Sunday, February 21, 2016

Ndanda walipa kisasi kwa 'Wanakimanumanu' Nangwanda Sijaona.



Hekaheka katika lango la African Sports


Mlinzi wa African Sports, Rahimu Juma akimiliki mpira mbele ya Omari Mponda wa Ndanda.


Mlinda mlango wa African Sports, Kabari Faraji, akiwa katika harakati za kuokoa mpira uliokwenda wavuni kufuatia pigo la penalt lililopigwa na Omari Mponda na kuipatia goli la kuongoza Ndanda.


Wachezaji wa Ndanda wakishangilia goli la pili na la ushindi kwa timu yao.



Na Juma Mohamed, Mtwara.
TIMU ya soka ya Ndanda Fc ya mkoani hapa kwa mara nyingine imewatoa kimasomaso mashabiki wao baada ya kuwalaza na viatu African Sports ya Tanga kwa kuwachapa magoli 2-1 katika mchezo wa ligii kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika katika uwanja wa Nangwanda Sijaona.
Ndanda wakiwa chini ya kocha msaidizi, Mussa Mbaya akisaidiwa na Nahodha wa kikosi hicho, Wilbert Mweta, walianza mchezo kwa kasi huku wakipiga pasi fupi na ndefu pale inapobidi na kujaribu kutengeza nafasi kadhaa langoni mwa wapinzani wao lakini mara kadhaa washambuliaji Omary Mponda na Atupele Green walishindwa kuzitumia.
Huku mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro, ukiwa karibu na kwenda mapumziko, Ndanda walipata penalt iliyotokana na mchezaji mmoja wa African Sports kuunawa mpira katika eneo la hatari, ambapo mpigaji Omary Mponda hakufanya hajizi baada ya kupiga mkwaju mkali uliomshinda mlinda mlango Kabari Fraji, na kuifanya Ndanda iende mapumziko ikiwa na goli hilo la kuongoza.

Mlinda mlango wa African Sports, Kabari Faraji, akiwa katika harakati za kuokoa mpira uliokwenda wavuni kufuatia pigo la penalt lililopigwa na Omari Mponda na kuipatia goli la kuongoza Ndanda.


Kipindi cha pili timu zote zilicheza kwa kushambuliana huku Ndanda wakionekana kupata kona nyingi ambazo hazikuweza kuwasaidia, huku wapinzani wao wakicheza kwa mipira mirefu ambapo walifanikiwa kufika langoni mwa Ndanda mara chache kabla ya kupata penalt katika dakika ya 79 kutokana na Salvatory Ntebe kufanya madhambi ndani ya eneo la hatari, ambapo Ally Ramadhani aliisawazishia A. Sports na kufanya matokeo kuwa goli 1-1.
Kufuatia kucheza madhambi katika eneo la hatari, Salvatory Ntebe alionyeshwa kadi ya njano na Martin Saanya lakini haikuifanya ngome ya Ndanda itetereke huku mlnzi kisiki, Kasian Ponera akionekana kufanya kazi kubwa leo kuwazuia washambuliaji wa Sports.
Baada ya Sports kusawazisha goli, Ndanda walionekana kucharuka na kufanya juhudi za kuongeza goli la pili huku mshambuliaji aliyeingia dakika 59 Salum Minelly aliyechukuwa nafasi ya Omary Mponda, akikosa nafasi nyingi za wazi ambazo angeweza kuipatia timu yake mabao mengi.

Wachezaji wa Ndanda wakimnyamazisha mwenzao, Salum Minelly, aliyekuwa akilia baada ya timu yake kufunga goli la pili, kutokana na yeye kupoteza nafasi nyingi za wazi.


Mabadiliko mengine kwa Ndanda yalikuwa ni ya kumtoa Bryson Raphael na Paul Ngalema aliyeumia na nafasi zao kuchukuliwa na Ahmad msumi na Buruhan Rashid, huku Sports wakiwatoa Fadhili Kizenga, Hussein Isa na Hamad Mbumba na nafasi zao kuzibwa na Hassan Materema, Ally Ramadhani na Maulid Abasi.
Mabadiliko hayo yalionekana kuwa na manufaa kwa Ndanda ambapo katika dakika 3 za nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika, kiungo Kigi Makasi aliwainua tena mashabiki wa Ndanda baada ya kupachika goli la pili na la ushindi kufuatia pasi fupi walizogongeana wachezaji ndani ya eneo la 18.

Furaha ya goli la ushindi


Baada ya mchezo, mwalimu wa Ndanda, Mussa Mbaya alisema wachezaji wake walipambana na kuweza kupata matokeo hayo ingawa alikiri kuwa mchezo ulikuwa ni mgumu.
Alisema baada ya mchezo huo, hakuna kulala na kwamba vijana wake wataendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiandaa kwa mchezo wa kombe la Azam Sports Federation Cup (FA), ambapo watacheza na JKT Ruvu Februari 26 katika uwanja wa Nangwanda.
Kwa matokeo hayo, Ndanda inapanda mpaka nafasi ya Nane katika msimamo wa ligi kwa kufikisha alama 23 baada kucheza mechi 20 wakiwa juu ya Toto Africans ya Mwanza yenye alama 22.

MATOKEO MECHI ZINGINE

Majimaji   1-0  Mtibwa Sugar

Mwadui    2-1  Coastal Union





No comments: