ina uelewa mdogo juu ya ugonjwa huo ambao unaweza kupelekea
kuwa kipofu iwapo utachelewa kupata tiba.
“Kuna
magonjwa mengine unatakiwa kuja hospitali mapema ili uchunguzi ufanyike mapema
na kuweza kubaini tatizo lakini kwasababu uelewa wa jamii ni mdogo wanakuja
wakiwa wamechelewa kwahiyo wanapoteza macho yao na kutoona tena..” alisema.
Athuman
Bakari, ni mmoja wa watu waliowahi kuugua ugonjwa huo kwa kipindi kirefu na
kumfanya ashindwe kuona vizuri, lakini kwa sasa amepona tatizo hilo baada ya
kupata matibabu kutoka kwa wataalamu kupitia hospitali ya Ligula.
“Nilisikia
vyombo vya habari kwamba watu wa msaada wa upasuaji wa macho wapo pale Ligula
wanapasua macho kama ni mgonjwa basi nenda..mimi nikaja nikawakuta wataalamu
baada ya kunichunguza kweli nikakutwa na tatizo, nikafanyiwa upasuaji baada ya
muda kweli sasa hivi najisikia niko vizuri, naona na biashara zangu nafanya
vizuri..” alisema.
No comments:
Post a Comment