Wachezaji wa Yanga wakishangilia goli, katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Simba. Yanga walishinda magoli 2-0 |
Na Juma Mohamed.
KWA mara
nyingine, wekundu wa Msimbazi timu ya Simba Sc leo imeshindwa kutamba mbele ya
watani wao Yanga Sc baada ya kukubali kichapo cha magoli 2-0 katika mchezo wa
ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliofanyika katika uwanja wa Taifa, jijini
Dar es Salaam.
Simba
walianza mchezo vizuri wakicheza kwa pasi fupi kama kawaida yao na kutengeneza
nafasi kadhaa langoni mwa Yanga ambao leo safu yao ya ulinzi iliyoongozwa na
Mbuyu Twite na Vicente Bosou ilionekana kuyumba katika dakika za mwanzo kwa
kufanya makosa ambayo hata hivyo Simba walishindwa kuyatumia.
Mambo yalianza
kwenda kombo kwa Simba mapema tu ambapo katika dakika ya 34, mlinzi wa kati
Abdi Banda alitolewa nje kwa kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi ikiwa ni kadi
ya pili ya njano akiipata muda mfupi baada ya kuonyeshwa kadi ya njano ya
kwanza, na kuifanya Simba kucheza pungufu.
Baada ya
hapo walianza kuyumba kwa kucheza bila maelewano na kupoteza hali ya kujiamini
ambapo katika dakika ya 39, mlinzi wa pembeni, Kessy Ramadhani alijikuta
akiwazawadia Yanga bao la kuongoza baada ya kufanya makosa ya kupiga pasi fupi
ya kuurejesha mpira kwa golikipa wake, Vicente Agban, ambao uliwahiwa na kiungo
wa Yanga, Donald Ngoma na kumlamba chenga kipa kasha kuukwamisha mpira wavuni.
Dakika 45 za
kwanza zikamalizika kwa Yanga kwenda mapumziko wakiwa kifua mbele kwa mtaji wa
goli moja la kuongoza.
Kipindi cha
pili Simba walirudi kwa kucheza kwa tahadhali huku wakiimarisha safu ya kiungo
na mbele kumwacha Hamisi Kiiza pekeake ambapo walijaribu kupanga mashambulizi
yao wakilazimisha kupita katikati jambo ambalo lilionekana kuwa gumu kwao hasa
baada ya wapinzani wao kuimarisha sehemu yao ya kiungo.
Dakika ya
79, Yanga walipata goli la pili kupitia kwa Amis Tambwe, aliyeunganisha krosi
ya Geofrey Mwashiuya aliyeingia kuchukuwa nafasi ya Harouna Niyonzima ambaye
aliumia, bao ambalo lilidumu mpaka mwisho wa mchezo.
Kwa matokeo
hayo, Yanga anarudi kileleni mwa ligi akiwa na alama 46 baada ya kucheza mara
19 huku Simba akirudi mpaka nafasi ya Tatu kwa kusalia na alama zake 45
ambapo sasa Azam ambao baada ya kushinda leo dhidi ya Mbeya City wamefikisha
alama 45 lakini wakiwazidi Simba magoli ya kufunga na kufungwa.
No comments:
Post a Comment