Monday, February 22, 2016

Wananchi Newala walalamikia ukosefu wa dawa.

Mmoja wa wakazi wa kata ya Kitangali wilayani Newala akiwasilisha malalamiko yake juu ya kero za huduma za afya wanazozipata wananchi.




Na Juma Mohamed, Newala.

WANANCHI Wilayani Newala wamelalamikia ukosefu wa dawa katika vituo vya afya na Zahanati na kudai kuwa hali hiyo inachangia watu wengi kutoona haja ya kujiunga katika Mifuko ya Afya ya Jamii (CHF).
Wakizungumza katika uzinduzi wa Kitaifa wa uhamasishaji wa mfuko wa Afya ya Jamii CHF Mkoa wa Mtwara, uliofanyika katika Kata za Kitangali na Chiwonga wilayani humo,  wananchi hao wamesema hali hiyo inawavunja moyo wananchi ambao wengi wao wana kipato cha kawaida.
“Wakazi wa kijiji cha kitangali au kata kwa ujumla, wako tayari kujiunga na huduma ya afya lakini tatizo ambalo watu wamelichanganua na mimi naomba nilizungumzie hapa, baada ya watu kujiunga hata wawe 29 wakishafika kwenye kituo kile baada ya kupata huduma wanaambiwa kwamba sisi hatuna dawa, nendeni kwenye maduka ya madawa huko pembeni mkanunue..” alisema Ismaili Makelele, mkazi wa Kitangali.
Alisema suala hilo linawakatisha tamaa kwa wale waliojiunga na wengine ambao wanatarajia kujiunga, kwasababu wanajiunga kwa kujua kuwa watapata huduma kwa ubora wakiwa na familia zao.
Kwa uapande wake Mkuu wa wilaya ya Newala, Christopher Magala,ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, aliwataka wananchi wa Kata hizo, kuona umuhimu wa kijiunga na mfuko huo na kuwasisitiza kuwa ugonjwa unapoingia mwilini kwa mtu hauwezi kubisha hodi.
“Niwaombe sana, hujui ni lini utaugua jiungeni na mfuko wa afya ya jamii ndio mkombozi wa utoaji wa huduma vijijini, na nitoe rai kwa wenzetu wa mfuko wa NHIF, kwanza niwapongeze kwa kuendelea kusimamia vizuri utoaji wa huduma za afya lakini niwaombe mwendelee kusaidia sekta hii ya afya na hasa ukuaji wa huduma za afya vijijini kwa kuwajengea uwezo..” alisema.
Naye, mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Newala, Maimuna Mtanda, alisema lengo la mfuko huo ni kuwafanya wananchi wachangie huduma ya afya na sio lazima watoe michango yao kwa mkupuo bali wanaweza kuchangia kwa awamu.
“Inawezakana mtu kutoa 10,000 kwa pamoja ikashindikana kutokana na majukumu tuliyonayo, peleka 5,000 tafuta tena 5,000 peleka kamilisha..nimesema hivyo kwasababu inawezekana leo una 10,000 mfukoni siku ugonjwa unakuja hauna hata shilingi, inawezekana ukasema nitaenda kumkopa Fulani naye hana..” alisema.







No comments: