Tuesday, February 23, 2016

Manispaa ya Mtwara kuwafikisha mahakamani wakwepa kodi.

Wajumbe wa kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, kilichokuwa na ajenda moja ya kujadili bajeti ya halmashauri




Katibu wa kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Mtwara Mikindani, Donald Nssoko, akisoma taarifa ya makisio ya bajeti ya Manispaa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.


Na Juma Mohamed, Mtwara.

KATIKA kuhakikisha inakabiliana na changamoto ya ukwepaji kodi kwa wananchi, halmashauri ya manispaa ya Mtwara Mikindani imesema itachukua hatua za kisheria kwa kuwafikisha mahakamani wananchi wote watakaobainika kukwepa kulipa kodi ili kusaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kwa halmashauri hiyo, kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Mtwara Mikindani, Donald Nssoko, alisema mpango huo ni miongoni mwa mikakati waliyojiwekea kama kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hiyo.
Alisema kumekuwa na tabia hiyo kwa wananchi wengi wa manispaa hiyo hasa katika ulipaji wa kodi za majengo, jambo ambalo linachangia kurudisha nyuma utekelezaji wa bajeti ambao manispaa imekuwa ikijiwekea ikiwa ni pamoja na bajeti ya mwaka 2014/2015.
“Ili kukabiliana na changamoto hiyo, halmashauri ya manispaa ya Mtwara Mikindani tumejiwekea mikakati na miongoni mwa mikakati hiyi ni pamoja na kutoa elimu ya ulipaji kodi kwa wananchi, kuchukua hatua za kisheria kwa wananchi hasa wale wasiolipa kodi za majengo na kuhakikisha vyanzo vyetu vya mapato vinaongezeka..” alisema.

Wajumbe

Alitaja changamoto nyingine zinazoikabili halmashauri katika utekelezaji wa bajeti zake kuwa ni pamoja na kupanda kwa gharama za vifaa mbalimbali hasa vya ujenzi na kukwamisha shughuli nyingine za kuboresha miundombinu ya halmashauri hiyo.
Aidha, alisema halmashauri hiyo imejiwekea mipango mbalimbali ya kimaendeleo na kwamba miongoni mwake ni kuwawezesha kiuchumi wananwake, vijana na makundi mengine kwa kuwapataia mikopo kwa ajili ya kuwainua katika shughuli zao.
Mipango mingine ni kuboresha miundombinu ya barabara za manispaa kwa kufanya marebisho ya mara kwa mara, kuboresha huduma za afya, kuongeza upatikani wa maji safi na salama pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka sh. Bilioni 3 mpaka bilioni 4 kwa mwaka.
Katika hatua nyingine, wajumbe wa baraza hilo walifikia hatua ya kupiga kura za ndio na hapana kwa ajili ya kamuamua ni shule ipi kati ya shule ya msingi Ufukoni na Mjimwema inapaswa kuongezewa madarasa ambapo shule hizo zote zinamahitaji yanayofanana.
Shule ya msingi Ufukoni imepangiwa kuongezewa madarasa mawili huku Mjimwema ikipangiwa kuongezewa darasa moja, ambapo baadhi ya wajumbe walipendekeza shule zote ziongezewe madarasa mawili ili ziwe sawa kutokana na kukabiliwa na changamoto za uhaba wa vyumba hivyo, na kwamba baada ya upigaji kura, wajumbe walipiga kura za hapana walishinda.
Katika bajeti iliyopangwa na Manispaa hiyo, fedha zimegawanywa katika vifungu viwili ambapo asilimia 40 ya fedha hizo za makisio kwa bajeti ya 2016/2017 ambazo ni sh. bilioni 36, zitakuwa ni kwa matumizi ya ofisi huku asilimia 60 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.








No comments: