Thursday, November 12, 2015

Wananchi wakosa huduma RITA Mtwara


Neema Namangaya, mkazi wa Mtwara vijijini ambaye anafuatilia cheti cha kuzaliwa cha mwanaye katika ofisi ya Wakala wa Usajili wa Vizazi na Vifo (RITA) mkoa wa Mtwara.



Neema Namangaya



Afisa Tawala wa wilaya ya Mtwara, Edith Shayo, akitolea ufafanuzi juu ya malalamiko ya wananchi kuhusu adha wanayoipata katika kufuatilia vyeti vya kuzaliwa vya watoto.


Na Juma Mohamed.

WANANCHI wa halmashauri ya Mtwara vijijini wamepaza sauti zao kuulalamikia uongozi wa Wakala wa Usajili wa Vizazi na Vifo (RITA) mkoa wa Mtwara, kutokana na usumbufu wanaoupata katika ufuatiliaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wachanga.
Wananchi hao ambao wanalazimika kusafiri kutoka vijijini kufuata huduma hiyo katika manispaa ya Mtwara Mikindani, walisema wanajikuta wanatumia gharama kubwa ya fedha katika nauli na kujikimu wanapokuwa mjini hapa kwa ajili ya kusubiri kwa kufuata maagizo wanayopewa na wahusika.
Wakizungumza juzi wakiwa nje ya ofisi hiyo, walisema mara kadhaa wamekuwa wakitekeleza bila mafanikio, maagizo wanayopewa na wahusika kwa kuwapangia tarehe za kupatiwa vyeti hivyo lakini inashindikana kutokana na ofisi kuwa inafungwa kila wanapofika na kukosa mtu wa kuwahudumia.
Husna Mohamed, mkazi wa kijiji cha Nanguruwe, alisema alianza kufuatilia cheti kwa ajili ya mwanaye tangu miezi sita iliyopita lakini bado hajafanikiwa na kwamba kila akifika ofisini hapo anapangiwa tarehe.

Liliane Vicent, mkazi wa Mtwara vijijini akizungumzia namna anavyokumbana na vikwazo katika kufuatilia cheti cha mtoto wake, katika ofisi ya Wakala wa Usajili wa Vizazi na Vifo (RITA) mkoa wa Mtwara.

“Tunashindwa kuwaelewa kwasababu sisi tunatumia nauli na maisha magumu, ndio maana sisi hatuwaelewi hawa watu..na sisi tumefikia sehemu za watu mjini hapa, tutakula nini anaposema tusubiri mpaka Jumatatu na lao Al-Hamis (juzi)..na sheria za kazi Al Hamisi mtu anakuwa kazini sasa tunamshanga sijui Babu sijui kijana aliko huko tunashangaa kila tukifika hapa hayupo..” alisema.
Alisema ofisi hiyo ilifungwa na hakukuwa na mtu isipokuwa walijibiwa na mtu wa ofisi nyingine (hakumtaja jina) kuwa mwenyewe hayupo na kuwataka warudi tena siku ya Jumatatu.
Alisema, ofisi hiyo imeanza kufungwa tangu mwezi Agosti mwaka huu baada ya kuanza kwa kampeni za Uchaguzi mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais uliofanyika mwezi Oktoba, kutokana na muhusika kuamua kujiingiza katika siasa.
“Yani tangia mwezi wa Nane kipindi cha kampeni kile, pale hapakuwa na mtu ukifika tu unaambiwa pamefungwa hayupo, mwenyewe amesafiri..zamani hapo alikuwa anafanya kazi ila baada ya kuanza kampeni mpaka hatua hii hafanyi kazi, pale pamefungwa nendeni mkapige picha tu muone..” aliongeza Husna.
Naye Liliane Vicent, alisema alianza kufuatilia toka mwezi June ambapo mpaka sasa bado hajafanikiwa kupata cheti jambo ambalo linampa gharama kubwa ya nauli kutokana na namna anavyopangiwa tarehe za kurudi kila baada ya mwezi huku kukiwa hakuna mafanio yoyote.

Neema Namangaya

“Toka mwezi wa sita nikja hapa naamibwa uje mwezi wa Saba, nilipofika sikupata nikaambiwa mpaka mwezi wa Nane, nilipofika mwezi wa Nane sikupata nikaambiwa njoo mwezi wa Tisa, nilipofika sijamkuta..basi yakaanza masuala ya uchaguzi nikaona haina jinsi nikaamua kubaki nyumabni..” alisema.
Kwa upande wake, Afisa Tawala wa wilaya ya Mtwara, ambako ndiko kuna ofisi hiyo, Edith Shayo, alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi hao na kusema kuwa mara kadhaa anajitahidi kutoka na kuwaeleza changamoto walizo nazo zinazosaabisha ofisi kufungwa na wao kukosa huduma.
Alisema, ofisi hiyo ina mtumishi mmoja hadi sasa ambaye anafanya kazi zote na kwamba akipatwa na dharula basi ofisi inafungwa kutokana na kukosa msaidizi huku akisema kuwa mtumishi aliyekuwepo awali alijiingiza katika masuala ya kisiasa kwa kugombea Udiwani katika kata moja ambaye hakuitaja.

Edith Shayo

Alisema kutokana na maamuzi yake hayo ambayo yalimuondoa moja kwa moja katika utumishi wa Wakala hiyo ya Serikali, walilazimika kumtafuta mtu mwingine ambaye walimuelekeza namna ya kutekeleza majuku ya ofisi hiyo, ambapo baada ya kujiridhisha kuwa anaweza kufanya wakamkabidhi ofisi ambapo anaendelea na kazi hadi sasa lakini toka wiki iliyopita alisafiri kwenda jijini Dar es Salaam kwa ajili ya masuala ya kiofisi.
“Nafikiri ni toka Al Hamisi iliyopita alisafiri kuna kikao huko Dar es Salaam kwa masuala hay ohayo ya RITA, kuna stakabadhi amepeleka walimuita wenyewe, na ndio maana umeona ofisi imefungwa..ni kweli watu huko nje unasikia wakilalamika na binafsi hua natoka na kuwaeleza, unajua sisi ni binadamu unakuta mtu anakuja amesimama mda mrefu ..hata juzi mimi nilikua hapa si unajua watu wanajazba..” alisema.
Kuhusu usumbufu wa kurudishwa mara kwa mara kwa kupangiwa tarehe za kufuata vyeti kwa wananchi, alisema alikuwa hafahamu chochote juu ya changamoto hiyo na kudai kuwa ndio ameisikia kwa mara ya kwanza, na kutaka kumafahamu mwananchi aliyetamka hayo ili aweze kuongea mbele yake.
Aliwataka wananchi kufika katika ofisi yake kueleza iwapo wanakumbwa na changamoto kama hizo na sio kuishia kulalamika wakiwa wenyewe bila kupata ufafanuzi kwa wahusika.


No comments: